Faith Fennidy: Nywele za binti huyo zenye asili ya kiafrika zimezua mjadala katika mitandao ya kijamii Louisiana, Marekani

Faith Fennidy

Chanzo cha picha, STEVEN FENNIDY/FACEBOOK

Maelezo ya picha, Faith Fennidy, akifuta machozi baada ya kushambuliwa kwa maneno kuhusu nywele zake

Video moja iliyotandaa mitandaoni inamuonesha msichana akiondoka shuleni kwasababu ya kuvunja sheria za shule imezua mjadala katika mitandao ya kijamii juu ya ubaguzi na ukosefu wa ufahamu kuhusu nywele za watu weusi.

Msichana huyo ana umri wa miaka kumi na mmoja anaitwa Faith Fennidy, anaonekana kwenye video hiyo iliyowekwa kwenye mtandao pendwa wa facebook, anaonekana akifuta machozi huku akikusanya vitu vyake katika shule ya Christ the King Parish iliyoko Terrytown, Louisiana.

Mama wa binti huyo Montrelle amemtaka mwalimu aeleze kwanini rasta za mwanawe zilizofungwa nyuma ya kisogo chake, ni kwa namna gani zimekuka sera za shule.

Shule hiyo ya binafsi imetoa msimamo wake kwa kueleza kuwa wasichana hawapaswi kuongeza chochote katika nywele zao iwe rasta ama wigi zinazotumika kuongeza urefu wa nywele.

Katika taarifa yake kwa BBC,jimbo la New Orleans limeeleza sera za shule zinaelekeza kila msichana kuwa na nywele zake za asili na si vinginevyo.Sera hii imewekwa bayana kwa wazazi wote wakati wa likizo na kabla ya kufunguliwa kwa shule, na inawahusu wanafunzi wote.

Familia ya binti huyo inafikiria kupata usaidizi wa kisheria kwa kilichotokea na kwamba wanafikiria kumhamisha mtoto wao katika shule hiyo na kwenda kusoma kwingine.

Kaka wa binti huyo aitwaye Steven, ndiye aliyerusha video hiyo katika mtandao wa Facebook, mapema wiki hii, akielezea kukerwa kwake kutokana na uelewa finyu juu ya nywele za watu weusi ikiwemo utunzaji wake.

Steven anasema, kuwa rasta zilizoongezwa kwenye nywele za dadake zinamsaidia na ni rahisi kwa utunzaji na kumpa nafasi dada yangu aweze kuogelea kirahisi na baada ya hapo hatalazimika kuzitengeneza kila usiku," alisema.

Anaendelea kushangaa kwamba kwanini sera ziwekwe bila hata majadiliano? Hii ndiyo sababu nasema hamjali na ndiyo njia mojawapo ama niite kikwazo cha kuwafanya watu weusi wasisome katika shule hiyo.Mtazamo wa Steven umesomwa na watu nusu milioni na kusambazwa mara elfu sitini na moja.

mwanamuziki T.I

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanamuziki T.I ameandika ujumbe katika mtandao wa Instagram akishutumu kisa hicho

Suala hili pia limeonekana kupata mjadala katika mtandao wa Instagram baada ya mwanamuziki T.I kurusha mtazamo wake akiilaumu shule hiyo ya Christ the King Parish, na kutoa wito kwa familia ya Faith endapo watahitaji msaada wake yuko tayari kusaidia.

T.I anasema huyu binti ni mrembo na nywele zake ziko sawa na hazina tatizo vinginevyo kuna suala lisilo la kawaida dhidi ya nywele za watu weusi anamaliza kusema T.I