Njia 4 za ‘kusuka ama kunyoa’ kuhusu mjadala wa bandari Tanzania

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Mjadala umeendelea kuwa mkubwa nchini Tanzania kuhusu suala la bandari. Umedumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na unaweza kuwa kuwa moja ya mijadala mirefu na iliyodumu kwa muda mrefu zaidi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Na hauonekani kumalizika katika majuma ya karibuni. Inaonekana dhahiri utaendelea kwa muda na kila litakapotajwa ama kutokea jambo lolote linalohusu bandari mjadala utaibuka na kushika kasi tena.

Mjadala huu unatokana na uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuingia mkataba na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari za bahari na maziwa Tanzania.

Mkataba huu unaofahamika kwa lugha ya Kiingereza kama Inter-Governmental Agreement-IGA na wenye ibara 31, uliingiwa mnamo Oktoba 25, 2022, kabla ya kuridhiwa na Bunge la nchi hiyo Juni 10, 2023 kupitia Azamio la Bunge.

Awali, kwa mujibu wa Azimio la Bunge kuhusu mkataba huo, Serikali, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding - MOU) na Kampuni ya DP World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai mnamo Februari 28, 2022.

Kwa mujibu wa Azimio hilo, makubaliano yanalenga kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa, maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors).

Sasa mchakato huu na makubaliano yaliyoingiwa hasa ya IGA, yameibua mjadala na mzozo mkubwa baina ya wanaounga mkono hatua na yaliyomo katika mkataba au makubaliano na wale wasiounga mkono ama hatua au baadhi ya yaliyopo kwenye mkataba au makubaliano hayo.

Yapi yanayoleta Mjadala?

Ukisikiliza maelezo ya upande wa wasemaji wa serikali wanapowasilisha hoja kuhusu mchakato huu hata Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipozunguma bungeni, wanatumia neno ‘Mkataba’. Aliwasilisha maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Dubai

Kwa muktadha huo aliwasilisha Mkataba, lakini mjadala uliibuka zaidi aliponukuliwa Spika wa Bunge, Tulia Ackson akieleza ‘Kilichopitishwa na Bunge [kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Dubai] sio mkataba ni makubaliano, na makubaliano ni hatua ya kwenda kwenye mkataba.’ Je ni Mkataba au Makuabliano? Huo ni mjadala.

Ukomo wa mkataba au makubaliano hayo pia ni mjadala. Wanaokosoa wanataka uwepo ukomo rasmi wa mkataba huo wakirejea mikataba ya aina hiyo kwa mataifa mengine kama Uingereza, inayoonyesha ukomo. Lakini Waziri Mbarawa alilieleza Bunge kuwa mkataba huu utakuwa hai mpaka pale ambapo shughuli za miradi zitasitishwa au kuisha kwa muda wa mikataba ya nchi mwenyeji na mikataba ya miradi.

Na akaeleza ‘Msingi wa Mkataba huu kuendana na mikataba ya miradi ni kutokana na kwamba unaweka msingi unaowezesha kuingia na kutekelezwa kwa mikataba 10 nchini. Iwapo mkataba huu utakuwa na ukomo kabla ya kuisha mikataba ya miradi iliyo chini ya mkataba huu, utekelezaji wa mikataba ya miradi baada ya kuisha kwa mkataba huu itakuwa batili”.

Sasa kutokuwepo kwa ukomo wa mkataba unaibua mjadala mwingine, kwanini? Je hatua hii ni kuiuza bandari mwekezaji, kuikodisha au kuibinafsisha? Wanaounga mkono au wanatetea wanasema ni uwekezaji wa kawaida kama ilivyokuwa kwa miaka 22 chini ya TICTS (Tanzania International Container Terminal Services).

Yapo mengi yanayoibua mjadala ukiacha suala la ukomo na je kilichoingiwa ni Mkataba au Makubaliano? Lipo suala la Mkataba au Makubaliano haya hayavunjiki, Mkataba au Makubaliano hayo ni ya upande mmoja, Je mkataba ni wa bandari ya Dar es Salaam pekee ama na bandari zingine? na lingine ni sheria za Uingereza kutumika kusimamia na kuongoza makubaliano ama mkataba huo baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA).

