Hivi ndivyo unavyoweza kukabiliana na 'magumu' ya Januari

Na Yusuph Mazimu

BBC Swahili

‘Januari ngumu sana’, huu mwezi dume’, hali ngumu mwezi huu’, haya ni maneno ya kawaida kabisa kuyasikia unapofika mwezi wa Januari wa kila mwaka.

Lakini Januari ya kwa huu inaweza kuwa ngumu zaidi hasa kiuchumi klutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita na migogoro inayoendelea duniani, athari za Covid_19 na mabadiliko ya tabia nchi.

Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF linasema kuwa uchumi wa dunia utakabiliwa na wakati mgumu zaidi mwaka huu wa 2023.

Ripoti zinaonyesha ukuaji wa uchumi duniani kwa mwaka 2023 unatarajiwa kuporomoka kwa asilimia 2%, huku mihimili mikubwa kichumi nchi kama China, Marekani na Umoja wa Ulaya, zikishuhudia kusuasua kwa shughuli zao.

Kwa mantiki hiyo, kuanzia Januari hii mpaka Disemba gharama za maisha zitaendelea kushuhudiwa zikiongezeka pamoja na mfumuko wa bei kupaa kwa baadhi ya bidhaa, hali iliyoanza kushuhudiwa kwa bidhaa katika mataifa hata ya Afrika Mashariki.

Bidhaa kama mchele, mafuta ya kula na hata bidhaa zingine kama mafuta ya petroli na dizeli, bei zake zimeendelea kuwa juu kulinganisha na miaka miwili iliyipita.

Kuna haja ya kuitazama Januari yako na namna unavyoweza kuikabili Januari ya sasa na Januari ijayo.

Kinacholiza watu Januari

Kwa maisha ya watu wenye kipato cha chini na kipato cha kati Januari ni wakati wanaolia na masuala ya ada, pango la nyumba, pango la vibanda vya biashara na matumizi mengine ya msimu ikiwemo kilimo.

Ni kipindi chenye mahitaji makubwa ya kifedha, lakini kwa upande wa kipato wengi husalie na kile kile ama kupungua zaidi. Ni mwezi unaofuata baada ya mwezi wa Disemba ambao unakuwa na shughuli nyingi za kijami na kifamilia. Ni mwezi wa shamrashamra wa sikukuu za mwisho wa mwaka, krismasi na mwaka mpya, sikuu zinazotumia gharama kubwa pia kwenye kuzishehereka.

‘Wengi hatupangi mambo yetu, inapofika Disemba, hujasevu kitu, umetumia zaidi kufurahia mwaka na hicho kinakuwa kilio kwa mwezi Januari, hayo ndo maisha yetu’, anasema Joel Mushi, mkazi wa Dar es Salaam.

Mwandishi mwandamizi wa BBC, Leonard Mubali ambaye amekuwa akifuatilia masuala ya uchumi na jamii anasema ‘ Januari inabebwa na mshahara wa mwezi Disemba, kwa wale wanaofanya kazi, na mshahara wa Disemba kwa taasisi nyingi hasa binafsi hutoka mapema, na huisha mapema pia, na hicho kinasababisha ugumu wa Mwezi Januari kwa wengi’.

Nini cha kufanya Januari?

Kwa kifupi Januari ni mwezi uliokaa ‘kimtego’ linapofika suala la kipato na mahitaji muhimu. Na Januari ya sasa haitatofautiana sana na Januari nyingine yoyote katika suala la mahitaji. Muhimu ni kujiuliza utawezaje kuabiliana na ugumu wa Januari, ama kuifanya Januari yako kuwa nyepesi?

1. Usifiche yanayokukabili

Kama kuna donda linaloweza kukutafuna na kukumaliza basi ni kuficha masuala yanayokukabili, kuficha masaibu yako yakiwemo ya kijamii na kufikiria kwamba unaweza kuyabeba peke yako. Fahamu hauko peke yako kwenye changamoto za Januari, kinachotofautisha changamoto zako na za jirani yako, jamaa yako au mtu mwingine yoyote ni ukubwa tu wa changamoto.

Lakini ukweli na uwazi wako kwa yanayokusibu mbele ya ndugu, marafiki na jamaa zako huenda ikakupa mwanga. Nenda shuleni kwa mtoto kaeleze ukweli umekwama, usifiche na huenda mkakubaliana na walimu namna ya kulipa kwa kiasi na kwa muda fulani.

Si dhambi kusema ‘sina ada ya mtoto wangu na sijui nitapata wapi, hapa kichwa kinaniuma’ , jibu lolote utakalopata linaweza kukupa mwanga wa safari yako ya Januari.

Liwe jibu baya, utajua ukaze buti, likiwa zuri itakupa unafuu. Sema usiache kusema.

Japo sio wote watakaokusaidia au kupenda kusikia matatizo yako, Kugesha anasema ‘ wewe sema tu, itakupunguzia mzigo kwenye kifua chako na kichwani kwako, ambaypo ni bora kwa afya yako ya akili’.

