Joseph Mbilinyi: Sugu kuishtaki BASATA baada ya wimbo wake kufungiwa

Chanzo cha picha, JOSEPH MBILINYI
Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina Sugu ana mpango wa kulishtaki baraza la sanaa nchini Tanzania (BASATA) kutokana na kuufungia wimbo wake.
Sugu amesema atawaelekeza wanasheria wake sita kufungua kesi mahakamani kuishtaki BASATA.
BASATA , chombo cha serikali ambacho kinasimamia shughuli za wanamuziki, filamu na kazi nyingine za sanaa ilitangaza kufungiwa kwa wimbo mpya wa Sugu unaoitwa 219 kwa madai kuwa una ujumbe wenye uchochezi.
''Basata imefungia wimbo wa Joseph Mbilinyi namba 219 kwa sababu una ujumbe wa kichochezi. Taasisi pia inamfungia mwanamuziki huyo kutokutumbuiza, kutorekodi na kusambaza muziki wake," Basata ilieleza kwenye taarifa yake.
Ilisema wimbo huo si kuwa una ujumbe wenye kuchochea lakini pia haukufuata taratibu za kuutoa wimbo huo.

Wakati wa uchangiaji wa makadirio ya bajeti bungeni, Sugu alisema ni bahati mbaya BASATA imeamua kuufungia wimbo 'uliovuja'.
''Wimbo umevuja. Wanawezaje kutoa kauli hiyo kufungia wimbo uliovuja? Hawajawahi kwenda kwenye studio ya kurekodi. Je wanataka sisi sote tuimbe nyimbo za mapenzi''? alihoji Sugu, akisisitiza kuwa imefikia wakati kila taasisi nchini inafanya kazi kama Polisi.
Lakini naibu waziri wa habari,utamaduni, sanaa na michezi, Juliana Shonza alisimama na kutoa taarifa kwa bunge kuwa binafsi alisikiliza wimbo huo na kujiridhisha kuwa kweli ulikuwa wa kichochezi.
Lakini akijibu taarifa hiyo, Sugu alisema'' Mimi si Diamond wala Roma. (ambao nyimbo zao zilifungiwa awali). Nitawaelekeza mawakili wangu kuchukua hatua," lisema












