Wakaazi waokota kilichosalia katika bomoa bomoa Kibera Kenya

kibera
Maelezo ya picha, Hii ni awamu ya pili ya ubomoaji wa makaazi ya watu zikiwemo pia shule na maeneo ya biashara

Shughuli ya kuondoa wakaazi kwa lazima imeanza katika mtaa wa mabanda wa Kibera - Nairobi Kenya.

Oparesheni hiyo imeendeshwa chini ya ulinzi mkali huku maafisa wa usalama wakishika doria wakati makaazi, shule na majengo ya biashara yakibomolewa.

Hatua hii inanuiwa kutoa nafasi ya upanuzi wa barabara inayotarajiwa kupunguza msongamano wa magari katika mji mkuu Nairobi.

Maelfu ya waathirka ni maskwota ambao wamelalamika kuwa shughuli hiyo imefanyika bila kuzingatia ubinadamu na wameomba kupewa makao au kulipwa fidia - maombi ambayo serikali imepuuza.

Wakaazi waokota kilichosalia katika bomoa bomoa Kibera
Maelezo ya picha, Wakaazi wamepewa ilani ya kuyahama makaazi yao kutoa nafasi ya ujenzi wa barabara

Zaidi ya familia elfu ishirini zinaathirika na mpango huo.

Serikali inasema tayari ilikuwa imetoa taarifa kwa wakaazi hao na walipaswa kuondoka tangu katikati ya mwezi huu wakitakiwa kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara itakayo liunganisha eneo la Mashariki na Magharibi mwa jiji hilo.

Serikali inasema inaimiliki ardhi hiyo inayozozaniwa na kwamba hakuna mtu atakayelipwa fidia.

ramani

Imeeleza kuwa barabara hiyo kuu yenye thamani ya $ milioni 20 inayojengwa katikati ya mtaa wa Kibera imenuiwa kupunguza msongamano wa magari magharibi mwa mji mkuu Nairobi.

Wamiliki wa Shule na biashara kadhaa katika eneo hilo ni miongoni mwa waliopewa ilani za kuondoka.

Sarah Bisebe, anayekiendesha kituo cha mafunzo kwa watoto wasiojiweza Egesa - ameiambia BBC kuwa ilani ya kuondoka ilitumbukizwa chini ya mlango usiku.

Ameelezea wasiwasi wake kwamba huenda ndio mwisho kwa watoto katika taasisi hiyo kupata elimu.

Maelfu ya waathirka ni maskwota ambao wamelalamika kuwa shughuli hiyo imefanyika bila kuzingatia ubinadamu na wameomba kupewa makao au kulipwa fidia
Maelezo ya picha, Maelfu ya waathirka ni maskwota ambao wamelalamika kuwa shughuli hiyo imefanyika bila kuzingatia ubinadamu na wameomba kupewa makao au kulipwa fidia

Sio mara ya kwanza kwa shughuli ya ubomozi au kufurushwa kwa watu kutoka ardhi ya umma kufanyika Kenya.

Hali hii imezusha maswali mengi kuhusu majukumu ya wabunge ambao wanatunga sheria na sera hizo.

Haya ni wakati hali ya wanaopoteza makaazi yao hawajui waelekee wapi na vilevile kuzusha maswali kuhusu tatizo la unyakuzi wa ardhi Kenya.

Kibera ni mtaa ambao una mchanganyiko wa watu kutoka tabaka mbali mbali, huku takwimu za Umoja wa mataifa zikikadiria kwamba kuna takriban kati ya watu 400,000 na milioni 1.5 wanaoishi katika eneo hilo.