Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bilkis Bano:Kwanini watuhumiwa hawa wa ubakaji wamepokelewa kama mashujaa?
Bilkis Bano ambaye alibakwa na genge la watu na kushuhudia watu 14 wa familia yake wakiuawa na kundi la Wahindu wakati wa ghasia za 2002 dhidi ya Uislamu katika jimbo la magharibi la India la Gujarat, amerudi tena kwenye vichwa vya habari.
Siku ya Jumatatu, wafungwa 11 waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela kwa ubakaji na mauaji katika kesi hiyo, walitoka gerezani na kukaribishwa kama mashujaa. Video iliyosambaa ilionyesha wanaume hao wakiwa wamejipanga nje ya gereza la Godhra huku ndugu zao wakiwapa peremende na kugusa miguu yao kuonyesha heshima.
Uamuzi wa kuwaachilia wafungwa hao ulitangazwa na serikali ya Gujarat siku ya Jumatatu, wakati India ikiadhimisha miaka 75 ya uhuru.
Hatua ya serikali ya jimbo hilo, chama cha Hindu Bharatiya Janata Party (BJP) ambacho ndio kipo madarakani huko Gujarat na kitaifa imekosolewa na vyama vya upinzani, wanaharakati na waandishi wa habari kadhaa, ambao wanasema kwamba inakwenda kinyume na haki za Waislamu walio wachache.
Mashambulizi dhidi ya jamii yameongezeka sana tangu BJP kuunda serikali ya shirikisho mnamo 2014.
Afisa mmoja mkuu alisema jopo la serikali limeidhinisha ombi la wafungwa hao la kusamehewa kwa vile walikuwa wamekaa gerezani kwa miaka 14, pamoja na mambo mengine ikiwa ni pamoja na umri na tabia zao gerezani.
Wanaume hao, ambao kwa mara ya kwanza walihukumiwa na mahakama mwaka 2008, wamekaa gerezani kwa miaka 15. Lakini wengi wameeleza kuwa kuachiliwa huko kulikiuka miongozo iliyotolewa na serikali ya shirikisho na serikali ya jimbo la Gujarat, wote wanasema kuwa wafungwa wa ubakaji na mauaji hawawezi kusamehewa.
Masharti ya kifungo cha maisha katika uhalifu huu kawaida hutumikiwa hadi kifo nchini India. Kikwazo kikubwa zaidi, kinachotabiriwa, kimekuwa kwa Bilkis Bano na familia yake. "Kwa dakika kadhaa jioni ya Jumatatu, Bilkis Bano hakuamini kwamba wafungwa walikuwa wameachiwa huru, kwanza aliangua kilio na kisha akanyamaza," mume wake Yakub Rasool aliambia The Indian Express. “Tumeachwa tumekufa ganzi, tumeshtuka na kutingishwa,” aliongeza.
Gazeti hilo lilisema walipowasiliana na Bilkis Bano siku ya Jumanne, alisema: "Tafadhali niache... Nimefanya dua [maombi] kwa ajili ya roho ya binti yangu Saleha [mtoto wa miaka mitatu alikuwa miongoni mwa waliouawa]".
Hasira na kukata tamaa kwa familia ni rahisi kuelewa kwa kuzingatia ukubwa wa uhalifu na vita vya muda mrefu vya kupigania haki.
Shambulio dhidi ya Bilkis Bano na familia yake lilikuwa moja ya uhalifu wa kutisha wakati wa ghasia hizo, ambazo zilianza baada ya mahujaji 60 wa Kihindu kufariki katika ajali ya moto kwenye treni ya abiria katika mji wa Godhra.
Wakiwalaumu Waislamu kwa kuanzisha moto huo, makundi ya Wahindu yalifanya fujo na kushambulia vitongoji vya Waislamu. Zaidi ya siku tatu, zaidi ya watu 1,000 walifariki, wengi wao wakiwa Waislamu.
Narendra Modi, ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu wa Gujarat, alikosolewa kwa kutofanya vya kutosha kuzuia mauaji hayo. Siku zote amekuwa akikana makosa na hajaomba radhi kwa ghasia hizo. Mwaka 2013, jopo la Mahakama ya Juu pia lilisema kwamba hakuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki. Lakini wakosoaji wameendelea kumlaumu kwa ghasia zilizotokea mbele yake.
Kwa miaka mingi, mahakama zimewahukumu makumi ya watu kwa kuhusika na ghasia hizo, lakini baadhi ya washtakiwa wa ngazi za juu walipata dhamana au kuachiliwa huru na mahakama za juu.
Hii ni pamoja na Maya Kodnani, waziri wa zamani na msaada wa Bw Modi, ambaye kesi mahakamani ilimwita "kiini cha ghasia".
