Fatuma Ahmed: Wanawake hutekeleza mchango muhimu vitani katika jeshi

Fatuma Ahmed
    • Author, John Nene
    • Nafasi, BBC Swahili

Mwanamke wa kwanza kupanda ngazi hadi Meja Jenerali katika Jeshi la Kenya, Fatuma Ahmed, amekosoa dhana ya wanawake kutohusishwa kikamilifu jeshini.

Fatuma hivi majuzi aliweka historia alipopandishwa ngazi na kuwa mwanamke wa kwanza nchini Kenya kushikilia wadhifa wa Meja Jenerali. Kabla ya hapo alikua Brigedia.

Anasema wanawake siku hizi jeshini wanafanya kazi yoyote ile wanaume wanatekeleza.

Fatuma alipokuwa anapandishwa cheo aliteuliwa Msaidizi wa Mkuu wa Majeshi anayeangazia wafanyakazi na mipango katika majeshi ya Kenya.

Je, wako mstari pia vitani pia kwa mfano kule Somalia dhidi ya Al-Shabab?

"Wanajeshi wetu wanawake wako kote huko," anasema Bi Fatuma.

"Kama ni kusafirisha silaha huko Somalia wanahusika, kuendesha vifaru wako ndani, na tena vita vya Somalia si vya mashambulizi hapa na hapa ni vya akili na sisi wanawake tuna akili pia ya vita.

Je, mwenyewe amewahi kuwa mstari wa mbele vitani.

"Bado sijakuwa huko lakini nimehusika na kulinda usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na New York huko Marekani."

Fatuma Ahmed

Fatuma anasema endapo kuna vita na anahitajika kuwa mstari wa mbele atajitosa uwanjani.

"Hiyo ndio kazi nimefunzwa na sitasita kuongoza nikiwa mbele vitani. Hapo unajua ni vita viwili, adui akumalize ama ummalize na nitamwangusha adui mara moja kutetea nchi yangu."

Meja jenerali huyo anasema vitani, hata kama yeye ni mwanamke, hana huruma.

"Wakati wa vita hakuna huruma ama kupendana, hata kama si mimi nashambuliwa nione wanavamia mwenzangu nafyatua risasi mara moja na kumuangusha adui."

Kuhusu cheo chake kipya cha Meja Jenerali, Fatuma anaeleza: "Nahusika na usafirishaji na ugavi wa rasilimali na ununuzi wa kila kitu hapa na kujua ni kitu gani wenzetu kule nje wanataka."

"Wajua mimi niko makao makuu ya jeshi, nahakikisha vifaa vinafika kwa wenzetu nje kama ni vita nashughulikia kila kitu watakacho. Kazi yetu ina vitengo vingi."

Meja Jenerali Fatuma Ahmed alipokuwa anapandishwa cheo

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Maelezo ya picha, Meja Jenerali Fatuma Ahmed alipokuwa anapandishwa cheo

Ni miaka 32 sasa Fatuma yuko jeshini. Kwanza alikua katika kile kitengo cha wanawake kijulikanacho kama Women Service Corps na kilipovunjwa mwaka wa 1972 akahamia jeshi la angani.

"Mimi mwenyewe nilijiunga na jeshi mwaka 1983 bila kushurutishwa na mtu. Niliposikia wanakuja kuchukua watu kule Meru nilijaribu bahati yangu nikachukuliwa. Watu wangu walishangaa sana wakajaribu kunishawishi nitoke lakini singeweza kuacha kazi. Kwetu sikutoka kwa watu wanajiweza sana kifedha. Sasa wanafurahia sana nilivyopiga hatua kubwa."

Mtanzania alitangulia

Fatuma ni mwanamke wa pili Afrika Mashariki kuwa Meja Jenerali, wa kwanza ni Zawadi Mdawili wa Tanzania mwaka wa 2007.

Mumewe Fatuma, George Owino ni mwanajeshi. Naye pia ni Meja Jenerali.

Akiwa nyumbani Fatuma anasema anampa Owino heshima kama mkuu wa nyumba.Nikiwa nyumbani napenda kupika wali lakini ugali lazima maanake mume wangu bila ugali haoni kama amekula.Wali yuala pia lakini ugali lazima.Wana watoto watatu, na kuhusu mtandio kama mwanamke wa Kiislamu, Fatuma anasema akiwa nje ya ofisi anajifunga mtandio kawaida.

"Ukiona hutajua ni mimi kabisa navaa kama mwanamke Mwislamu."

Kwa jumla anafurahia maendeleo ya wanawake jeshini.

"Polepole wanawake tunapanda ngazi na siwezi kusema tumefikia wanaaume maanake kwa mfano hapa Kenya tulianza kuhusishwa nyanja zote mwaka 2000."