Kwa ufuatiliaji nilioufanya, masuala haya manne, ama moja kati ya haya ama yote ama baadhi yakifanyika huenda yakasaidia kuuzima moto wa mjadala huu unaotishia kuleta mpasuko nchini humo...

1. Kurejesha mkataba wa IGA bungeni na kubatilisha azimio la bunge

Bunge kupitisha Azimio la kuunga mkono Mkataba huu wa IGA baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai maana yake wananchi wa Tanzania wameridhia kupitia kwa wawakilishi wao, wabunge. Hatua ya sasa ina baraka za wananchi kwa mifumo iliyopo, kwa sababu ya sharti la makubaliano lililotaka bunge kuridhia.

Ili kupata fursa ya kurejea na kufanya marekebisho mengine, Serikali haiwezi kufanya kiholela, lazima Bunge liwe na mkono wake tena kwa Azimio lake ililolopitisha kuhusu bandari, ili kuuisukuma serikali kufanya marekebisho kwenye vipengele vinavyoonekana vina ukakasi kwa wengine.

Hili halionekani kama jambo rahisi sana kwa sasa kutokana na mchakato ulipofika. Mkataba ulishasainiwa na shughuli za awali zimeanza. Lakini kwa kauli za wabunge mbalimbali na Spika Tulia, hilo si jambo linalowezekana kutokea kwa haraka.

2. Kuunda timu ya pamoja

Kama njia ya kwanza haiwezekani kwa sasa, inaweza kuundwa timu ya pamoja itakayojumuisha wanaopinga ama kukosoa mchakato ama vipengele vya mkataba, na wale wanaounga mkono pamoja na wadau wengine muhimu kama chama cha wanasheria Tanganyika (TLS). Hao wote wakakaa pamoja na kuainisha vipengele vya mzozo na kuangalia kisheria vinawezaje kushughulikiwa, nchi inapokwenda kuingia mikataba ya utekelezaji (HGA).

Aina hii ya njia hata Rais Samia Suluhu Hassan aliitaja juma hivi karibuni wakati akiwaapisha viongozi Ikulu, baaada ya kufanya marekebisho ya wizara na kuteua viongozi kadhaa.

‘Ukisoma kwenye mitandoa huko, tunakosolewa huku kushoto, kulia, kusini, kaskazini, mpaka nje mpaka wapi, sasa wale mnaohisi wana mchango mzuri mnaweza mkawajumuisha, wakawa sehemu ya tume ya mipango, wakafikiri pamoja na sisi, ili tukaondosha lile vuguvugu kwamba wamefikiri nini, wamepanga nini, tutakuwatumepanga wote’ alisema Rais Samia.

Lakini akaongeza ‘ Tanzania ni yetu wote, wote tufikri, wote tukawaze kwa ajili ya nchi yetu’.

Kwa sababu fursa ya pili iliyopo ni mikataba ya utekelezaji (HGA) kuhusu bandari ambayo itaingia baada na ambayo inaweza kufikia 10, basi timu hii mahususi pamoja na mipango mingine muhimu ya nchi inayogusa rasilimali na umma wa watanzania inaweza kuwa muhimu kwa hili la bandari.

3. Kuundwa kwa Kampuni ya DP World Tanzania Limited

Hii njia ambayo mara kadhaa imetumika kwa nchi nyingi zinapoleta wawekezaji wanaogusa rasilimali muhimu za nchi. Na pia si njia ngeni Tanzania. Mzozo wa kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick ulisababisha kuundwa kwa kampuni ya pamoja na serikali inayoitwa Twiga Minerals Corporation Limited ambayo Serikali ya Tanzania ina umiliki wa hisa asilimia 16. Maana yake ni kwamba shughuli za migidi iliyo chini ya Barrick zinasimamiwa kwa uwazi zaidi chini ya kampuni hiyo ya pamoja.

Kampuni ya LZ Nickel Limited ya Uingereza ikafuata nyayo za Barrick ikaingia ubia na Serikali ya Tanzania na kuanzisha kampuni ya pamoja ya uchimbaji madini ya Tembo Nickel.

Kwa upande wa bandari inaweza kufuata njia hii. Ikaundwa kampuni itakayoitwa DP World Tanzania Limited ama jina lolote tu.

