Mwanamume aponzwa na uvumi kuhusu harusi ya Dr Dre nchini Korea Kusini

Mwanamume wa miaka 73 nchini Korea Kusinia mepigwa faini kwa kueneza uvumi mtandaoni kwamba mjane wa rais wa zamani wa nchi hiyo anapanga kuolewa na nyota wa muziki wa rap Dr Dre.

Mwanamume huyo ambaye jina lake halijatajwa alikuwa amesema kwamba harusi hiyo iliyokusudiwa ilikuwa na lengo la kufuja fedha zilizoachwa na ikiongozi wa zamani Kim Dae-jung.

Mjane wa Kim, Lee Hee-ho, ana miaka 95 lakini bado huwa na ushawishi sana Korea Kusini.

Mahakama moja mjini Seoul iliamua Ijumaa kwamba Lee "alivunjia heshima marehemu na jamaa za marehemu".

"Uvumi huo kuhusu fedha hizo na ndoa kati ya Lee na Dr Dre ni mambo mabayo hayana msingi," alisema Jaji Lee Eun-hee, na akamtoza Lee faini ya won 5m za Korea ($4,400; £3,410).

Haijabainika, hata hivyo, iwapo kuna yeyote ambaye alishawishika na taarifa hizo kuhusu urafiki huo usio wa kawaida.

Dr Dre - ambaye jina lake halisi ni Andre Romelle Young - ni maarufu sana katika tasnia ya muziki wa rap.

Yeye ni mwanzilishi wa kundi la muziki wa 'gangsta rap' kwa jina NWA na pia ndiye mwanzilishi wa kampuni ya kurekodi na kuuza muziki ya Death Row Records, ambayo imefanya kazi na wanamuziki kama vile Snoop Dog, Tupac Shakur na Young Soldierz.

Kwa sasa ni miongoni mwa wanamuziki tajiri zaidi duniani.

Bi Lee, alikuwa mke wa rais aliyeongoza Korea Kusini kuanzia 1998 hadi 2003.

Mumewe alipigania sana mashauriano na Korea Kaskazini na alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2000 kwa juhudi hizo.

Bi Lee amebaki kuwa na ushawishi sana na amezuru Korea Kaskazini mara mbili tangu kifo cha mumewe mwaka 2009.

Haijabainika iwapo anazipenda nyimbo za Dr Dre.