Zanzibar yapambana kutokomeza ugonjwa wa Chikungunya

Chikungunya huenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chikungunya huenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae

Mamlaka visiwani Zanzibar zinapambana kuutokomeza ugonjwa wa ''Chikungunya'', ugonjwa unaoenezwa na mbu, virusi vinavyoelezwa kuenenzwa na mbu huyo vinaelezwa kuingia visiwani Zanzibar mwaka huu.

Waziri wa Afya visiwani humo, Hamad Rashid Mohammed amsesema maradhi hayo yalianza kuripotiwa eneo la Stone Town, Serikali ikachukua hatua ya kupulizia dawa katika eneo hilo ili kudhibiti virusi.

Kwa mujibu wa Waziri, ugonjwa huu husambazwa iwapo mbu mwenye virusi atamng'ata mtu.

Ingawa Chikungunya si ugonjwa unaoua mara zote, husabaisha maumivu ya viungo kwa muda wa miezi au miaka kadhaa.Wataalam wameeleza.

Chikungunya ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae.Dalili za ugonjwa huu ni kuumwa mafua makali, homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo, hasa mikono ,miguu, uchovu wa mwili, kichefuchefu.

Waziri Hamad ameeleza hali ilivyo hivi sasa akisema hali si ya kutisha

chandarua

'Hali ni nzuri ingawa kuna maeneo yameathirika, idadi si kubwa ya kutisha walioathirika ni wastani wa idadi ya watu kati ya sita mpaka saba na hakuna yeyote ambaye amepoteza maisha''.

Waziri Hamad amewataka watu kuchukua tahadhari kuepuka ugonjwa huu:

''Chikungunya ni ugonjwa ambao unatibika cha msingi ni kuzingatia usafi na ajitahidi kuvaa shati ya mikono mirefu kwa sababu mbu hushambulia mchana na si usiku na hupenda kushambulia maeneo yenye mikusanyiko tukifanya hayo tatizo tutalimaliza.''

Bwana Hamad amesema walioathiriwa na ugonjwa huo wako hospitali kwa ajili ya mapumziko na kuongezewa maji.

Neno CHIKUNGUNYA ni neno la kimakonde kabila linalopatikana kusini mwa Tanzania, likiwa na maana ya kitu kilichobadilika umbile lake(kujikunja) na kuwa tofauti na awali, wakichukulia dalili ya kuvimba kwa maungio kunakosababishwa na ugonjwa huu.

Kwa mara ya kwanza uligundulika mwaka 1952 ambapo mlipuko wa ugonjwa huu ulitokea maeneo ya kusini mwa Tanzania hasa Mkoa wa Mtwara Lakini kwa sasa ugonjwa huu umezikumba takribani nchi 60 duniani kwenye mabara ya Asia, Ulaya na bara la Amerika na hivi karibuni Ugonjwa huu uliripotiwa kutokea mjini Mombasa nchini Kenya.