Na sasa wanaume waliomkosea Bilkis Bano pia wameachiliwa.
Mei 2017 kwenye nyumba moja mjini Delhi, siku chache tu baada ya Mahakama Kuu ya Bombay kuthibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa watu 11 waliopatikana na hatia katika kesi yake, Bilkis Bano alijaribu kuzuia machozi, alisimulia mambo ya kutisha ya shambulio hilo.
Asubuhi baada ya treni kuwaka moto, Bilkis Bano, wakati huo akiwa na umri wa miaka 19 na mjamzito wa mtoto wake wa pili alienda kuwatembelea wazazi wake katika kijiji kiitwacho Randhikpur karibu na Godhra pamoja na binti yake wa miaka mitatu.
"Nilikuwa jikoni nikitengeneza chakula cha mchana, kisha shangazi yangu na watoto wake walikuja mbio. Walisema nyumba zao zinachomwa moto na tulilazimika kuondoka mara moja," aliniambia. "Tuliondoka na nguo tulizokuwa tumevaa tu, hatukuwa na hata muda wa kuvaa malapa yetu."
Bilkis Bano alikuwa katika kundi la Waislamu 17 lililojumuisha binti yake, mama yake, binamu yake mjamzito, wadogo zake, wapwa na wapwa, na wanaume wawili wazima.
Katika siku chache zilizofuata, walisafiri kutoka kijiji hadi kijiji, wakitafuta makao katika misikiti au kujikimu kwa wema wa majirani wa Kihindu.
Asubuhi ya tarehe 3 Machi, walipokuwa wakitoka kwenda katika kijiji cha jirani ambako waliamini wangekuwa salama zaidi, kundi la wanaume liliwazuia.
"Walitushambulia kwa mapanga na fimbo. Mmoja wao alinipokonya binti yangu kutoka mapajani mwangu na kumtupa chini na kukiweka kichwa chake kwenye mwamba."
Washambuliaji wake walikuwa majirani zake kijijini, wanaume ambao alikuwa akiwaona karibu kila siku alipokuwa akikua. Walimvua nguo na kadhaa kati yao walimbaka, wakipuuza maombi yake ya kuhurumiwa.
Binamu yake, ambaye alikuwa amejifungua mtoto siku mbili zilizopita walipokuwa wakitoroka, alibakwa na kuuawa na mtoto wake mchanga aliuawa.
Bilkis Bano alinusurika kwa sababu alipoteza fahamu na washambuliaji wake wakaondoka, wakiamini amekufa. Wavulana wawili wa miaka saba na minne ndio pekee walionusurika katika mauaji hayo.
Vita vya kupigania haki yake vilikuwa vya muda mrefu na vya kutisha. Imethibitishwa kwamba baadhi ya maafisa wa polisi na serikali walijaribu kumtisha, ushahidi uliharibiwa na waliofariki kwa tukio hilo walizikwa bila uchunguzi wa miili.
Madaktari waliompima walisema hajabakwa, na alipokea vitisho vya kuuawa.
Wahusika walikamatwa kwa mara ya kwanza katika kesi hiyo mwaka wa 2004 baada ya Mahakama ya Juu ya India kukabidhi kesi hiyo kwa wachunguzi wa shirikisho.
Mahakama kuu pia ilikubali kwamba mahakama za Gujarat zisingeweza kutoa haki yake na kuhamishia kesi yake Mumbai. Vita ya kutafuta haki yake pia ilikuwa ya ikivuruga familia yake kwani wamelazimika kuhama nyumbani mara kadhaa.
"Bado hatuwezi kurudi nyumbani kwa sababu tunaogopa. Polisi na utawala wa serikali daima wamesaidia washambuliaji wetu. Tunapokuwa Gujarat, bado tunafunika nyuso zetu, hatutoi anwani zetu," mume wake alisemaa.
Wakati wa kesi, kulikuwa na wito wa hukumu ya kifo kwa washambuliaji wa Bilkis Bano, ikiwa ni pamoja na kutoka kwake mwenyewe.
Lakini baada ya mahakama kuu ya Mumbai kuwahukumu kifungo cha maisha, aliniambia "hakupenda kulipiza kisasi" na "anataka tu waelewe walichofanya." "Natumaini siku moja watatambua ukubwa wa uhalifu wao, jinsi walivyoua watoto wadogo na kubaka wanawake."
Lakini, aliongeza, alitaka "watumie maisha yao yote gerezani." Siku ya Jumanne, Bw Rasool aliliambia gazeti la Indian Express kwamba mkewe alikuwa "amefadhaika na anahuzuni". "Vita ambavyo tulipigana kwa miaka mingi vimemalizika mara moja," alisema. "Hatujapata hata wakati wa kutafakari habari hii na tunajua kuwa wafungwa tayari wamefika majumbani mwao."