Ngũgĩ wa Thiong'o: Mfahamu nguli wa fasihi Afrika aliyeacha alama isiyofutika

Chanzo cha picha, Ngugi wa Thiong'o
Ngũgĩ wa Thiong'o, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 87, alikuwa kinara wa fasihi ya kisasa ya Afrika - msimuliaji hadithi ambaye alikataa kuzuiwa na jela, uhamisho au ugonjwa.
Kazi yake ilichukua takriban miongo sita, hasa akiandika kuhusu mabadiliko ya nchi yake - Kenya - ikiwa chini ya ukolini hadi ikapata Demokrasia .
Ngũgĩ alipendekezwa kushinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi mara nyingi, lakini akiwaacha mashabiki wake shingo upande kila mshindi wa tuzo hiyo alipotangazwa.
Atakumbukwa sio tu kama mwandishi anayestahili tuzo hiyo ya Nobel, lakini pia kama mtetezi mkali wa fasihi iliyoandikwa kwa lugha asili za Kiafrika.
Lakini Ngugi wa Thiong'o ni nani haswa?
Ngũgĩ alizaliwa na kupatiwa jina la James Thiong'o Ngũgĩ mwaka wa 1938, wakati Kenya ilipokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza. Alilelewa katika mji wa Limuru akiwa katika familia kubwa ya wafanyakazi wa kilimo wa kipato cha chini.
Wazazi wake walihifadhi pesa ili kumlipia masomo yake akiwa katika shule ya upili ya Alliance, shule ya bweni inayoendeshwa na wamishonari wa Uingereza.
Katika mahojiano, Ngũgĩ alikumbuka kurudi nyumbani kutoka Alliance mwishoni mwa muhula na kukuta kijiji chake kizima kilikuwa kimeharibiwa na utawala wa mkoloni.
Wanafamilia wake walikuwa miongoni mwa mamia na maelfu waliolazimika kuishi katika kambi za kizuizini wakati wa msako dhidi ya Mau Mau, vuguvugu la wapigania uhuru.
Maasi ya Mau Mau, ambayo yalidumu kutoka 1952 hadi 1960, yaligusa maisha ya Ngũgĩ kwa njia nyingi na za uharibifu.
Katika mojawapo ya mateso makali zaidi, kakake Ngũgĩ, Gitogo, aliuawa kwa kupigwa risasi mgongoni kwa kukataa kutii amri ya askari wa Uingereza.
Gitogo hakuwa amesikia amri hiyo kwa sababu alikuwa kiziwi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 1959, wakati Waingereza wakijitahidi kudumisha utawala wao nchini Kenya, Ngũgĩ aliondoka kwenda kusoma Uganda. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, ambacho kinasalia kuwa moja ya vyuo vikuu vya hadhi kuu barani Afrika.
Wakati wa mkutano wa waandishi huko Makerere, Ngũgĩ alitoa riwaya yake ya kwanza na mwandishi anayeheshimika wa Nigeria Chinua Achebe.
Achebe alipeleka riwaya hiyo kwa mchapishaji wake nchini Uingereza na kitabu hicho, kwa jina Weep Not, Child, kikatolewa mwaka wa 1964. Ilikuwa ni riwaya ya kwanza kuu ya lugha ya Kiingereza kuandikwa na raia wa Afrika Mashariki.
Ngũgĩ aliandika kwa haraka riwaya nynegine mbili maarufu zaidi, A Grain of Wheat na The River Between. Mnamo 1972, gazeti la Times la Uingereza lilisema Ngũgĩ, wakati huo akiwa na umri wa miaka 33, "alikubaliwa kama mmoja wa waandishi bora wa kisasa wa Afrika".
Mwaka 1977 - ulikuwa kipindi ambacho kiliashiria mabadiliko makubwa katika maisha na kazi ya Ngũgĩ. Kwa kuanzia, huu ndio mwaka ambao alikuja kuwa Ngũgĩ wa Thiong'o na kuliwacha jina lake la kuzaliwa, James. Ngũgĩ alifanya mabadiliko kwa vile alitaka jina lisilo na ushawishi wa kikoloni.
Pia aliacha Kiingereza kama lugha kuu ya fasihi yake na akaapa kuandika tu katika lugha yake ya mama, Kikuyu.
Alichapisha riwaya yake ya mwisho ya lugha ya Kiingereza, Petals of Blood, mwaka 1977.
Vitabu vya awali vya Ngũgĩ vilikuwa vinakosoa serikali ya kikoloni, lakini Petals of Blood aliwashambulia viongozi wapya wa Kenya huru, na kuwaonyesha kama tabaka la wasomi ambao walikuwa wamesaliti Wakenya wa kawaida.
