Shambulio la Westgate nchini Kenya: Jinsi manusura alivyopona

tt

Chanzo cha picha, JEWEL KIRIUNGI/BBC

    • Author, Jewel Kiriungi
    • Nafasi, BBC News, Nairobi

Akiwa amelazimika kutembea kwa magongo baada ya kupigwa risasi tano wakati wa shambulio la wanamgambo wa Al shabab kwenye Jumba la maduka la Westgate nchini Kenya muongo mmoja uliopita, Shamim Allu sasa amejiwekea lengo la kufika hadi kambi ya msingi ya Mlima Everest.

"Kufika Everest lengo kubwa sana kwangu, kubwa sana," mama huyo mwenye umri wa miaka 61 aliambia BBC.

"Nitawasilisha ujumbe wangu wa amani na matumaini na ujasiri na msamaha kwa kufika Everest."

Mnamo tarehe 21 Septemba 2013, Bi Allu alinusurika katika moja ya mashambulizi mabaya zaidi ya kigaidi katika historia ya Kenya.

Wanamgambo waliojifunika nyuso zao na waliokuwa na silaha nzito kutoka kwa kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-Qaeda walivamia jengo la maduka la Westgate katika mji mkuu wa Nairobi, na kulishikilia kwa siku nne, katika shambulio lililosababisha vifo vya watu 67 na zaidi ya 200 kujeruhiwa.

Wakati huo, Bi Allu alifanya kazi kama mtangazaji katika kituo cha redio cha FM ambacho kilikuwa kikiandaa shindano la kupikia la watoto kwenye paa la jumba la hilo la maduka. Saa sita mchana, walisikia milio ya risasi.

"Kulikuwa na mvulana mdogo. Alionekana kuwa na hofu kwa sababu sauti ya milipuko ilikuwa ikisikika karibu yetu zaidi na zaidi. Nilimshika mkono na nikasema: 'Kaa nami'," anakumbuka, na kuongeza kwamba alishtukia amegigwa.

"Niliweka mkono wangu nyuma ya mgongo wangu, na niliona ulikuwa umelowa. Na nilipotazama, nilijiona na na shimo kubwa juu ya mkono wangu pia. Na hapo ndipo nikajipata nikiwaza: 'Ee Mungu wangu, nimepigwa risasi."

Bi Alu alikuwa amepigwa risasi moja kwenye kifundo cha mguu, mbili mkononi na mbili zilipitia mgongoni hadi kwenye utumbo wake.

"Bado nakumbuka hali ya joto na harufu yake Ilikuwa kama chuma na ilikuwa harufu ya damu. Hakuna kinachokuandaa kwa tukio la hatari lililo mbele yako. Ilikuwa vurugu tu,” anasema.

tt

Chanzo cha picha, KENYAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/GETTY IMAGE

Maelezo ya picha, Shambuio hilo la siku nne lilisababisha uharibifu mkubwa kwenye jumba hilo la maduka

Watu waliangukiana huku wakisukumana kujaribu kutoroka. Sekunde chache baadaye, guruneti ililipuka na vipande vyake vikasalia kwenye kifundo cha mguu na mgongoni mwa Bi Allu. Mvulana mdogo aliyekuwa amembeba alikufa mikononi mwake muda mfupi baadaye.

Alisikitika sana, kuingiwa na hofu ya hatari inayomkodolea macho.

"Nilielekeza umakini wangu kwenye miti. Kulikuwa na miti nyuma ya Westgate. Na nilifikiri nikitazama miti na kuelekeza mawazo yangu kwenye miti, ningeweza kupata nguvu kutoka kwenye miti hiyo huku kusubiri kupata msaada," Bi Allu anakumbuka.

Aliokolewa takriban saa nne na nusu baadaye na vikosi vya usalama na Shirika la Msalaba Mwekundu, kabla ya kupelekwa hospitalini - mwanzo wa kupona kwa muda mrefu na ngumu kutokana na majeraha na kiwewe.

Bi Alu aliugua sana kwa mapafu yake yalidhurika, na alitumia magongo kutembea kwa miaka miwili. Baadhi ya vipande vya maguruneti bado vimekwama mgongoni mwake.

Bi Allu amehifadhi fulana aliyokuwa amevaa siku ya shambulio hilo, ikiwa na matundu yaliyotokana na risasi na vipande vya guruneti iliyolipuka.

Chanzo cha picha, JEWEL KIRIUNGI/BBC

Maelezo ya picha, Bi Allu amehifadhi fulana aliyokuwa amevaa siku ya shambulio hilo, ikiwa na matundu yaliyotokana na risasi na vipande vya guruneti iliyolipuka.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mnamo mwaka wa 2018, alitiwa moyo na mpanda mlima wa China Xia Boyu, ambaye alikua mtu wa kwanza kukatwa viungo mara mbili kuupanda Mlima Everest kutoka upande wa Nepal.

