Ashraf Pahlavi: Dada wa mfalme wa Iran, anayetuhumiwa kufanya kazi na mashirika kadhaa ya kijasusi

Chanzo cha picha, Bettman via Getty Images
- Author, Waqar Mfi and Ifraan Yasser
- Akiripoti kutoka, BBC Urdu - BBC International Press
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Jasiri, hodari, na mwenye msimamo, au mwanamke aliyeishi maisha ya kifahari baada ya kuondoka katika nchi yake.
Takriban muongo mmoja baada ya kifo chake, taswira hizi mbili tofauti bado zinamuandama binti mfalme Ashraf Pahlavi, pacha wa Shah wa Iran aliyeondolewa madarakani, Mohammad Reza Pahlavi.
Wengi wanaamini kwamba utu wake ulifaa zaidi kuchukua mamlaka kuliko kaka yake, ambaye alionekana na wengine kama mtu mwenye haya na kusitasita.
Lakini katika maisha yake yote, hasa baada ya kuanguka kwa utawala wa kaka yake, nadharia kuhusu ushawishi wake katika siasa za kisasa za Iran zilimfuatilia bila kukoma, ndani ya Iran na hata alipokuwa uhamishoni huko Ufaransa na Marekani.
Katika kitabu chake cha kumbukumbu, "Faces in a Mirror: Memoirs from Exile", Ashraf aliandika:
"Kujihusisha kwangu na siasa kulizua jarida lilichapisha uvumi usiokoma, ambayo mara kwa mara ilichapisha hadithi zinazohusisha jina langu na kila aina ya masuala — kutoka mambo madogo hadi mauaji ya maafisa wa ngazi za juu."
Magazeti ya Ulaya yalikuwa yananitaja kama 'nguvu nyuma ya ufalme' au 'Chui mweusi wa Iran'."
Operesheni Ajax: Mshiriki muhimu katika mapinduzi
Ushawishi wa Ashraf wakati wa uwaziri mkuu wa Mohammad Mossadegh ulikuwa wazi kiasi kwamba mwaka 1952, kufuatia maandamano dhidi ya serikali, Mossadegh aliamuru Ashraf na mama yake kufukuzwa nchini.
Na hofu yake haikuwa bure.
Wanahistoria wengi wanaamini kuwa Ashraf alikuwa na nafasi muhimu katika Operesheni Ajax ya mwaka 1953 mapinduzi yaliyopangwa na Marekani na Uingereza ya kumuondoa Mossadegh madarakani na kumrejesha kaka yake kama Shah wa Iran.
Katika kumbukumbu zake, Ashraf alitetea uamuzi wake wa kuingilia kati akisema alikuwa akilinda Iran dhidi ya "kuangukia mikononi mwa wakomunisti." Hata hivyo, nia yake halisi bado ni suala la mjadala.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati akiwa uhamishoni Paris, mashirika ya kijasusi ya kigeni yalimkaribia, yakimwona kama mtu mwenye ushawishi, mzalendo wa kweli na kiungo muhimu katika njama ya kumuondoa Mossadegh, hasa kwa lengo la kulinda maslahi ya mafuta na siasa za kieneo.
Wakati huo, kaka yake Shah Mohammad Reza Pahlavi, alikuwa amekataa kushirikiana na Marekani na Uingereza katika mpango huo.
Kwa siri, Ashraf alirudi Iran.
Kulingana na nyaraka za CIA zilizochapishwa baadaye na The New York Times, Ashraf alishirikiana na shirika hilo kufanikisha kuangushwa kwa Mossadegh na kumrejesha kaka yake madarakani kama mfalme.
"Wapanga mapinduzi walihitaji mtu mwenye uaminifu usiotetereka na ambaye hangeweza kushinikizwa," aliandika Ashraf.
"Ndio maana walinichagua mimi kufikisha ujumbe kwa Shah kwa njia salama."
Lakini mwanahistoria Stephen Kinzer, katika kitabu chake All the Shah's Men, anatoa picha tofauti.
Anadai kuwa Ashraf alikuwa akifurahia maisha ya kasino na vilabu vya usiku Paris alipokaribiwa na Assadollah Rashidian, wakala wa Kermit Roosevelt wa CIA.
