Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zambia-Egypt: Kukamatwa kwa fedha na dhahabu zisizojulikana mmiliki wake
Ndege ya kibinafsi iliyopatikana na zaidi ya dola za kimarekani milioni 5 pesa taslimu, dhahabu bandia, bunduki na risasi inachunguzwa katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka.
Kila mtu anajua ndege hiyo iliruka kutoka mji mkuu wa Misri, Cairo, na kutua nchini Zambia wiki mbili zilizopita, lakini hapo ndipo taarifa zinapoishia. Hadi sasa hakuna mtu nchini Misri au Zambia anayekubali aliikodi au kumiliki vilivyomo ndani yake.
Pamoja na maswali mengi uvumi usio na majibu umekuwa ukivuma.
Je, wanaohusika wanaweza kuwa viongozi wa kisiasa au kijeshi wa ngazi za juu wa Misri au Zambia? Je, hii ilikuwa safari yake ya kwanza kushikwa kati ya mamia ambazo hazikushikwa?
Kinachojulikana ni kwamba Wamisri wote sita waliokuwemo ndani ya ndege hiyo na wengine waliojiunga nao katika uwanja wa ndege wa Lusaka wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.
Baadhi ya Wazambia wanaoshikiliwa wamefunguliwa mashtaka ya ujasusi na kujipatia fedha kwa njia za uongo. Wamisri bado hawajafunguliwa mashtaka.
Mwana habari atoweka
Ulimwengu ungeendelea kutojua kama si mwandishi wa habari ambaye tovuti yake ya Matsda2sh, iliwashutumu maafisa wa Misri kwa kuhusika na tukio hilo.
Mara tu baada ya hapo vikosi vya usalama vya Misri vilivyovalia kiraia vilivamia nyumba ya Karim Asaad, Cairo usiku wa manane na kumkamata. Mwanzoni alitoweka tu. Hakuna aliyejua ni wapi yupo au kwa nini Bw Asaad alichukuliwa.
Kisha waandishi wa habari wa kujitegemea wa Misri walichapisha nyaraka kwenye mitandao ya kijamii zinazodaiwa ni za uchunguzi wa polisi wa Zambia kuhusu ndege hiyo iliyojaa fedha.
Waliozichapisha waliwataja maafisa watatu wa kijeshi wa Misri na afisa mkuu wa polisi miongoni mwa waliokamatwa huko Zambia.
Msururu wa maandamano kwenye mitandao ya kijamii, mengi yakiwa ni ya wanahabari wenzake, yalipelekea kuachiliwa kwake siku mbili baadaye.
Mara tu baada ya hapo mwangaza ulihamia Zambia baada ya ndege kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kenneth Kaunda wa Lusaka.
Inaonekana, mwanamume Mzambia aliyebeba mifuko inayoonekana kuwa na dhahabu aliruhusiwa kupita uwanja wa ndege na kukutana na Wamisri waliowasili kwenye ndege.
Hakuna anayeonekana kujua ni nani aliyeidhinisha hili lakini, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Zambia, zawadi ya pesa ilisaidia kurahisisha njia yake.
Baada ya kupanda ndani ya ndege mtu huyo inadaiwa aliuza sehemu ya dhahabu aliyokuwa amebeba kwa wanaume waliokuwa kwenye ndege.
Jambo ambalo halijabainika ni iwapo walifanikiwa kugundua kuwa kile alichokuwa akiuza kilikuwa ghushi kabla ya maafisa wa usalama kufika kupekua ndege hiyo.
Maafisa kadhaa walioingia kwenye ndege hiyo wanachunguzwa kwa madai ya kupokea hadi dola 200,000 kila mmoja kutoka kwa raia hao wa Misri waliokuwa ndani ya ndege. Inadaiwa hayo yalikuwa malipo yao kwa kuruhusu ndege hiyo kupaa bila kumkamata mtu yeyote.
Habari ziliposikika kwamba pesa nyingi kwenye ndege hiyo zinagaiwa, kundi jengine la maafisa wa usalama lilivamia ndege hiyo na kuwakamata waliokuwa ndani.
Kitendawili cha dhahabu
Yumkini washukiwa hao walipata shida kueleza walichokuwa wakifanya na mamilioni ya pesa, bastola kadhaa, risasi 126 na kile kinachoonekana kuwa zaidi ya kilo 100 za dhahabu.
Inaonekana Wamisri waliokuwemo ndani ya ndege wanaweza kuwa wameokolewa dhidi ya utapeli.
Wakili wa Zambia anayesimamia mmoja wa watu 10 waliokamatwa alisema kitendawili kingine ni kwa nini vikosi vya usalama vilionekana havijui hesabu.
Makebi Zulu aliambia BBC kwamba mwanzoni polisi walisema wamepata dola za kimarekani milioni 11 pesa taslimu. Baadaye ilishushwa hadi dola milioni 7 kabla ya kuwa dola milioni 5.7.
Sababu moja inaweza kuwa karibu nusu ya pesa zilitolewa kwenye ndege kabla ya timu iliyowakamata kuwasili.
Mvujisha taarifa
Bw Zulu pia amechanganyikiwa kuhusu jinsi watu hao walivyotendewa tangu wakamatwe. Anasema kwamba wakati Mzambia na wageni wengine watatu walipopelekwa jela kusubiri siku yao mahakamani, Wamisri hao sita waliwekwa katika nyumba ya wageni.
Mwanamume anayedaiwa kubeba mifuko ya dhahabu bandia kwenye ndege amekuwa mtoa taarifa na anaripotiwa kusaidia polisi wa Zambia kufahamu haya yote. Katika siku chache zilizopita raia kadhaa zaidi wa Zambia wamekamatwa katika kiwanda cha kusindika dhahabu bandia, na kukamatwa zaidi kunaweza kufuata.
Taasisi moja iitwayo Egypt Technocrats, inayoundwa na wataalamu huru wa Misri wanaoishi duniani kote, inadai kuwa kuna zaidi ya kampuni 300 za siri ndani ya Misri zinazohusika na shughuli za utakatishaji fedha.
Wengine wanasema kiasi kikubwa cha pesa kinaweza kuwa kilitoroshwa nje ya nchi tangu Rais Abdel Fattah al-Sisi aingie madarakani miaka tisa iliyopita. Ikiwa ni kweli, je, safari hii ya ndege inaweza kuwa moja tu au kuna mamia ya safari kama hizo?
Nadharia inayoelezwa na baadhi ya watu ni kwamba maafisa wakuu wa kijeshi na wafanyabiashara nchini Misri, wakihofia kwamba utawala wa Rais Sisi unaweza kusambaratika, wamekuwa wakijaribu kuzipeleka fedha zao nje ya nchi.
Hakuna mwenye uhakika lipi ni la kweli na lipi la uongo. Matumaini ni kwamba kesi itakapofanyika hatimaye maswali mengi yatajibiwa. Hata hivyo, hatari ni kwamba inaweza kusababisha maswali Zaidi.