Aliamua kujipatia changamoto - kimwili na kisaikolojia.

"Kujaribu kuvaa viatu vilivyofungwa ilikuwa changamoto ya kwanza kwa sababu mguu wangu haukuweza kuingia. Nilijifunza jinsi ya kutembeza mguu. Maumivu yalikuwa mengi, lakini sasa nilikuwa na lengo," anasema.

"Nilianza kutembea kilomita nikiwa na malengelenge makubwa na maumivu. Na sasa, nadhani naweza kutembea [kilomita] 11."

Mama huyo mwenye umri wa miaka 61 mara nyingi hupanda Mlima Kenya, mlima wa pili kwa urefu barani Afrika. Inamchukua siku tano hadi saba, kufikia urefu wa takriban mita 3,660 (futi 12,000) juu ya usawa wa bahari.

Ni sehemu ya mazoezi yake ya kukwea mita 5,300 kufika Mlima Everest mnamo Novemba. Hii inatarajiwa kuchukua siku 15 hadi 20.

Bi Allu anachukulia kupanda mlima huo maarufu duniani kama fursa ya kuvutia umma kuhusu umuhimu wa mazingira.

"Ninatumai kuwa naweza kuzungumzia utunzaji wa mazingira kwa sababu miti ndiyo iliyookoa maisha yangu siku hiyo," anaongeza.

Safari ngumu ya Bi Allu kupata nafuu ni jambo ambalo Valentine Kadzo, manusura mwingine wa shambulio hilo, anaweza kuhusika nalo.

Valentine Kadzo

Chanzo cha picha, JEWEL KIRIUNGI/BBC

Maelezo ya picha, Valentine Kadzo bado anaogopa kuenda kwenye maduka makubwa

Mama huyo wa watoto wanne alikuwa akifanya kazi katika soko kwenye ghorofa ya chini ya jumba hilo wakati ufyatuaji risasi ulipoanza.

Katika ghasia zilizofuata, Bi Kadzo alipigwa na risasi kiunoni na watu waliokuwa wamejihami alipokuwa akijificha chini ya meza yake.

"Niliomba.Nilisali sala ya mwisho ambayo ninasikia watu wakisema. Kisha katikati ya sala hiyo, nikasema: "Hapana! sifi leo." Nilimwambia Mungu: "Nikija leo, watoto wangu watateseka."

Bi Kadzo alitolewa hospitali baada ya siku tatu. Licha ya kupokea ushauri nasaha na usaidizi mwingine, baadhi ya majeraha bado hayajapona.

"Nikienda kwenye maduka au sehemu ambayo ninahisi imefungwa, lazima nitafute mahali pa kujificha. Kisha naweza kwenda na kuketi. Inatisha. Sio sawa."

Shambulio hilo pia liliathiri familia za manusura. Wengi walipata kiwewe cha pili kutokana na kuwaona wapendwa wao wakipitia matukio ya karibu kufa.

Familia ya Bi Alu haikuasazwa. Baba na dadake wote waliugua ugonjwa wa mfadhaiko wa baada ya kiwewe (PTSD) kwani walikuwa walezi wake wakuu baada ya shambulio hilo.

"Baba alitoka kuwa binadamu anayefaa sana - alikuwa mkulima, mwenye nguvu, mwenye bidii, hakuna kitu kibaya kwake - hadi kuwa na PTSD. Figo zake zilianza kushindwa. Shinikizo lake la damu lilitoka kwa usawa, na baba alikuwa amekwenda."

Watu wawili pekee ndio wamepatikana na hatia kutokana na unyama huo. Mohammed Ahmed Abdi alipata kifungo cha miaka 33 jela na Hussein Hassan Mustafa miaka 18 kwa kuunga mkono na kusaidia kundi la kigaidi.

Wakati wa kesi yao, serikali ilisema wanamgambo wanne walifanya shambulio hilo, na walipatikana wamekufa kwenye vifusi vya duka hilo.

Ili kukabiliana na kiwewe, Bi Allu alianzisha mpango unaoitwa Miti ya Amani.

Ameshirikiana na mashirika kama vile Rotary Club katika mji aliozaliwa wa Nanyuki kupanda miti kote nchini Kenya. Zaidi ya 5,000 zimepandwa hadi sasa.

Bi Alu anasema imemsaidia kuponya majeraha yake.

"Usikate tamaa na kamwe usiwe mwathirika. Kataa kuwa muathiriwa," Bi Alu mwenye umri wa miaka 61 anawashauri manusura wa mashambulio ya kigaidi na mashambulio mengine.

Maelezo ya video, Shambulizi la Westgate:Ni nini kilitokea Westgate miaka 10 iliyopita?
Pia uanaweza kusoma: