Vita vya Ukraine: Familia ya Zambia yadai majibu kutoka Urusi kuhusu kifo cha kijana wao

Lemekhani Nyirenda

Chanzo cha picha, ZAMBIANS IN MOSCOW/ FACEBOOK

Kifo cha mwanafunzi wa Zambia mwenye umri wa miaka 23 ambaye alikuwa ameandikishwa kuipigania Urusi nchini Ukraine kimeiacha familia hiyo ikiwa na huzuni, dada yake mkubwa ameaimbia BBC.

Sio tu kwamba amekufa bali pia maswali yasiyo na majibu kuhusu kifo cha kikatili cha kijana huyo katika nchi ya kigeni.

Lemekhani Nyirenda alikuwa akitumikia kifungo kinachohusiana na dawa za kulevya nchini Urusi lakini aliachiliwa na kupelekwa mstari wa mbele nchini Ukraine. "Tunataka kujua aliandikishwaje bila familia yake kujulishwa? Je, alilazimishwa?" aliuliza Muzang'alu Nyirenda.

Familia ilihisi "imeibiwa" na kifo cha kaka yake, aliongeza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia Stanley Kakubo alitangaza Jumatatu kwamba Bw Nyirenda, ambaye alikuwa akisoma katika Taasisi ya Fizikia ya Uhandisi ya Moscow, alikuwa akitumikia kifungo cha miaka tisa jela kwa kosa la kutumia dawa za kulevya.

Alisema Bw Nyirenda aliuawa kwenye mstari wa mbele mwezi Septemba, lakini mamlaka ya Urusi ilikuwa imetoka tu kufahamisha Zambia kuhusu kifo hicho.

Bw.Kakubo alisema kuwa Zambia ilidai majibu kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo na kwa nini alitumwa Ukraine. Wazambia wengi wameshtushwa na habari hizo, lakini pia wamechanganyikiwa kwamba serikali haijatoa taarifa zaidi kueleza hali iliyosababisha mwanafunzi huyo kupelekwa Ukraine.

Vita vya Ukraine vinasemekana kugharimu maisha ya makumi ya maelfu ya watu

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wa Bi.Nyirenda, kaka yake alisafiri hadi Urusi mnamo 2019 kusomea uhandisi wa nyuklia kwa ufadhili wa serikali, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ambao ulianza miaka mingi nyuma. "Kuna mengi ambayo hatuyajui. Kwa nini serikali ya Zambia haikujua kwamba anapelekwa vitani kupigana?" dada yake mkubwa aliiambia BBC. "Watu waliompeleka kwenye vita hivyo walitudharau kama familia, hakuwa kitu kwao. Walimtumia," alisema.

Dawa za kulevya na kukamatwa

Bw.Nyirenda alikuwa akifanya kazi kama msafirishaji wa muda alipokamatwa mwaka wa 2020 akiwa na kifurushi kilichokuwa na dawa za kulevya, dada yake alisema. "Tunaamini alikuwa hajui kilichomo kwenye kifurushi alicholeta, alituambia hajui. alikuwa akipata ujumbe kwa ajili ya kuchukua mizigo na maelekezo ya mahali pa kuipeleka," alisema. "

Wakati mmoja alizuiliwa na polisi na kupekuliwa na wakapata dawa kwenye kifurushi. Alieleza kuwa alikuwa akifanya kazi kwa msafirishaji mtandaoni na hakujua kuhusu vifurushi hivyo lakini alikamatwa," Bi Nyirenda alisema.

Familia, hata hivyo, daima ilibaki na matumaini kwamba angerudi nyumbani salama. Lakini alipokuwa akitumikia kifungo chake katika gereza la usalama aliandikishwa, familia yake inaamini, na Wagner Group, kundi la mamluki la Urusi ambalo limekuwa likiwaandikisha wafungwa kupigania Urusi nchini Ukraine ili wapate uhuru wao.

Mnamo Septemba, picha zilizovuja zilionesha Yevgeny Prigozhin, mkuu wa kikundi cha Wagner, akielezea sheria za mapigano, kama vile kutotoroka au kujamiiana na wanawake wa Ukraine, na kisha kuwapa wafungwa dakika tano kuamua ikiwa wanataka kujiandikisha.

Aliwaambia wafungwa angewatoa gerezani wakiwa hai lakini akasema hangeweza kuwaahidi kuwarudisha wakiwa hai.

Wameiba ndugu yangu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lemekhani ambaye alizaliwa na wataalamu wa chuo kikuu Edwin na Florence Nyirenda, alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne. Hata alipokuwa gerezani alipata njia ya kuwasiliana na wapendwa wake huko Zambia.

Mara ya mwisho wazazi wake kumsikia ilikuwa tarehe 31 Agosti kwenye simu ya siri ambayo iliwajaza wasiwasi. "Aliwaambia wazazi wangu: "Siko tena gerezani lakini nilipo ni siri." Wazazi wangu walikuwa na wasiwasi, sote tulikuwa wakati alipokuwa akishiriki hili. Tulijua alikuwa mfungwa katika nchi ya kigeni ambako hakuwa na haki. tulikuwa na wasiwasi kuhusu kinachoendelea lakini hakuweza kuwaeleza zaidi na wazazi wangu hawakuchunguza zaidi,"

Bi Nyirenda alisema. Familia iliarifu mamlaka ya Zambia kuhusu simu hiyo isiyo ya kawaida na kuhakikishiwa uchunguzi kuhusu mahali alipo, lakini miezi kadhaa baadaye taarifa za kifo cha kijana huyo zilitolewa.

"Alikuwa mdogo, waliyachukua maisha yake mbali naye. Ana kaka pacha, wameiba nusu nyingine ya kaka yangu," dada yake alisema huku akitokwa na machozi. "Lemekhani alikuwa na mipango mingi sana. Alikuwa na mipango ya kusaidia kuijenga Zambia. Wametuibia," alisema. "Hakuna kufungwa, ni maswali tu. Tunamtaka nyumbani ili tumlaze kwa amani.

Tunataka arudi na watu wanaompenda lakini tunastahili majibu," alisema Bi Nyirenda. Mwili wake, kwa mujibu wa maafisa wa Zambia, umesafirishwa hadi katika mji wa mpakani wa kusini mwa Urusi wa Rostov kwa maandalizi ya kurejeshwa Lusaka ambako familia yake itamzika.

Maswali zaidi ya BBC kwa wizara ya mambo ya nje ya Zambia hayajajibiwa.

Zambia imechukua msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita vya Russia na Ukraine, kama nchi nyingine nyingi za Afrika, lakini inasema inalaani aina yoyote ya vita.