2. Toka nje, usijifungie

Kukaa mahali pamoja kunaweza kukuongezea ugumu zaidi wa kufikiria magumu yako na mawazo ya yale unayopitia ukiwa huna njia ya karibu na rahisi ya kuyatatua. Kutoka nje kutembea hasa kwneye sehemu ambazo kuna vitu vya asili kutakusaidia kukupa haueni

Mtaalam wa afya Uingereza, Hellen Garr, aliwahi kunukuliwa na mtandao wa masuala ya afya wa bmj.com akisema kutoka na kwenda mahali kukutana na vitu vya asili kama maji ya bahari, mto au ziwani au ukatembelea sehemu nzuri yenye miti ya asili ni dawa tosha ya afya ya akili. Kwa sababu wakati huu msongo ulionao wa ada unatikisa afya ya akili.

Garr anasema utulivu wa akili unaweza kukupa akili ya kufikiria namna ya kutatua tatizo.

Hili linaungwa mkono na Raphael Kugesha, mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa Jamii kutoka Tanzania anayeongeza ‘Lakini kutoka nje na kutembea huku na huko, kunaweza kukusaidia kukutana na watu, ambao huenda ukapata mbinu ya namna ya kutoka, wanasema kwenye wengi hakuharibiki neno’.

3. Omba msaada

Kuomba msaada ni njia inayotumika sana na wengi. Inasaidia, inafanya kazi ingawa inaweza isifanye kwa kila mtu. Wapo ndugu jamaa na marafiki wenye uwezo na moyo wa kusaidia wanaweza kukusaidia hata kama sio kwa kiwango unachotraka, lakini unaweza kusaidika kiasi.

Wengine wanaweza kukupa msaada kwa kukukopesha fedha ama kukuazima, usijali kama iko ndani ya uwezo wako fanya hivyo, ili kuisukuma Januaria yako.

‘Kama umekwama kabisa, inaruhusiwa kusogeza matatizo mbele, azima au kopa mahali pesa utarudisha baadaye ili utatue shida zako za muhimu sasa’, anasema Mubali.

4. ‘fanya kile kilicho sahihi kwako’

Januari ni wakati ambao, wengi wanakua wanatingwa na mengi kichwani. Ni wakati tishio wa afya yako ya akili. Watalaam wanasisitiza kuwa ‘fanya kile kilicho sahihi kwako’ sio sahihi kwa watu wengine, kwa mujibu wa Andrew Molodynski, mtaalam wa magonjwa ya akili na mhadhiri wa chuo kikuu cha Oxford kama alivyonukuliwa na mtandao wa afya wa bmj.com. 

Mambo mengine yanayosisitizwa na wataalamu wa afya, uchumi na mipango kwa ajili ya Januari yao ngumu ni kujipa muda wa kufanya mazoezi, kufanya zaidi vitu unavyopenda, kuwa na mipango kulingana na uwezo wako na fanya kile kilicho ndani ya uwezo wako, usichune ngozi kwa sababu umeshindwa kulipa ada ama kodi ya pango kwa chumba ama nyumba unayokaa.

5. Usikate tamaa

Kukata tamaa ni msumari wa mwisho kwenye jeneza lako. Kukatabtamaa uwe msamiati wa mwisho kuusikia, usiuruhusu kwenye kichwa na akili yako kwa sasa. Jipe moyo japo moyo wa shida. Usikate tamaa hata kama una hofu ya kushindwa kuyakabili matatizo yako ya Januari. Usichague kabisa kukata tamaa

Aliwahi kunukuliwa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ‘Daima inaonekana (jambo fulani ) haliwezekani hadi pale litakapofanikiwa’. Hakuna kitu kigumu chini ya jua.

6. Ifanye Januari kuwa sawa na Septemba au Machi

Si dhana inayoweza kukubalika na wengi, lakini inaweza kukusaidia kama uzito wa mwezi Januari utaufanya kuwa sawa na uzito wa mwezi mwingine wowote. Kwa nidhamu ya kipato na matumizi yako.

‘Unaweza kuikabili Januari ya mwakani kuanzia Januari ya sasa, usiisubiri Januari ifike ili uanze kuikabili, unaweza kuikabili ila kwa kiwango cha kuumiza kiasi, Jaribu kuitumia Januari kuifikiria na kuikabilia Januari ijayo’, anashauri Kugesha.

Kwa mantiki ya wakati, Januari si sawa na miezi mingine katika mwaka. Lakini kwa mantiki ya kukabiliana na maisha yako, ufanye mwezi Januari kama mwezi mwingine wowote, uwe Septemba, Disemba au Novemba.

Panga mambo yako ya mwaka mzima sasa, ikiwemo namna utakavyosheherekea sikukuu yako ya kuzaliwa na sikukuu za mwisho wa mwaka, bila kuathiri Januari yako ijayo.