Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watangazaji wauawa wakiwa hewani
Wanaume watatu wamekamatwa kufuatia mauaji ya watangazaji wawili wa kituo cha Radio waliokuwa hewani katika Jamuhuri ya Dominika.
Mmoja wa waandishi alikuwa akipeperusha matangazo kwenye ukurasa wa Facebook wakati alipopigwa risasi na kuuawa.
Kanda ya video imeonyesha matangazo hayo yakikatizwa ghafla na kisha mwanamke mmoja anasikika akilia "Risasi! Risasi! Risasi!".
Polisi wamethibitisha shambulio hilo lilifanyika hapo Jumanne katika eneo la San Pedro de Macoris, mashariki mwa mji mkuu wa Santo Domingo.
Waliouawa ni pamoja na mtangazaji Luis Manuel Medina na msimamizi wa matangazo Leo Martinez.
Mwanamke mmoja alijeruhiwa na anaendelea kupokea matibabu.
Wanaume waliokamatwa hawajafunguliwa mashtaka na polisi wanasema hawajui kilichosababisha mauaji hayo na kuongeza uchunguzi unaendelea.
Hapo mwezi Agosti mwaka 2015, waandishi habari wawili wa Marekani walipigwa risasi na kuuawa wakati wakitangaza kwenye runinga katika jimbo la Virginia.