Ngũgĩ hakuishia hapo. Mwaka huohuo, aliandika tamthilia ya Ngaahika Ndeenda (I Will Marry When I Want), iliyokuwa na taswira kali ya mapambano ya kitabaka ya Kenya.
Shughuli zake za kuigiza zilizimwa na serikali ya Rais wa wakati huo Jomo Kenyatta naye Ngũgĩ akafungwa katika jela yenye ulinzi mkali kwa mwaka mmoja bila kufunguliwa mashtaka.
Ilikuwa ni miezi 12 yenye matunda, hata hivyo - kwani Ngũgĩ aliandika riwaya yake ya kwanza ya Kikuyu, Ibilisi Msalabani, akiwa gerezani. Inasemekana alitumia karatasi ya chooni kuandika kitabu kizima, kwani hakuwa na daftari.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ngũgĩ aliachiliwa baada ya Daniel arap Moi kumrithi Bw Kenyatta kama rais.
Ngũgĩ alisema kuwa miaka minne baadaye, akiwa London kwa ajili ya uzinduzi wa kitabu chake, aligundua kuwa kulikuwa na njama ya kumuua akirejea Kenya.
Ngũgĩ alianza uhamisho wa kujitegemea nchini Uingereza na kisha Marekani. Hakurejea Kenya kwa miaka 22.
Hatimaye aliporejea, alikaribishwa kama shujaa - maelfu ya Wakenya walijitokeza kumlaki.
Lakini kurudi nyumbani kuliharibiwa wakati wavamizi walipovamia nyumba ya Ngũgĩ, wakimshambulia mwandishi kikatili na kumbaka mkewe.
Ngũgĩ alisisitiza kuwa shambulio hilo lilikuwa la "kisiasa".
Alirudi Marekani, ambako alikuwa ameshikilia uprofesa katika vyuo vikuu vikiwemo Yale, New York na California Irvine.
Katika taaluma na kwingineko, Ngũgĩ alijulikana kama mmoja wa watetezi wakuu wa fasihi iliyoandikwa kwa lugha za Kiafrika.
Katika maisha yake yote - na hadi leo - fasihi ya Kiafrika ilitawaliwa na vitabu vilivyoandikwa kwa Kiingereza au Kifaransa, lugha rasmi katika nchi nyingi za bara.
"Kuna tofauti gani kati ya mwanasiasa anayesema Afrika haiwezi kufanya bila ubeberu na mwandishi anayesema Afrika haiwezi kufanya bila lugha za Ulaya?" Ngũgĩ aliuliza katika mkusanyiko wa insha motomoto, unaoitwa Decolonising the Mind.
Katika sehemu moja, Ngũgĩ alimwita Chinua Achebe - mwandishi ambaye alisaidia kuanzisha kazi yake - kwa kuandika kwa Kiingereza. Matokeo yake, urafiki wao ukaharibika.
Mbali na kazi yake ya fasihi, Ngũgĩ alioa - na pia akatoa talaka - mara mbili. Alikuwa na watoto tisa, wanne kati yao ni waandishi waliochapisha vitabu.
"Familia yangu imekuwa mmoja wa wapinzani wangu wa fasihi," Ngũgĩ alitania katika mahojiano ya 2020 LA Times.

Mwanawe, Mukoma wa Ngũgĩ, amedai kuwa mamake alidhulumiwa kimwili na Ngũgĩ wa Thiong'o.
"Baadhi ya kumbukumbu zangu za utotoni ni kwenda kumtembelea kwa nyanya yangu ambapo angetafuta hifadhi," mwanawe aliandika katika chapisho la mtandao wa kijamii, ambalo Ngũgĩ wa Thiong'o hakujibu.
Baadaye katika maisha yake, afya ya Ngũgĩ ilidhoofika. Alikuwa na upasuaji wa moyo mara tatu mnamo 2019 na akaanza kuhangaika na tatizo la figo. Mnamo 1995, aligunduliwa na saratani ya kibofu cha mkojo na kupewa miezi mitatu ya kuishi.
Ngũgĩ alipona, hata hivyo, akiongeza saratani kwenye orodha ndefu ya mapambano ambayo alikuwa ameshinda.
Lakini sasa moja ya taa elekezi za fasihi ya Afrika - kama mwandishi wa Nigeria Chimamanda Ngozi Adichie alivyowahi kumuita - ameondoka, akiacha ulimwengu wa maneno kuwa mweusi kidogo.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












