Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Katumbi asema atarejea DR Congo kuwania urais
Mwanasiasa aliyetangaza nia ya kuwania urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi, ambaye amekuwa akiishi uhamishoni, amesema atarejea nyumbani.
Bw Katumbi, rafiki wa karibu wa zamani wa Rais Joseph Kabila amekuwa akiishi Ubelgiji.
Aliondoka nchini DR Congo mapema mwaka huu baada ya kutuhumiwa kuajiri mamluki kwa lengo la kupindua serikali ya Rais Kabila.
Na baadaye mwezi Juni, alipatikana na hatia ya kuuza nyumba kinyume cha sheria na akahukumiwa kifungo cha miezi 36 jela.
Akiongea na BBC akiwa ziarani London, Bw Katumbi amesema:
"Mimi ni raia wa Congo, nitarejea nyumbani na bado nawania urais. Tuhuma kwamba nilipanga kupindua serikali zinakusudiwa kunizuia."