Je, Ronaldo atairudisha Serie A katika umaarufu wake wa zamani?

Cristiano Ronaldo aliwahi kushinda tuzo za mchezaji bora wa dunia mara tano
Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo aliwahi kushinda tuzo za mchezaji bora wa dunia mara tano

Ligi ya Serie A haiwezi ikawa ni ya mtu mmoja tu, haijawahi kuwa hivyo na haitakaa kuwa ya Cristiano Ronaldo pekee.

Hatahivyo, ni ngumu sana kudharau namna gani kuhamia kwake katika timu ya Juventus kumeleta kishindo katika ligi hiyo hata kabla ya mpira kuanza kuchezwa.

Ronaldo mwenye miaka 33 na mshindi mara tano wa tuzo za mchezaji bora wa dunia, Ballon d'Or, si tu ni mmoja ya wachezaji bora wawili wa mpira wa miguu katika mwongo uliopita bali ni mmoja ya watu maarufu kabisa duniani kwa sasa.

Katika mitandao ya kijamii, Ronaldo anawafuasi milioni 313 na yawezekana kabisa umati huu mkubwa wa watu sasa utaelekeza macho na masikio yao kuelekea Serie A.

"Hatimaye dunia inaiongelea ligi ya Italia tena," kocha maarufu wa Italia Fabio Capello ameliambia gazeti la Gazzetta dello Sport. "Katika miaka ya 80 na 90 sisi (Italia) tuliwakilisha ubora na umaarufu, halafu tukapotea na tukashindwa kuwekeza katika miundombinu ya kuturudisha juu."

"Kwa kuwa na Ronaldo sasa twaweza kujaribu kunyanyua vichwa juu, lakini hilo pekee halitoshi, tunahitaji kutumia weledi wa hali ya juu kutumia mshawasha wa Ronaldo ili kuupa mchezo wetu uhai kwa mara nyengine," amesema Capello.

Makubaliano katika vyombo vya habari ni kuwa uhamisho wa Ronaldo kutoka Real Madrid ya Uhispania kwenda Juve uliogharimu pauni milioni 99.2 ni hatua muhimu zaidi iliyochukuliwa katika harakati za kuirejesha Serie A katika umaarufu wake wa zamani.

"Kilele klilikuwa mwaka 2003 pale tulipoingiza timu zetu mbili katika fainali ya klabu bingwa bara Ulaya," amekumbushia kocha wa zamani wa Juve Claudio Ranieri, alipoongea na gazeti la Stampa. "Hatujarejea katika zama zile bado, lakini nahisi siku za unyonge zimefikia tamati."

Je, Ronaldo atamnufaisha nani zaidi?

Je,Ronaldo anaifaidisha ligi yote ama Juve pekee

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ronaldo mwenye umri wa miaka 33

Ni Dhahiri kuwa Ronaldo amerejesha matumaini. Hatahivyo, kumekuwa na mjadala mkali kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa ambapo swali kuu ni;

Je,Ronaldo anaifaidisha ligi yote ama Juve pekee?

Cristiano Ronaldo akisalimia mashabiki wa Juventus uwanja wa Allianz

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo akisalimia mashabiki wa Juventus uwanja wa Allianz

Kwa upande wa mapato, washindani wa Juve tayari wameanza kuongeza gharama za tikiti na kufanya mashabiki wa Juve kupinga ongezeko hilo ambalo litawafanya warudi mifuko mitupu kila mara timu yao itakapokuwa uwanja wa ugenini.

Lakini inaonekana timu nyengine hazina namna bali kumtumia vizuri Ronaldo kimapato. Mchezaji bora wa dunia akienda Ferrara, Frosinone na Sassuolo tiketi lazima ziwe pesa juu.

Hata kabla ya ujio wa Ronaldo, Juve ambao pia wanajulikana kama 'Kibibi kizee' wamechukua ubingwa wa Serie A kwa misimu saba mfululizo.

Msimu uliopita, 2017/18 walichukua kwa tofauti ya alama nne juu ya Napoli na Roma wakashika nafasi ya tatu.

Nahodha wa Roma Daniele De Rossi kwa kuonesha kukata tamaa na mwenendo wa Juve alisema: "Wameshaiua ligigi kidogo."

Inter wanaonekana kuwa wapo tayari kupambana kikamilifu na Juve msimu ujao baada ya kuwasajili wachezaji nyota kama Stefan de Vrij, Radja Nainggolan, Sime Vrsaljko na Keita Balde Diao.

Kwa upande wa Napoli wao wameweza kumnyakua kocha maarufu Carlo Ancelotti ambaye amewika na vilabu kama AC Milan, Real Madrid na Bayern Munich. Ancelotti alishinda pamoja na Ronaldo klabu bingwa Ulaya wakiwa na Real mwaka 2014, sasa anakibarua kigumu kupeleka mafanikio Napoli.

Roma walikuwa na msimu mzuri nje ya Italia pia kwa kufika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya na wameongeza nguvu ya kikosi chao kwa kuwasaini wachezaji makinda na machahchari kama Justin Kluivert na Ante Coric. Pia wamenyakua wachezaji wazoefu na mahiri kama Javier Pastore na kiungo Steven N'Zonzi ambaye alikuwa ni sehemu ya kikosi cha timu ya Ufaransa iliyoshinda kombe la dunia nchini Urusi.

Mwisho wa siku, licha ya kumsajili Ronaldo, bado Juve watakuwa na wakati mgumu kutetea ubingwa wa ligi kwa mara ya nane mfululizo.

Kwa upande wa ligi ya Serie A kwa ujumla wake, bado kuna matatizo na kashfa nyingi ambazo zimekuwa ni kielezo cha mpira wa Italia. Ronaldo bila shaka atakuwa kielezo pia cha Serie A.

"Kuna maisha zaidi ya Cristiano Ronaldo," gazeti la Corriere dello Sport limeandika.