Wakazi 70,000 kuhamishwa Frankfurt kwa sababu ya bomu kubwa

Bomu hilo la Uingereza lilipatikana ardhini katika eneo la Wismarer Strasse, iliyoko karibu na katikati mwa mji

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Bomu hilo la Uingereza lilipatikana ardhini katika eneo la Wismarer Strasse, iliyoko karibu na katikati mwa mji

Polisi nchini Ujerumani, watawaondoa zaidi ya watu 70,000 kutoka maskani yao hapo siku ya Jumapili, baada ya kupatikana bomu kubwa ambalo halijalipuka katika mji wa Frankfurt.

Bomu hilo linaloaminika kuachwa na wanajeshi wa Uingereza wakati wa vita kuu vya pili vya dunia.

Hiyo ni mojawepo ya operesheni kubwa mno ya aina yake kuwahi kufanyika nchini Ujerumani tangu kumalizika kwa vita hivyo.

Bomu hilo la tani 1.4 lililoundiwa Uingereza na kupewa jina la utani "blockbuster' wakati wa vita hivyo kutokana na uwezo wake wa kuramba barabara nzima, lilipatikana karibu na Chuo Kikuu cha Goethe Frankfurt.

Watu katika Chuo hicho, Benki kuu na hospitali zilizoko karibu wataondolewa.

Polisi inasema kuwa bomu hilo lilikuwa chapa HC 4000, muundo unaotumika kwa mashambulizi ya angani na jeshi la Uingereza.

Lilipatikana katika eneo la Wismarer Strasse, lililoko karibu na kaikati mwa mji na kilomita 2.5(maili 1.5) kaskazii mwa soko kuu la eneo hilo mjini humo.

Je, Bomu ambalo halijalipuka lina hatari gani?

Maafisa wa polisi wanalinda eneo hilo "hakuna hatari yoyote kwa sasa".

Wataalamu wa kudungua bomu, wanachunguza bomu hilo na kusema kuwa shughuli za kuwahamisha watu, zinaweza kungojea hadi mwishoni mwa juma

"Tunajaribu kufanya kila tuwezalo na mbinu muafaka wa kuwahamisha watu," msemaji mmoja wa kike wa idara ya polisi mjini Frankfurt amesema.

Mabomu ambayo hayakulipuka mara kwa mara yamekuwa yakipatikana yamezikwa chini ya ardhi nchini Ujerumani.

Zaidi ya watu 20,000 wataondolewa magharibi mwa mji wa Koblenz siku ya Jumamosi, baada ya mabomu hilo kugunduliwa.

Mwezi Mei mwaka huu, zaidi ya watu 50,000 mjini Hannover, walilazimika kuondoka majumbani mwao, huku wataalamu wakitafuta mbinu ya kudungua mabomu matatu yaliyoachwa na wanajeshi wa Uingereza.