Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afrika Kusini: Familia yenye utata ya Gupta yavamiwa na polisi
Watu watatu wamekamatwa baada ya nyumba ya familia ya Gupta yenye utata nchini Afrika Kusini kuvamiwa katika muendelezo wa uchunguzi dhidi ya familia hiyo inayodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa serikali.
Familia tajiri ya wazaliwa wa India ya Gupta imeshutumiwa kwa kutumia urafiki wao na Rais Zuma kwa manufaa binafsi na kibiashara.
Bwana Zuma na wakina Gupta wote wamekana shutuma hizo dhidi yao.
Kwa kiasi shinikizo kubwa la Zuma kujiuzulu linatokana na uhusiano wake na familia hiyo.
Anatarajiwa kuzungumza hivi karibuni kuhusu wito wa chama cha ANC wa kuondoka madarakani.
Cheo cha Zuma kama kiongozi wa chama kilichukuliwa na makamu wake, Cyril Ramaphosa, Disemba mwaka jana ,lakini hadi sasa amekataa wito wa chama kujiuzulu.
Afisa mmoja wa chama amesema alikuwa tayari kuachia ngazi ndani ya miezi mitatu hadi sita ijayo, lakini viongozi wa juu wanataka atoke mara moja.
Kiongozi huyo mwenye kashfa nyingi amekuwa madarakani tangu mwaka 2009.
Kikosi maalum cha 'The Hawks', kimethibitisha wamezingira eneo la Gupta mjini Johannesburg Jumatano asubuhi.
Familia ya Gupta inayomiliki baadhi ya biashara Afrika Kusini imeshutumiwa kutumia ushawishi wao na urafiki na Jacob Zuma vibaya kupata mikataba ya serikali inayogharimu mamilioni ya dola za kimarekani.