Waigizaji wataandamana Washington Trump atakapoapishwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Waigizaji maarufu wa kike wa Hollywood watashiriki maandamano mjini Washington siku moja baada ya Donald Trump kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Marekani.
Mwigizaji America Ferrera wa kipindi cha Ugly Betty, aliyemuunga mkono Hilary Clinton wa chama cha Democratic, anasaidia katika shughuli za kupanga maandamano hayo.
Waigizaji wengine wa kike watakaoshiriki ni pamoja na Amy Schumer, Scarlett Johansson, Frances McDormand na Zendaya.
Katika hotuba yake alisema: "Tangu uchaguzi ukamilike, watu wengi wanahofia sauti yao haitasikika,''amesema America Ferrera.
''Kama wasanii, wanawake na zaidi ya yote Wamarekani waliojitolea ni muhimu tushirikiane kulinda hadhi na hadhi ya jamii yetu.''
Scarlett Johansson, ameshutumu utawala mpya wa Marekani kwa kuingilia uhuru wa wanawake kufanya maamuzi kuhusu uzazi na utoaji mimba.
Amesema anashiriki maandamano hayo kuhakikisha sauti yake inasikika na "kusimamia kile anachokiamini".

Chanzo cha picha, Getty Images
Waandamanaji wanasema wanatarajia zaidi ya watu laki moja kushiriki maandamano ya Januari 21, siku itakayofuata baada ya kuapishwa kwa Donald Trump.
Chelsea Handler, ataongoza maandamano ya kinadada katika eneo la Park City jimbo la Utah, katika mojawapo wa zaidi ya maandamano 150 iliyopangwa kote Amerika na katika maeneo mengine ulimwenguni Jumamosi ijayo.
Waigizaji wengine maarufu ambao wamethibitisha kushiriki maandamano ya Washington ni pamoja na Uzo Aduba wa The New Black, Lea DeLaria na Diane Guerrero. Wengine watakaoshiriki kupitia njia zingine kuunga mkono mpango huo ni Katy Perry, Julianne Moore, Cher na Debra Messing.












