Marekani yataka Urusi kuchunguzwa kwa uhalifu wa kivita

Chanzo cha picha, Reuters
Serikali ya Urusi na ile ya Syria zinafaa kuchunguzwa kwa uhalifu wa kivita ,waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani amesema.
''Urusi na utawala wa Syria zinafaa kuelezea kwa nini wanaendelea kushambulia hospitali na vifaa vyangine vya matibabu na watoto'',alisema.''Hivi ni vitendo ambavyo vinahitaji uchunguzi wa uhalifu wa kivita''.
Moscow kwa mara nyengine imekana kushambulia raia na kusema kuwa ilikuwa ikilenga makundi ya kigaidi nchini Syria.
Bwana Kerry hatahivyo amesema kuwa mashambulio ya Urusi na Syria katika hospitali yalikuwa sio ya bahati mbaya na kwamba ni mpango wa vita vyake nchini humo.

''Ni mpango wa kuwatishia wananchi na kumuua mtu yeyote ama watu wowote wanaopinga mipango yao ya kijeshi'',alisema.
Bwana Kerry alikuwa akizungumza mjini Washington katika mkutano na wanahabari pamoja na waziri wa maswala ya kigeni nchini Ufaransa Jean-Marc Ayrault.








