Trump ashutumiwa kwa sababu ya Ivanka

Chanzo cha picha, AP
Viongozi wa chama cha Democratic nchini Marekani wamemshutumu Rais wa Marekani Donald Trump kuandika kwenye Twitter akishutumu maduka ya jumla ya Nordstrom kwa kuacha kuuza nguo za kampuni inayomilikiwa na bintiye.
Bw Trump aliandika kwenye Twitter kwamba "Ivanka ameonewa sana" na maduka hayo.
Seneta mmoja wa chama cha Democratic amesema hatua hiyo "haifai" naye afisa mmoja wa zamani wa maadili katika ikulu ya White House alisema "ni ya kushangaza".
Mapema mwezi huu, maduka ya Nordstrom yalikuwa ya tano kuacha kuuza mavazi ya kampuni ya Ivanka Trump, kwa walichosema kuwa ni kushuka kwa mauzo.
Hatua hiyo imechukuliwa huku baadhi ya watu wakiwasihi wateja kususia bidhaa za Trump.
Wanahakati wamepatia kampeni yao jina #GrabYourWallet (Twaa pochi lako), wakirejelea matamshi ya Bw Trump mwaka 2005 kuhusu wanawake.
Msemaji wa seneta wa Pennsylvania Bob Casey alisema seneta huyo "anahisi ni ukiukaji wa maadili na hatua isiyofaa kwa rais kushambulia kampuni ya kibinafsi kwa kukataa kutajirisha familia yake".
Norm Eisen, ambaye alihudumu kama afisa wa maadili katika ikulu ya White House chini ya Rais Barack Obama, alisema hatua hiyo ni "ya kushangaza" na akawashauri Nordstrom kumfungulia kesi Bw Trump chini ya sheria za California kuhusu ushindani kibiashara.


Chanzo cha picha, AP
Ikulu ya White House imedunisha mzozo huo.
Msemaji wa ikulu Sean Spicer alisema hatua ya Nordstrom iliongozwa na siasa, na kwamba rais alikuwa tu anajibu "shambulio" dhidi ya binti yake.

Chanzo cha picha, Twitter
Ujumbe wa Bw Trump kwenye Twitter ulichapishwa kwenye akaunti yake ya kibinafsi ya @realDonaldTrump, kisha ukasambazwa na akaunti rasmi ya rais ya @POTUS.
Bei ya hisa za maduka hayo ya jumla ilishuka 0.7%, kabla ya kuanza kupanda tena.















