Tunachokijua kuhusu mashambulizi ya Iran kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani, Al Udeid

s
Muda wa kusoma: Dakika 3

Iran imerusha makombora katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Qatar, ikisema kuwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo yake ya nyuklia mwishoni mwa wiki.

Mashuhuda wameripoti kusikia milio mikubwa angani juu ya Qatar, huku video zikionyesha miale mikali angani mifumo ya ulinzi wa anga ikijaribu kuzuia makombora.

Huu ni mlolongo wa ongezeko la mvutano katika mzozo unaohusisha Iran, Israel, na Marekani, ambao umeona hali ya wasiwasi Mashariki ya Kati ikipanda kwa viwango visivyo vya kawaida katika siku za hivi karibuni.

Maelezo ya shambulio hili la hivi punde bado yanaendelea kujitokeza. Haya hapa tunayoyafahamu hadi sasa.

Iran Ilishambulia nini na kwanini?

b
Maelezo ya picha, Kambi ya Al Udeid iko jirani na Iran

Makombora ya Iran yalilenga kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani Mashariki ya Kati, Kambi ya Anga ya Al Udeid.

Takriban raia 8,000 wa Marekani wanaishi huko, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kambi hiyo ni makao makuu ya operesheni zote za anga za jeshi la Marekani katika eneo hilo. Baadhi ya wanajeshi wa Uingereza pia wanahudumu huko kwa zamu.

Serikali ya Qatar imesema hakuna mtu aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo, na kwamba kambi hiyo ilikuwa imeelekezwa watu watoke kabla ya shambulio.

Haijulikani iwapo makombora yoyote yalipiga kambi hiyo, au kama kumekuwa na uharibifu wa mali.

Shambulio hilo lilithibitishwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya serikali ya Iran, na baadaye na jeshi.

Taarifa kutoka IRGC, tawi lenye nguvu zaidi la jeshi la Iran, ilisema kuwa "Iran haitaacha shambulio lolote dhidi ya mamlaka yake bila jibu", na kuongeza: "Kambi za Marekani katika eneo hilo si nguvu bali ni udhaifu."

Marekani ilikuwa imeonya hapo awali Iran isijibu mashambulizi yake kwenye vituo vya nyuklia na iliwahimiza viongozi wa Tehran kukubaliana na mwisho wa kidiplomasia wa uhasama katika eneo hilo.

Ikulu ya White House bado haijajibu shambulio hili la hivi punde.

Marekani na nchi nyingine zilijiandaaje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulikuwa na dalili Jumatatu kwamba Iran ilishukiwa kujiandaa kurusha makombora kuelekea Qatar.

Masaa machache kabla ya shambulio, Qatar ilisema inafunga kwa muda anga yake.

Hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Marekani na Uingereza kuwaambia raia wao nchini humo kutafuta hifadhi hadi ilani nyingine.

Maonyo hayo hayakutoa dalili wazi kwamba shambulio lilikuwa linakaribia: Marekani ilisema ilitoa agizo hilo "kwa tahadhari kubwa", huku Uingereza ikisema ilikuwa inafuata maelekezo ya Wamarekani.

Hata hivyo, takriban saa moja kabla ya shambulio, BBC ilipata habari za "tishio la kuaminika" kwa kambi hiyo.

Kwa nyongeza, baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vilinukuu maafisa wa Marekani wasiojulikana wakisema kwamba mitambo ya kurushia makombora ya Iran ilikuwa imewekwa tayari kwa shambulio kuelekea Qatar.

Tovuti za kufuatilia ndege zilionyesha kuwa ndege tayari zilianza kuelekea viwanja vingine vya ndege kabla ya urushaji wa makombora. Kulingana na Flightradar24, kulikuwa na ndege 100 zilizokuwa zikielekea Doha muda mfupi kabla ya makombora kugunduliwa.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad ni mojawapo ya viwanja 10 vya ndege vilivyo na shughuli nyingi zaidi duniani kwa safari za kimataifa, huku takriban abiria 140,000 wakipita hapo kwa siku.

Tulifikaje hapa?

Usiku wa Jumamosi, Marekani ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya vituo vitatu vya nyuklia ndani ya Iran.

Hiyo ilikuja baada ya siku kadhaa za kutokuwa na uhakika iwapo Marekani itajiunga na operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya Iran, ambazo zilianza Juni 13.

Israel imekuwa ikirusha makombora kila siku dhidi ya vituo vya nyuklia na kijeshi ndani ya Iran, ambavyo serikali yake inasema ni muhimu kuzuia Iran kujenga silaha za nyuklia.

Serikali mfululizo za Israel na Marekani zimekuwa zikijaribu kuzuia Iran kumiliki silaha za nyuklia. Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya kiraia.

Marekani ilidai mashambulizi yake yaliharibu vibaya mpango wa nyuklia wa Iran, ingawa kiwango chake kamili bado hakijulikani.

Mashambulizi kati ya Iran na Israel pia yaliendelea Jumatatu.