Milipuko yawaua watu 36 kanisani nchini Misri

Chanzo cha picha, EPA
Takriban watu 36 wameuawa nchini Misri kufuatia milipuko iliyolenga waumini wa kanisa la Coptic leo Jumapili.
Watu 11 waliuawa wakati mlipuko ulitoke katika kanisa la St Mark's Coptic mjini Alexandria.
Pope Tawadros II, ambaye ni mkuu wa kanisa la Coptic alikuwa amehudhuria misa katika kanisa hilo.

Watu wengine 25 walikuwa wameuawa mapema katika kanisa la St George's Coptic, mji wa Tanta umbali wa takriban kilomita 130 kusini mashariki.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari ,Pope Tawadros hakuhumia. Msaidizi wake alisema kuwa shambulizi la Alexandria liliendeshwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga nje ya kanisa.
Kundi la Islamic State linasema kuwa ndilo liliendesha mashambulizi hayo.
Mwezi Disemba mwaka uliopita, watu 25 waliuawa wakati bomu lilipolipuka katika kanisa la Coptic cathedral mjini Cairo wakati wa sala.

Chanzo cha picha, Reuters
Ghasia dhidi ya wakiristo wa Coptic, zimekuwa nyingi miaka ya hivi karibuni, hasa tangu mwaka 2013 wakati jeshi lilipompindua rais aliyekuwa amechaguliwa.
Baadhi ya wafuasi wa rais aliyetimuliwa Mohammed Morsi, ambaye alitoka kundi la Muslim Brotherhood, waliwalaumu wakiristo kwa kuunga mkono kupinduliwa kwake.