Kinzer anadai kuwa awali Ashraf alisita, lakini alibadilisha mawazo baada ya kupewa koti la manyoya aina ya mink na pesa taslimu na mawakala wa Uingereza na Marekani wakiongozwa na wakala wa Norman Darbyshire.
"Macho yake yalimetameta," alisema wakala Norman Darbyshire, na ndipo Ashraf alikubali kwenda Tehran.
Hata hivyo, Ashraf anadai katika kumbukumbu zake kuwa alikataa "hundi isiyo na kikomo" waliyompa, na alichukua hatari zote kwa uamuzi wake binafsi.
Anasimulia kwamba alifanya safari hiyo ya siri, akijua kabisa hatari iliyohusika, akisema, "Itakuwaje ikiwa mmoja wa wanaume wa Mossadegh angenitambua kwenye uwanja wa ndege? Je, ningekamatwa? Ningehalalishaje kuingia kwangu Iran kinyume cha sheria?"

Chanzo cha picha, Daniel SIMON/Gamma-Rapho via Getty Images
Alipowasili Tehran, ambayo ilikuwa chini ya sheria ya kijeshi, alikamatwa na maafisa wa serikali ya Mossadegh, ambao walimtaka aondoke mara moja.
Ashraf aliwajibu kwa dharau: "Mwambieni bwana wenu aende kuzimu. Mimi ni Muirani, nitabaki nchini kwangu kadiri nitakavyo."
Na kweli alibaki, na kupitia malkia Thuraya, alifanikiwa kufikisha ujumbe muhimu kwa kaka yake bila kufichua yaliyomo.
Kwa maoni yake, mapinduzi hayo hayakuwa operesheni ya kijeshi ya moja kwa moja ya CIA, bali yalikuwa "operesheni ya kisaikolojia", kwa kutumia vyombo vya habari kuchochea uungwaji mkono wa wananchi dhidi ya Mossadegh.
"Sijawahi kuwa mama mzuri."
Ashraf Pahlavi aliolewa mara tatu, na ndoa zote zilivunjika kwa talaka.
Ndoa ya kwanza ilikuwa mwaka 1937 akiwa na miaka 17 pekee,
Alikuwa na watoto watatu.
Katika mahojiano ya mwaka 1980 na New York Times, alikiri:
"Sikuwahi kuwa mama mzuri kwa sababu maisha yangu hayakuniruhusu kutumia muda na watoto wangu."
Alikuwa akilengwa mara kwa mara na uvumi wa mapenzi na viongozi wa kisiasa, jambo lililomfanya awe mwangalifu hata katika mahusiano ya kweli:
"Kila mwanasiasa niliyefanya naye kazi nilihusishwa naye kimapenzi. Ilifika wakati hata mwanaume aliyenivutia kwa dhati, nilihisi sina uhuru wa kihisia."Aliandika kwa kitabu cha kumbukumbu.

Chanzo cha picha, Photo by Keystone-France/Gamma-Keystone via Getty Images
Mwezi Machi, Gazeti la New York Times lilimtaja kama mwanamke ambaye alipendelea kufanya kazi saa 10 kwa siku huko Manhattan wakati wa miezi ya baridi ya Februari na Machi, akihudhuria mikutano hadi usiku, na kutoroka kwenye hali ya hewa ya joto.
Katika miaka ya 1970, Ashraf aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Aliwakilisha Iran katika UNESCO na taasisi nyingine za kimataifa.
Mwandishi wa habari Kathleen Telch aliripoti kwamba Ashraf Pahlavi alijiona kuwa mtetezi wa wanawake, "lakini sio aina ya kubeba mabango ya uanaharakati"
Aliona hijabu kama alama ya "kurudi nyuma kimaendeleo" na aliunga mkono marufuku ya kuvaa vazi hilo iliyoanzishwa na baba yake, Reza Shah, mwaka 1936.
Uvaaji hijabu
Katika kipande cha maoni kilichochapishwa mwaka 1976, mwishoni mwa mwaka wa kimataifa ulioteuliwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wanawake, Pahlavi alitoa wito kwa wanawake kushinikiza serikali zao kufuta sheria na kanuni zinazozuia maendeleo ya wanawake.
