Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni silaha gani zilitumika katika mashambulio ya Iran na Israeli ilizuiaje?
Kwa mara ya kwanza Iran ilifanya mashambulizi dhidi ya Israel.
Usiku wa manane siku ya Jumamosi, ving'ora vilisikika nchini Israel kutahadharisha kuhusu mashambulizi ya anga, wakazi walishauriwa kutafuta makazi, na milipuko ilisikika huku ulinzi wa anga ukianza.
Vizuizi hivyo viliangaza anga wakati wa usiku katika maeneo kadhaa kote Israel, huku washirika wake wakiangusha ndege nyingi zisizo na rubani na makombora kabla ya kufika Israel.
Takribani nchi tisa zilishiriki katika shughuli hiyo ya kijeshi; Makombora yalirushwa kutoka Iran, Iraq, Syria, na Yemen, na yaliangushwa na Israel, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Jordan.
Mfumo wa kombora wa Iron Dome wa Israel unafanya kazi vipi?
Haya ndiyo tunayoyajua kuhusu shambulio hilo hadi sasa.
Mashambulizi na droni, balestiki na makombora
Jeshi la Israel lilisema Jumapili kwamba Iran imerusha zaidi ya ndege 300 zisizo na rubani na makombora kuelekea Israel.
Msemaji wa jeshi Daniel Hagari amesema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni kuwa shambulio hilo lilijumuisha ndege zisizo na rubani 170 na makombora 30 ya baharini ambayo hakuna hata moja lililoingia katika ardhi ya Israel na makombora 110 ya balestiki ambayo idadi ndogo ya makombora hayo yalifika Israel.
BBC haijathibitisha takwimu hizi kwa uhuru.
Umbali mfupi zaidi kutoka Iran hadi Israel ni takribani kilomita 1,000 (maili 620) kupitia Iraq, Syria na Jordan.
Mashambulizi kutoka nchi kadhaa
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran lilisema Jumamosi jioni kwamba limerusha ndege zisizo na rubani na makombora.
Vyanzo vya usalama vya Iraq viliiambia Reuters kwamba makombora yalionekana yakiruka juu ya anga ya Iraq kuelekea Israel.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran lilieleza kuwa makombora hayo ya balistiki yalirushwa takribani saa moja baada ya kurushwa kwa ndege zisizo na rubani, kiasi kwamba yalifika Israel karibu wakati huo huo.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema kuwa vikosi vya Marekani vilinasa makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen.
Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon lilitangaza kuwa pia limerusha makombora mawili katika kambi ya kijeshi ya Israel katika eneo la Golan Heights linalokaliwa kwa mabavu ambalo Israel ililiteka kutoka Syria, hatua ambayo haikutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
Israel na washirika wake wazuia ndege zisizo na rubani na makombora mengi
Mkuu wa majeshi ya wanamaji, Hagari alisema kuwa takribani asilimia 99 ya makombora yaliyoingia yalinaswa ama nje ya anga ya Israel au juu ya Israel.
Mizinga hiyo ilijumuisha ndege zisizo na rubani na makombora ya kusafiri, ambayo hufuata njia iliyonyooka, na makombora mengi ya balestiki.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema majeshi ya Marekani "yaliisaidia Israel kuangusha karibu ndege zote" zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa na Iran siku ya Jumapili.
Ameongeza katika taarifa yake kuwa Marekani ilisafirisha ndege na meli za kivita hadi eneo hilo kabla ya shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea.
Vyombo vya habari vya Iran vinathibitisha jukumu la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran kukamata meli "iliyohusishwa na Israel"
Vyanzo vya usalama viliiambia Reuters kwamba vikosi vya Marekani, vinavyofanya kazi kutoka kwenye vituo visivyojulikana katika eneo hilo, vilidungua ndege kadhaa zisizo na rubani za Iran kusini mwa Syria karibu na mpaka na Jordan.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alithibitisha kuwa ndege ya jeshi la anga la Uingereza pia ilidungua idadi kadhaa ya ndege zisizo na rubani za Iran. Sunak alisema shambulio la Iran lilikuwa "ongezeko la hatari na lisilo la lazima, ambalo ninalaani vikali."
