Kipande kikubwa cha barafu chameguka Antarctica

Larsen C crack

Chanzo cha picha, NASA / SUOMI NPP / SIMON PROUD

Maelezo ya picha, Picha za barafu hiyo iliyopigwa na satelaiti ya Suomi NPP inayomilikiwa na NASA

Kipande kikubwa zaidi cha barafu kuwahi kuonekana duniani kimemefuka kutoka kwenye eneo la Antarctica.

Jiwe hilo kubwa la barafu linakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilomita mraba 6,000, ukubwa sawa na wa eneo la Wales nchini Uingereza.

Kipande hicho cha barafu kina ukubwa mara 50 kushinda kisiwa cha Manhattan, Marekani

Satelaiti ya Marekani ilionesha jiwe hilo kubwa likiwa limemeguka ilipokuwa inapitia eneo la barafu lifahamikalo kama Larsen C Jumatano.

Wanasayansi walikuwa wanatarajia hilo. Wamekuwa wakifuatilia ufa mkubwa katika barafu ya Larsen kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Larsen C ndiyo sehemu kubwa ya barafu iliyo kaskazini zaidi mwa dunia eneo la Antarctica.

Watafiti walikuwa awali wamesema iwapo eneo hilo lingepoteza kipande hicho cha barafu basi sehemu yote yenyewe itakuwa hatarini ya kupasuka tena siku za usoni.

Eneo la barafu la Larsen C lina kina cha mita 350.

Barafu hiyo huelea maeneo ya pembeni Antarctica Magharibi na kuzuia mito ya barafu ambayo huisaidia kukaa imara.

Watafiti wamekuwa wakifuatilia Larsen C baada ya kumeguka kwa sehemu ya barafu ya Larsen A mwaka 1995 na kisha kupasuka ghafla kwa sehemu ya barafu ya Larsen B mwaka 2002.

Wataalamu wanakadiria kwamba iwapo barafu yote kwenye sehemu hiyo ya bahari ya Larsen C itayeyuka na kuwa maji na kuingia baharini, viwango vya maji baharini vitapanda kwa sentimeta 10.

Graphic showing how the iceberg compares to London, Hawaii and Cyprus
Barafu

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Ufa uliokuwa kwenye eneo hilo la barafu kabla ya kipande hicho kumeguka
Barafu

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Picha zilizopigwa Novemba mwaka jana zikionyesha ufa uliotokea
Larsen C

Chanzo cha picha, BAS

Maelezo ya picha, Kwa sasa ni katikati mwa majira ya baridi Antarctic. Ufa kwenye barafu hiyo ulipigwa picha majira ya joto yaliyopita.
Map