Mateka wasema walikula panya Somalia

Mateka walioachiliwa huru baada ya kuwasili Kenya, 23 Oktoba 2016.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mateka hao waliachiliwa huru wikendi na wakafika Kenya Jumapili

Kundi la mabaharia ambao waliachiliwa huru Jumamosi baada ya kuzuiliwa na maharamia kwa miaka mitano nchini Somalia walikula hata panya ili waishi, mmoja wao ameambia BBC.

Arnel Balbero, kutoka Ufilipino amesema walikuwa wanapewa maji kidogo sana na walijihisi kama "wafu waliokuwa wakitembea" kufikia wakati wa kuachiliwa huru kwao.

Mabaharia hao walitekwa wakiwa kwenye meli mwaka 2012 kwenye pwani ya Ushelisheli na wakapelekwa Somalia bara na kuzuiliwa mateka.

Waliachiliwa huru Jumamosi. Taarifa zinasema waliokuwa wanawazuilia mateka walilipwa kikombozi.

Mabaharia hao walitoka Uchina, Ufilipino, Cambodia, Indonesia, Vietnam na Taiwan.

Bw Balbero alikuwa mmoja wa mabaharia waliokuwa kwenye meli ya FV Naham 3 ilipotekwa.

Meli hiyo ilizama mwaka mmoja baadaye na wakapelekwa Somalia bara kuzuiliwa.

Bw Balbero aliambia BBC kwamba kwa miaka minne unusu ambayo walikuwa mateka, yeye na wenzake walikuwa kama "wafu waliokuwa wanatembea."

Alipoulizwa maharamia waliwashughulikia vipi, alisema: "Walitupa maji kidogo tu. Tulikuwa panya. Ndio, tulipika panya na kuwala huko msituni."

"Tulikuwa tunakula kila kitu, kila kitu. Ukihisi njaa, unakula."

Mateka wakijiandaa kuabiri ndege baada ya kuachiliwa huru Galkayo, Somalia Jumapili 23 Oktoba 2016.

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Walikuwa 29 walipotekwa lakini mmoja alifariki wakati wa kutekwa nyara. Wengine wawili walifariki baada ya kuugua wakishikiliwa mateka

'Bila maji, bila chakula, bila maji'

Amesema pia kwamba anatarajia watatizika sana kuzoea maisha baada ya waliyopitia huko.

"Sijui mambo yakoje ... huko nje, duniani haya yote yakimalizika, itakuwa vigumu sana kuanza tena maisha."

Shen Jui-chang

Chanzo cha picha, Cheng-yuan Tsai

Maelezo ya picha, Shen Jui-chang, Mhandisi kutoka Taiwan, alikuwa kwenye kanda ya mateka iliyotolewa majuzi. Video hiyo ilipigwa 2014

Kwenye ukanda wa video unaoonyesha mateka hao, ambao ulipigwa mwaka 2014, mwanamume aliyetambuliwa kama Shen Jui-chang, mhandisi kuoka Taiwan anasikika akisema walipewa lita moja ya maji pekee licha ya joto kali.

"Hakuna maji, hakuna chakula," anasema na kuongeza kwamba "kila mmoja wetu anaugua ugonjwa fulani."

"Maharamia hawatupatii dawa, wanasema hawana pesa za kununua dawa. Hivi ndivyo vijana wawili walifariki," anasema kwenye video hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Taiwan imesema wanaume hao waliachiliwa huru baada ya kulipwa kwa kikombozi na mmiliki wa meli hiyo pamoja na makundi yaliyopewa kazi ya kuendesha mazungumzo na watekaji nyara, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Taiwan.

Meli hiyo ilipeperusha bendera ya Oman lakini ilimilikiwa na kampuni ya Taiwan.