Vita vya Ukraine: ‘Hakuna kusalimisha eneo lolote la Ukraine kwa Putin’- Zelensky

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amefutilia mbali uwezekano wa eneo lolote la nchi yake kukabidhiwa kwa Urusi katika makubaliano ya amani na taifa hilo .
Katika mahojiano na BBC kuadhimisha mwaka mmoja tangu uvamizi kamili wa Urusi, alionya kukubali ardhi ya nchi yake kutwaliwa na Urusi kutamaanisha kwamba Urusi inaweza "kurejea tena", wakati kuna uwezekano wa silaha za Magharibi kuleta amani karibu.
Bw Zelensky pia alisema mashambulizi yaliyotabiriwa ya kipindi cha masika tayari yameanza.
"Mashambulizi ya Urusi tayari yanatokea kutoka pande kadhaa," alisema.
Anaamini, hata hivyo, kuwa vikosi vya Ukraine vinaweza kuendelea kulinda ardhi ya nchi dhidi ya Urusi na kuwazuia wanajeshi wa Moscow kusonga mbele hadi watakapoweza kuanzisha mashambulizi - ingawa alirudia wito wake wa kuomba msaada zaidi wa kijeshi kutoka kwa nchi za Magharibi.
"Bila shaka, silaha za kisasa huharakisha amani. Silaha ndiyo lugha pekee ambayo Urusi inaelewa," Bw Zelensky aliambia BBC.
Alikutana na viongozi wa Uingereza na EU wiki iliyopita katika jitihada za kuimarisha uungwaji mkono wa kimataifa na kuomba silaha za kisasa ili kulinda nchi yake. Wakati rais wa Ukraine alipoomba ndege za kisasa za kivita, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alisema "hakuna kisichowezekana'.
Lakini Kyiv imezidi kuchanganyikiwa na kasi ambayo silaha za Magharibi zimewasili. Uwasilishaji wa mizinga ya vita - iliyoahidiwa mwezi uliopita na nchi nyingi za Magharibi , ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Marekani na Uingereza - bado haijafika wiki kadhaa kwenye uwanja wa vita.
Rais Zelensky pia alizungumzia tishio la kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko la kuanzisha vita pamoja na wanajeshi wa Urusi kutoka katika eneo lake ikiwa mwanajeshi mmoja wa Ukraine atavuka mpaka.
"Natumai [Belarus] haitajiunga na [vita]," alisema. "Ikitokea, tutapigana na tutanusurika." Kuruhusu Urusi kutumia Belarus kama kituo cha kutayarisha mashambulizi tena itakuwa "kosa kubwa", aliongeza.

Chanzo cha picha, BBC/GOKTAY KORALTAN
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vikosi vya Urusi vilizindua sehemu ya uvamizi wao kamili kutoka Belarus miezi 12 iliyopita.
Vilielekea kusini kwenda mji mkuu wa Ukraine Kyiv lakini walipigwa vita na kurudishwa nyuma ndani ya wiki chache, baada ya kupata hasara kubwa.
Alipoulizwa ikiwa alishangazwa na mbinu za Urusi katika vita hivyo, Bw Zelensky alizitaja kuwa "zisizo na thamani".
"Jinsi walivyoharibu kila kitu. Ikiwa askari wao walipokea [na kutekeleza] maagizo hayo, hiyo inamaanisha wana maadili sawa."
Takwimu za Ukraine zilizotolewa wiki hii zilionyesha kuwa wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine wanakufa kwa idadi kubwa mwezi huu kuliko wakati wowote tangu wiki ya kwanza ya uvamizi wao. Takwimu haziwezi kuthibitishwa, lakini Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema mwelekeo huo "huenda ni sahihi".
"Leo, kuishi kwetu ni umoja wetu," alisema Bw Zelensky juu ya jinsi alifikiri vita vitaisha. "Naamini Ukraine inapigania maisha yake." Nchi yake ilikuwa ikielekea Ulaya kiuchumi, na pia kupitia maadili yake, alisema.
"Tulichagua njia hii. Tunataka hakikisho la usalama. Maelewano yoyote ya kimaeneo yatatufanya kuwa dhaifu kama taifa."
"Sio kuhusu maelewano yenyewe," alisema. "Kwa nini tutaogopa hilo? Tuna mamilioni ya maelewano katika maisha kila siku.
"Swali ni kwa nani? Kwa Putin? Hapana. Kwa sababu hakuna uaminifu. Majadiliano naye? Hapana. Kwa sababu hakuna uaminifu."