Kabla ya Mapinduzi ya Irani mwaka 1979, alikuwa na jukumu muhimu katika kuzuia uvaaji wa hijabu na kukuza haki za wanawake, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono Sheria ya Ulinzi wa Familia, ambayo ilikuza umri wa kisheria wa ndoa, kuanzisha mahakama maalum za familia, na kuwapa wanawake haki zaidi katika talaka.
Katika kumbukumbu zake, aliiona hijabu kama ishara ya "kuwa nyuma" kwa Irani, na alizingatia marufuku yake mnamo 1936 na baba yake, Reza Shah, hatua ya kihistoria na muhimu kuelekea ukombozi wa wanawake.
Kulingana na mwandishi wa habari wa Washington Post Brian Murphy, Ashraf, dadake mkubwa Shams, na mama yao walikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza wa Iran kuacha kujifunga hijabu ya kitamaduni mapema miaka ya 1930.
Pahlavi anaeleza, kwa huzuni ya wazi, jinsi alivyohisi alipolazimika kuwaona wanawake wakiwa wamevaa mtandio tena wakati na baada ya mapinduzi.
Tuhuma za ufisadi au uwekezaji katika sekta ya ujenzi?
Ashraf alikumbwa na tuhuma nyingi za kifedha, hasa kuhusu uwekezaji wa mali na mashirika ya kifamilia alipokuwa akiishi Iran na pia akifanya kazi katika baadhi ya makampuni ng'ambo.
Alijitetea katika kumbukumbu zake kwa kusema:
"Nilishutumiwa kwa ubadhirifu wa mali, lakini hakuna aliyesema taasisi hizo zilikuwa na bodi huru za wakurugenzi na idara za fedha zilizojitegemea."

Chanzo cha picha, Stills/Gamma-Rapho via Getty Images
Katika kumbukumbu zake, Ashraf Pahlavi pia aliandika: "Wapinzani wangu walinishutumu kuwa mfanyabiashara, jasusi, mwenye uhusiano na mafia (hata mara moja nilielezewa kuwa muuza madawa ya kulevya), na wakala wa mashirika yote ya kijasusi na kukabiliana na kijasusi duniani."
Mnamo 1980, alijitetea katika mahojiano na The New York Times, akisisitiza kwamba utajiri wake haukutoka kwa "vyanzo visivyo halali," bali kutoka kwa ardhi alizorithi ambazo zimeongezeka thamani kutokana na maendeleo ya Iran.
Uhamisho na Kifo
Baada ya Mapinduzi ya Irani ya 1979 na kuanguka kwa utawala wa kaka yake, Pahlavi aliishi New York, Paris, na kwenye Riviera ya Ufaransa.
Licha ya ushawishi wake wa kisiasa na sauti katika masuala ya Irani kupungua, aliendelea kuandika na kuzungumza, akijaribu kushawishi na kuchochea, akielezea kaka yake kama "mtu aliyekata tamaa" aliyesalitiwa na Marekani.
Ingawa sauti yake uhamishoni ilitulia, maisha yake yalikuwa ya kustaajabisha.
The Associated Press ilielezea maisha yake uhamishoni kama "msiba wa mwandishi mahiri Shakespearean."
Mtoto wa kiume wa Ashraf Pahlavi, Shahriar, aliuawa mjini Paris muda mfupi baada ya Mapinduzi ya Iran.
Aliandika katika kumbukumbu zake: "Mwanangu Shahriar aliuawa kikatili na gaidi mwenye uhusiano na Khomeini kwenye mtaa wa Paris. Kama nisingekaribia kupooza kutokana na mshtuko na mvutano ulioongezeka, habari hizi zingeniharibu akili."
Ndugu yake pacha alikufa kwa saratani muda mfupi baadaye mwaka wa 1980.
Kisha akapoteza mpwa wake kutokana na matumizi ya dawa za kulevya huko London mwaka wa 2001, na mpwa wake akajiua huko Boston, Marekani, miaka kumi baadaye.
Ashraf Pahlavi aliaga dunia mjini Monaco Januari 7, 2016, akiwa na umri wa miaka 96, baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kusahau unaofahamika kama Alzheimer.
Maisha yake yalijaa huzuni na kuhama, lakini - kulingana na wengi - alikuwa na athari kubwa ya kihistoria.














