Mataifa gani yanapigiwa chapuo kubeba kombe la dunia 2026?

Chanzo cha picha, Getty Images
Droo ya Kombe la Dunia 2026 imeshafanyika, na sasa maandalizi kuelekea michuano hii itakayopigwa mwakani nchini Marekani, Canada na Mexico yameanza rasmi.
Kama kawaida, tunaweza kutarajia vipaji vipya kujitokeza, matokeo ya kushangaza, presha, na burudani ya hali ya juu.
Lakini ni nchi zipi zinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kubeba taji hilo kwa mujibu wa wabashiri, rekodi za hivi karibuni na maoni ya wachambuzi?
Bado timu sita hazijajulikana mpaka hatua ya mchujo wa Machi, lakini tumetazama ni kina nani wanaoonekana kuwa kwenye mbio za kutwaa kombe hilo ambalo fainali yake itapigwa jijini New York mwezi Julai.
Kwa mujibu wa viwango vya ubora vya FIFA, Ujerumani, Hispania na Ubelgiji zinaoekana kupangwa katika makundi 'rahisi' zaidi. Uholanzi na Ufaransa zinnaonekana kuwa katika makundi magumu zaidi.
Timu gani ziko kwenye kiwango bora?
England walifuzu Kombe la Dunia 2026 bila kupoteza hata mechi moja na hawakuruhusu bao lolote.
Wakiwa wamefika fainali za Euro mara mbili mfululizo na robo fainali ya Kombe la Dunia 2022, kuna matumaini makubwa kwamba huu unaweza kuwa mwaka wao chini ya kocha mpya Thomas Tuchel.
Wabashiri pia wanaipa England nafasi kubwa wakiwa wa pili nyuma ya Hispania.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hispania, mabingwa wa Euro 2024, walikuwa karibu kukamilisha kampeni ya kufuzu bila kupoteza, ila sare ya 2-2 na Uturuki ndiyo doa pekee. Wana kipaji kipya hatari, Lamine Yamal wa Barcelona.
Hawajapoteza mechi ya mashindano tangu Machi 2023, isipokuwa kufungwa kwa mikwaju ya penalti kwenye fainali ya Nations League dhidi ya Ureno.
Ufaransa, waliokuwa washindi wa pili 2022, pia wako vizuri na hawakupoteza mechi kwenye kufuzu.
Ujerumani pia wanaonekana kuwa na nafasi nzuri kwa mujibu wa data na wabashiri.
Brazil walikuwa na kampeni mbaya ya kufuzu walimaliza nafasi ya tano na walifungwa mechi 6 kati ya 18. Lakini bado wabashiri wanaweka Brazil nafasi ya nne, ingawa Opta wanaweka nafasi ya saba.
Argentina, mabingwa watetezi, walimaliza kileleni mwa kundi lao kwa mbali, wakiwa pointi 9 mbele ya Ecuador. Na Messi akitarajiwa kucheza, Argentina wanaingia kama miongoni mwa wanaopigiwa chapuo.
Japan walikuwa bora katika kufuzu kwa Asia, wakipoteza mechi moja pekee.
Morocco, waliotia fora kwenye Kombe la Dunia 2022 wakiingia nusu fainali, walishinda mechi zao zote 8 za kufuzu Afrika.
Hata hivyo, mataifa ya Afrika yanaweza kuchoka kwa sababu yatacheza AFCON na Kombe la Dunia ndani ya kipindi kifupi cha miezi sita.
Ureno ya Cristiano Ronaldo haiwezi kupuuzwa, na Italia inahitaji mchujo kufuzu, lakini mara zote ni timu hatari kwenye mashindano.
Droo kamili ya kombe la dunia 2026:
Group A: Mexico, Afrika Kusini, Korea Kusini, mshindi wa mchujo wa UEFA D
Group B: Canada, mshindi wa mchujo Uefa A, Qatar, Uswisi
Group C: Brazil, Morocco, Haiti, Scotland
Group D: USA, Paraguay, Australia, mshindi wa Uefa C
Group E: Ujerumani, Curacao, Ivory Coast, Ecuador
Group F: Netherlands, Japan, mshindi wa Uefa B, Tunisia
Group G: Ubelgiji, Misri, Iran, New Zealand
Group H: Hispania, Cape Verde, Saudi Arabia, Uruguay
Group I: Ufaransa, Senegal, mshindi wa Fifa play-off 2, Norway
Group J: Argentina, Algeria, Austria, Jordan
Group K: Ureno, mshindi wa Fifa play-off 1, Uzbekistan, Colombia
Group L: England, Croatia, Ghana, Panama












