Ajali ya ndege Cuba: Boeing 737 yaanguka karibu na uwanja wa ndege wa Havana

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Ndege ya kubeba abiria aina ya Boeing 737 ya shirika la ndege la taifa Cuba, Cubana de Aviacion, imeanguka na kulipuka karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jose Marti, Havana, vyombo vya habari Cuba vinasema.
Shirika la habari la Prensa Latina limesema ndege hiyo imeanguka muda mfupi baada ya kupaa.
Taarifa zinasema ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 104. Kufikia sasa, hakujatolewa taarifa kuhusu hatima yao.
Radio Habana Cuba imeripoti kwamba ilikuwa ndege ya safari za ndani ya nchi na ilikuwa safarini kutoka Havana kwenda Holguin, mashariki mwa taifa hilo.
Watu walioshuhudia wameambia shirika la habari la AFP kwamba waliona moshi mwingi ukipaa angani kutoka eneo la ajali hiyo.
Wazima moto na watoaji huduma za dharura wakiwa na magari ya kuwabebea wagonjwa wamefika eneo hilo.
Rais wa taifa hilo Miguel Diaz-Canel ambaye aliapishwa mwezi jana, yumo njiani kuelekea eneo la mkasa, shifika la AFP linasema.
Radio Habana Cuba imesema kwenye Twitter kwamba ndege hiyo ilianguka kwenye "barabara kuu" kati ya Boyeros na Havana, karibu na uwanja huo wa ndege.













