'Sio wapelelezi, ni Mama na Baba': Mtoto wa wanandoa wanaoshikiliwa Iran

D

Chanzo cha picha, FAMILIA

Maelezo ya picha, Craig na Lindsay Foreman, seremala na mkufunzi, wanazuiliwa nchini Iran kwa tuhuma za ujasusi.
    • Author, Maia Davies
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mtoto wa kiume wa wanandoa wa Uingereza wanaozuiliwa nchini Iran amesema aliangua kilio alipopata habari kuhusu kukamatwa kwao na hajapata tena mawasiliano nao kwa muda wa miezi sita.

Craig na Lindsay Foreman walikuwa kwenye safari ya pikipiki kuzunguka ulimwengu wakati walipokamatwa mwezi Januari na baadaye kushtakiwa kwa ujasusi, jambo ambalo familia yao inakanusha.

Mtoto wao Joe Bennett aliiambia BBC Breakfast: "Nataka kuwa wazi, wazazi wangu si wapelelezi, hawahusiki na siasa, si wahalifu. Ni Mama na Baba."

Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), imesema inaendelea kuisaidia familia na kuwasilisha malalamiko moja kwa moja kwa Iran.

Bw na Bi Foreman, wote wana umri wa miaka 52 kutoka East Sussex, walikuwa wakiendesha pikipiki kutoka Uhispania hadi Australia walipovuka mpaka na kuingia Iran tarehe 31 Desemba.

Bw. Bennett anasema mara ya mwisho alizungumza na wazazi wake tarehe 3 Januari kabla ya kukamatwa kwao, alijua kuwa wamekamatwa mwishoni mwa Januari na kushtakiwa kwa ujasusi mwezi Februari.

"Sikujua nifanye nini au nielekee wapi," anasema.

Bennett anasema "barua" moja iliyoandikwa na mama yake kabla ya kushikiliwa ilisambazwa na marafiki na familia tangu wakati huo, na taarifa kuhusu hali zao zilitolewa mara tatu na maafisa wa ubalozi wa Uingereza - ya mwisho ilikuwa Mei.

"Ni vigumu ikiwa umezoea kusikia sauti ya mtu kila siku," anasema Bennett.

"Analala juu ya godoro jembamba," alisema kuhusu mama yake, "hilo husababisha shida nyingi."

Pia unaweza kusoma

Wakati wa vita

d
Maelezo ya picha, "Sio wahalifu - ni mama na baba tu," ansema mtoto wa wao
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anasema mzozo kati ya Iran na Israel uliozuka mwezi Juni, kilikuwa ni kipindi cha "kutisha," "hatukuwa tunajua wakati huo ikiwa wako salama au la."

Wanandoa hao walipaswa kupelekwa katika Gereza maarufu la Evin huko Tehran tarehe 8 Juni, ambalo lililipuliwa na Israel tarehe 23 Juni. Vita hivyo pia vilishuhudia Uingereza ikiondoa wafanyakazi wake wa ubalozi katika jiji hilo.

Bennett anakumbuka akifikiria: "Sasa wameachwa peke yao, hakuna watu ambao wanaweza kujua usalama na ustawi wao."

Amesema Ofisi ya Mambo ya Nje lazima ichukue hatua za haraka kuwarudisha nyumbani, akiongeza kuwa "hawako wazi" juu ya mkakati wao wa kufanya hivyo.

Kwa sasa FCDO inashauri watu wasiende Iran, inasema raia wa Uingereza au wenye uraia wa Uingereza-Irani wako katika "hatari kubwa" ya kukamatwa, kuhojiwa au kuwekwa kizuizini.

Pia ofisi hiyo inasema msaada wa serikali ya Uingereza "ni mdogo sana nchini Iran."

"Hakuna usaidizi wa ana kwa ana wa kibalozi utakaowezekana wakati wa dharura na serikali ya Uingereza haitaweza kukusaidia ikiwa utapata shida nchini Iran," unasema mwongozo huo.

Bennett anasema familia ilikuwa na mashaka kuhusu uamuzi wao wa kusafiri kwenda katika nchini hiyo na wakauliza, "kwa nini mnaenda huko?"

Anasema wanandoa hao walifanya safari yao "kwa njia sahihi" - kwa viza sahihi, wakiambatana na waongoza watalii wenye leseni, na kukaa katika hoteli kando ya barabara kuu.

"Walifuata kila mwongozo ulivyoelezwa katika kitabu... na hilo halikutosha."

Bennett anaamini walikamatwa kwa sababu "wana pasi za kusafiria za Uingereza na zinatumiwa na serikali ya Iran kama njia ya mtaji wa kisiasa."

Tuhuma dhidi yao

Msemaji WA serikali ya Iran alisema mwezi Februari, wanandoa hao waliingia Iran "chini ya kivuli cha watalii" na "kukusanya habari" katika maeneo kadhaa ya nchi.

Amesema wanandoa hao walikuwa wakifuatiliwa na mashirika ya kijasusi na walikamatwa katika "operesheni iliyoratibiwa ya kijasusi."

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imewakamata makumi ya Wairani wenye uraia wa nchi mbili au ukaazi wa kudumu wa nchi ya kigeni, wengi wao wameshtakiwa kwa ujasusi na makosa yanayohusu usalama wa taifa. 15 kati yao wana uhusiano na Uingereza.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mara nyingi yanashikiliwa kama mtaji, na huachiwa pale Iran inapopokea kitu kama malipo.

Bennett amesema ofisi ya masuala ya kigeni imekuwa "ikiwaunga mkono kwa maneno na Faraja.”

Aliongeza kuwa mbinu yao ya "diplomasia ya utulivu" imekuwa "ikiendelea kwa muda mrefu" na familia haijawekwa "wazi mkakati wao ni nini."

"Tunajua tunasimama wapi na tunataka nini, ni kazi yao sasa kufanikisha hili."

Msemaji wa FCDO amesema: "Tunaendelea kuwasilisha kesi hii moja kwa moja kwa mamlaka ya Iran, tunawapa usaidizi wa kibalozi na tunaendelea kuwasiliana kwa karibu na familia."