Kuhusu Jordan, ambayo ina mkataba wa amani na Israel licha ya kukosolewa vikali kwa vita vya Gaza, pia ilinasa vitu vilivyoingia kwenye anga yake ili kuhakikisha usalama wa raia wake, kulingana na taarifa ya Baraza la Mawaziri la Jordan.
Jeshi la Israel lilisema Ufaransa ilisaidia kufanya doria za anga, lakini haijabainika iwapo ilidungua ndege zisizo na rubani au makombora.
Idadi ya makombora yaliyofika Israel na uharibifu uliofanywa
Huko Jerusalem, waandishi wa BBC waliripoti kusikia ving'ora na kuona mfumo wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome wa Israel ukifanya kazi, ambao unatumia rada kufuatilia makombora na kutofautisha kati ya yale ambayo yanaweza kugonga maeneo ya makazi na yale ambayo hayawezi.
Kilitokea nini Israel baada ya shambulio la Iran?
Makombora ya interceptor hurushwa tu kuelekea kwenye makombora ambayo yanatarajiwa kulenga maeneo yenye watu wengi.
Admiral Hagari alisema kuwa idadi ndogo ya makombora ya balistiki yalipenya anga ya Israel na kushambulia eneo hilo.
Hagari alieleza kuwa "moja ilisababisha uharibifu mdogo" kwenye kituo cha anga cha Nevatim katika jangwa la Negev kusini mwa Israel, akiongeza kuwa kituo hicho "bado kinafanya kazi," huku Shirika rasmi la Habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilisema kuwa shambulio hilo lilikabiliana na "pigo kali" kwenye kambi ya anga.
Admiral Hagari alisema msichana mwenye umri wa miaka 10 alijeruhiwa vibaya na vipande vipande. Iliripotiwa kuwa msichana huyo ni wa Wabedui wa Kiarabu karibu na mji wa kusini wa Aradi. Alijeruhiwa baada ya kukutwa ndege isiyo na rubani ya Iran, na kuhamishiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Jordan pia ilisema kwamba baadhi zilianguka kwenye eneo lake "bila kusababisha uharibifu wowote au majeraha yoyote kwa raia."
Kinachoendelea sasa
Kituo cha televisheni cha Israel cha Channel 12 kilimnukuu afisa mmoja wa Israel ambaye hakutajwa jina akisema kutakuwa na "jibu kubwa" kwa shambulio hilo.
Anga ya Israel imefunguliwa tena, kama ilivyo kwa nchi jirani, lakini Waziri wa Ulinzi Yoav Galant alisema makabiliano na Iran "bado hayajaisha."
Wakati huo huo, Iran iliionya Israel kwamba jibu lake "litakuwa kubwa zaidi kuliko hatua ya kijeshi usiku wa leo ikiwa Israel itajibu Iran," Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Mohammad Bagheri aliiambia televisheni ya taifa.
Bagheri alisema kuwa vituo vya Marekani vitashambuliwa ikiwa Marekani itashiriki katika majibu ya Israel.
Kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran Hossein Salami pia alisema kuwa Tehran itajibu shambulio lolote la Israel linalolenga maslahi yake, maafisa au raia.
Je, Iran ilitaka kuwasilisha ujumbe gani kupitia mashambulizi yake dhidi ya Israel?
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepangwa kukutana takriban 20:00 GMT kujadili mzozo wa hivi punde, kwa ombi la Israel.
Biden alisema pia atakutana na viongozi wa Kundi la nchi Saba kuu siku ya Jumapili, ili kuratibu "mwitikio wa kidiplomasia" kwa shambulio la Iran.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga