Rais Magufuli: Mshahara wangu ni shilingi milioni 9 za Tanzania

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Tanzania John Magufuli amefichua kuwa anapokea mshahara wa kila mwezi wa shilingi milioni 9 za Tanzania.
Hii ni robo ya mshahara ambao mtangulizi wake Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa akipokea iwapo takwimu zilizonakiliwa na Afrika Review miaka mitatu iliopita ni za kweli.
Rais Magufuli alifichua hayo katika taarifa ya moja kwa moja katika runinga mapema Jumanne katika hotuba kwa muungano wa serikali za mitaani wakati ambapo alikuwa akikisisitiza kuhusu umuhimu kwa kukabiliana na rushwa.
''Baadhi ya wanachama wa bodi za mashirika ya uma walikuwa wakisafiri hadi Dubai kufanya mikutano yao huko ili wajilipe marupuru mengi.Hivi sasa hawataki kile serikali yangu inachofanya''.
Kwa jina la utani 'Tinga', Magufuli ambaye alichukua mamlaka 2015, anajulikana kwa kufanya ziara za kushtukizia katika taasisi za serikali katika juhudi za kukabiliana na ufisadi pamoja na wale wasiofika kazini bila sababu.
Mwaka uliopita, mbunge mmoja wa upinzani alimtaka kutangaza mshahara anaopata na kuhoji kwamba anapaswa kulipa kodi.









