Iran yaweka kamera ili kuwanasa wanawake ambao hawajavaa hijabu

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanawake wa Irani wakipita kwenye mtaa wa masheikn, Tehran, Iran, 19 Septemba 2022

Mamlaka ya Irani imeanza kuweka kamera katika maeneo ya umma ili kuwatambua wanawake ambao hawajavaa hijabu, polisi wametangaza.

Wanawake wanaoonekana kutofunika nywele zao wamepokea "ujumbe wa onyo kama matokeo yake", polisi walisema.

Hii itasaidia kuzuia "upinzani dhidi ya sheria ya hijabu", polisi waliongeza.

Mwaka jana, kulitokea maandamano makubwa yaliochochewa na kifo cha Mahsa Amini akiwa mikononi mwa polisi, msichana mdogo wa Kikurdi aliyekamatwa kwa madai ya kukiuka sheria ya hijabu.

Tangu kifo cha Bi Amin, idadi ya wanawake ambao wamekuwa wakitembea bila kuvaa hijabu zao imeongezeka, haswa katika miji mikubwa, licha ya hatari ya kukamatwa.

Taarifa ya polisi iliyochapishwa na Shirika la Habari la Kiislamu la Republic News linalomilikiwa na serikali ilisema mfumo huo ulitumia kamera zinazoitwa "smart" na zana zingine kutambua na kutuma "nyaraka na jumbe za onyo kwa wanaokiuka sheria ya hijabu".

Wanawake wametakiwa kisheria kufunika nywele zao na hijab (hijabu) tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 yalioweka tafsiri kali ya sheria za kidini. Wanawake wanaokiuka sheria hutozwa faini au kukamatwa

Taarifa ya polisi ya Jumamosi ilieleza hijab kama "moja ya misingi ya ustaarabu wa taifa la Iran" na kuwataka wamiliki wa biashara kuzingatia sheria kupitia "ukaguzi thabiti".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mashambulizi ya hadharani kwa wanawake waliofichuliwa si jambo la kawaida.

Wiki iliyopita, video ya mwanamume akiwarushia mtindi wanawake wawili ambao hawajavaa hijab ilisambazwa sana mtandaoni na baadae wanawake hao kukamatwa chini ya sheria ya hijabu.

Maelfu ya waandamanaji nchini Iran wametiwa mbaroni na wanne wamenyongwa tangu mwezi Disemba, lakini watu wenye msimamo mkali wameendelea kusisitiza kuwa mambo zaidi yafanywe ili kutekeleza sheria.

Jumamosi iliyopita, Rais wa Iran Ebrahim Raisi alirejelea kwamba wanawake wa Iran lazima wavae hijabu kama "sharti la lazima la kidini".

Mkuu wa mahakama ya Iran Gholamhossein Mohseni-Ejei, hata hivyo, alionya siku ya Ijumaa kwamba ukandamizaji ulioenea huenda usiwe njia bora ya kuwahimiza wanawake kufuata sheria.

“Matatizo ya kitamaduni lazima yatatuliwe kwa njia za kitamaduni... Tukitaka kutatua matatizo hayo kwa kukamata na kufungwa, gharama zitaongezeka na hatutaona ufanisi unaotarajiwa,” alisema.