Zitto Kabwe, mchumi kitaaluma na kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo aliwahi kugusia hili la kuundwa kwa kampuni ya pamoja. Zitto alienda mbali zaidi akipendekeza kampuni hiyo ya pamoja iitwe Tanzania-Dubai Ports Limited (TDPL) akipendekeza umiliki wa kampuni hiyo uwe wa asilimia 50 kwa 50.

Inawezekana na mantiki ya aina hii ya uwekezaji ni kuhakikisha watanzania wanaendelea kumiliki rasilimali zao na kuzisimamia. Pia ikiundwa na kusajiliwa kwa sheria za Tanzania, maana yake italazimika kufuata sheria za nchi kwenye masuala yote ya utekelezaji wa shughuli za bandari.

4. Kutambua na kuheshimu maoni kinzani

Mambo yote matatu ya juu yakishindikana angalau njia hii ya nne inaweza kutumika. Pengine ni njia rahisi kabisa kuliko zote kwa kuwa iko kwenye uwezo wa kila upande, wale wanaounga mkono na wale wanaopinga ama kukosoa mchakato ama IGA. Kuwe na kutambua na kuheshimu maoni kinzani.

Hapa linaonekana lipo tatizo. Wale wanaounga mkono baadhi hawataki kukubali kirahisi kwamba kuna mawazo tofauti na wale wanaopinga hawataki kukubali kirahisi kwamba wanaounga mkono nao wanahaki ya mawazo kwa kile walichokileta.

Wanaounga mkono wasiwaone wasiounga mkono kama maadui kwa sababu wanayo haki kikatiba kushiriki mjadala huo kama walivyo wao, ni nchi yao na bandari ni yao pia.

Wanaounga mkono wasijione ni bora kwa maoni yako kuliko wengine, wakajiona wana haki ya kulisemea suala la bandari kuliko wengine ama wakawaona wanaokosoa ni maadui.... ni watanzania wenzao, ni ndugu zao na zaidi ni jamii moja yenye nia njema kwa maoni yao tofauti

Kadhalika wasiounga mkono au wakososaji pia wanawajibu wa kuheshimu maoni ya walioona mkataba/makubaliano yako sawa. Wasijione wana haki ya kusema kuliko wengine, wana haki ya kushutumu kuliko wengine....wasione walioleta jambo hili wana nia ovu, pengine iko nia njema na waliona lilivyo jambo hili linafaa kwa maslahi ya nchi.

‘Muhimu sasa kuvumiliana na kujenga hoja bila kukwaza wengine kiutu na kisheria, anasema Raphael Kugesha, mtaalam wa maendeleo ya uchumi wa jamii, Tanzana.

‘Kukiwa na kukubaliana kwa uvumilivu wa hoja, kueleweshana na uwazi, pengine tusingekuwa na mijadlaa mikubwa hivi, tusingekuwa na kesi za kupinga ama kuitana Polisi’, na hata wanaopinga wasingetumia maneno makali mengine mpaka yanayogusa utu’, anasema Kugesha.

Uzuri hoja kubwa inayobishaniwaniwa....si faida za uwekezaji huo katika bandari....wengi wanaounga mkono na wanaopinga wanakubaliana uwekezaji wowote mkubwa zaidi ya ule wa sasa na hata uwepo wa TICTS utakuwa na faida zaidi kwa Tanzania

Kuanzia ufanisi wake kwa kupunguza muda wa meli kukaa gatini kutoka siku 5 kwa sasa mpaka saa 24, kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4 na nusu mpaka siku 2, Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 hadi saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA na kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33.

Faida zingine tarajiwa ni kupunguza gharama za utumiaji wa bandari, kuongeza ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, kusimika mifumo ya TEHAMA, kuboresha magati na kubwa zaidi kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka shilingi trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi shilingi trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.

Haya yanaelezwa na Serikali na ukisikiliza mjadala, wengi wanakubaliana kuhusu faida za uwekezaji na namna utakavyochagiza na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuchagiza shughuli za viwanda na biashara.

Nachokiona, mzozo mkubwa wa mjadala ni kuhusu yaliyomo kwenye Mkataba wa IGA. Kwa msingi huu suala hili ni jepesi kwa kuwa wote wanaopinga na wanaounga mkono wanataka kitu kizuri kwa bandari yao... ni kuamua tu kusuka ama kunyoa.