Real Madrid v Manchester City: Namna Erling Haaland alivyogeuka mwanasoka mahiri duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Erling Haaland, nyota wa wa Norway mwenye umri wa miaka 22 tayari amefunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja tena wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kuliko mchezaji yoyote na ni mchezaji wa pili katika historia ya ligi kuu ya England kufunga mabao zaidi ya 50 katika mashindano yote kwenye msimu mmoja- na wa kwanza katika miaka 95 iliyopita.
Haya yote yanatokea ikiwa zimesalia mechi za lala salama kabla ya kampeni kumalizika, katika msimu wake wa kwanza wa ligi kuu hiyo baada ya kuhamia Manchester City akitokea Borussia Dortmund kwa pauni milioni 51.2 msimu uliopita.
Uchezaji mwingi wa Haaland umewasaidia mabingwa hao kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi na kuwania makombe matatu msimu huu, wakiingia fainali ya Kombe la FA na wako nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Haaland and wenzake wa City watakuwa dimbani Bernabeu leo Jumanne kwa mechi ya kwanza dhidi ya mabingwa hao wa Ulaya wakiwa na imani kwamba huu unaweza kuwa mwaka wao.
Tangu wakati wakimfundisha Lionel Messi huko Barcelona mbinu za Pep Guardiola zimetajwa kubebwa zaidi na uwepo wa mchezaji mmoja tu, lakini jambo la kutisha sasa kwa Ulaya nzima ni kwamba ubora zaidi wa Haaland unaendelea kutarajiwa.
Avunja rekodi za dunia akiwa na umri wa miaka mitano tu

Chanzo cha picha, Getty Images
Alizaliwa Leeds mwaka wa 2000, mtoto wa mlinzi wa zamani wa Nottingham Forest, Leeds na Manchester City Alf-Inge Haaland na mwanariadha Gry Marita Braut ambao ni kama wamezaliwa kuwa wanamichezo tangu utotoni.
Mnamo 2006, aliweka rekodi ya dunia kwa wachezjai wa umri wake kwa kuruka kwa muda mrefu zaidi akiruka mita 1.63. Alikuwa na umri wa miaka mitano.
Akiwa kijana - baada ya kurejea katika mji wa wazazi wake wa Norway wa Bryne n umri wa miaka mitatu - alikuwa winga mwembamba, mwenye kasi na aliyejituma sana.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Na hata wakati huo Haaland alikuwa mwanafunzi mwenye shauku ya mchezo huo wa soka, akiwafuatilia kw akaribu nyota kama Zlatan Ibrahimovic, Robin van Persie, Jamie Vardy, Messi na Mario Balotelli.
Wazazi walimruhusu Erling kukua kiasili zaidi na, alipokua anakuwa na kujiamini, alifanya vilevile kwa ukubwa na kiwango akiwa Byrne, klabu yake ya utotoni ambako alipitia katika timu zake za watoto.
Sasa ni mshambuliaji wa kati mwenye urefu wa futi 6 na inchi 4.
"Ninakimbia mbio zile zile nilikuw anakimbia nikiwa na umri wa miaka 13," anasema.
Kocha Alf-Ingve Berntsen, ambaye alimfundisha kwa miaka minane huko Bryne, alisema: "Akiwa na umri wa miaka 13, tayari niliona kwamba mtoto huyu angekuwa sehemu ya timu ya taifa ya Norway kwa maadili yake ya soka kujituma na busara."
Alicheza Molde FC kati ya mwaka 2017-19 chini ya ukufunzi wa Ole Gunnar Solskjaer, ambaye alimtengea saa kadhaa Haaland kumfundisha ana kwa ana, alimsaidia kumkuza na kukuza kipaji chake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Haaland alihamia Red Bull Salzburg mnamo 2019, akifunga mabao 25 katika mechi 23 ikijumuisha hat-trick ya ndani ya dakika 45 kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Genk ambayo ilikuwa uthubitisho mkubwa kwamba alikuwa katika kiwango bora.
Akahamia Borussia Dortmund kwa takriban euro 20m. Licha ya kuvivutia vilabu kama Manchester United na Juventus, mshambuliaji huyo alichagua klabu hiyo ya Ujerumani kwa kuangalia kwamba angepata muda zaidi wa kucheza kabla ya kufikiria timu kubwa.
Ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya kujiunga na mojawapo ya vilabu vikubwa zaidi duniani - huku Manchester City.
Haaland atakuwa na umri wa miaka 26 tu mkataba wake wa miaka mitano utakapomalizika na wengi wanatarajia huenda akaelekea Hispania na Italia kukamilisha hamu yake ya kupata mafanikio katika ligi kubwa zaidi ulimwenguni.
'Hakuna mchezaji aliyemshawishi Guardiola zaidi tangu Messi'

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata Haaland mwenyewe ameshangazwa kidogo na jinsi ameweza kufanya vizuri tena kwa haraka tangu ajiunge Etihad.
Moja ya sababu kuu za mafanikio yake ni mkufunzi wake, Ivar Eggja, ambaye anafanya kazi kwa ukaribu na baba yake na kufanya kazi ya ‘kumuwezesha’ mshambuliaji huyo – kwa kumtafutia nyumba, kumwangalia mlo wake na kumpa kila anachohitaji ili fikra zake ziwe ni soka tu.
Mpaka Haaland anatua Manchester, tayari alikuwa na kila kitu.
Kitu kikubwa kuhusu nyota huyu ni ukweli kwamba hajaridhika kamwe na mafanikio ya sasa- kila wakati anatafuta kuboresha.
Mkufunzi wa Manchester City Muitaliano Mario Pafundi anamsukuma lakini pia anamsaidia kuuelewa mwili wake. Hii ina maana kwamba Haaland hadi sasa ameepuka majeraha ambayo yalimrudisha nyuma mwaka jana akiwa klabu ya Borussia Dortmund.
Ameongeza kilo 12 za misuli katika kipindi cha miezi 15 iliyopita kutokana na programa anayopewa ukiacha vinasaba, mfano kiwango cha chakula bora, pamoja na mazoezi na mtindo wa maisha uliotulia unaojumuisha vipindi vya kutafakari ambavyo hutumia hakikisha akili yake iko mahali sahihi.
"Haaland anaishi saa 24 kama mwanasoka wa kulipwa, akijali na kuthamini kazi yake, mapenzi yake, na kile anachopenda," Guardiola alisema.












