Ukatili mtandaoni: Jinsi wanawake wanavyokabiliwa na hatari kubwa na namna wanavyoweza kujilinda

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukatili wa kidijitali ni mojawapo ya aina za unyanyasaji zinazokua kwa kasi zaidi na unawasukuma wanawake kujiondoa mtandaoni. Kuanzia matusi na ufuatiliaji hadi video bandia (deepfakes) na kufichuliwa kwa taarifa binafsi (doxing), mamilioni ya wanawake na wasichana hukumbana na unyanyasaji kila mwaka.
Kuna takribani watu bilioni sita wanaotumia mtandao duniani, na wanaume milioni 280 zaidi ya wanawake wamekuwa mtandaoni mwaka huu, kwa mujibu wa Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano (International Telecommunication Union), shirika maalumu la Umoja wa Mataifa la teknolojia za kidijitali.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa wanawake, wasichana, na watu wasiozingatia misingi ya kijinsia ya kawaida (gender-non-conforming) wana uwezekano mkubwa zaidi wa kulengwa na hupata madhara makubwa na ya muda mrefu kwa sababu ya jinsi yao.
Tafiti kutoka maeneo mbalimbali duniani zinaonesha kuwa hadi asilimia 58 ya wanawake na wasichana wamewahi kukumbwa na ukatili mtandaoni, kulingana na UN Women.

Chanzo cha picha, Getty Images
Aina tano za ukatili wa kidijitali
1. Uchokozi mtandaoni
Uchokozi mtandaoni (trolling) unahusisha kuchapisha ujumbe wa makusudi wenye kuchokoza au wenye matusi mtandaoni ili kumkera mtu, kumshawishi kutoa majibu ya hasira, au kusababisha vurugu.
Kuna aina kuu mbili za wachokozi mtandaoni, kwa mujibu wa Centre for Countering Digital Hate (CCDH), shirika lisilo la kiserikali la Uingereza na Marekani linalolenga kukomesha ueneaji wa chuki na upotoshaji mtandaoni:
- Wachokozi wanaolenga watu maarufu; wenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii ili kuongeza kasi ya unyanyasaji.
- Wachokozi wanaochochewa na "negative social potency" – yaani wale wanaofurahia madhara yanayowapata wengine.
Kunaweza kuwa na sababu nyingi zinazowafanya watu kuchokoza mtandaoni, na kila mchokozi huwa tofauti na mwingine.
Kwa kawaida wachokozi hupata furaha wanapofanikiwa kuwakera wanaowalenga kwa unyanyasaji, hivyo iwapo mwathiriwa atawajibu, huwahamasisha kuendelea.
Uchokozi mtandaoni unaweza kusababisha viwango vya juu vya wasiwasi na kupungua kwa kujiamini kwa muathiriwa.
2.Kufichua taarifa binafsi mtandaoni

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufichua taarifa binafsi mtandaoni (doxing) kunarejelea kitendo cha kuweka wazi taarifa za siri au binafsi za mtu mtandaoni, mara nyingi kwa nia ovu.
Kitendo hiki kinaweza kusababisha madhara ya moja kwa moja katika maisha halisi kama vile ufuatiliaji (stalking), vitisho, na hata ukatili wa kimwili.
Mnamo mwaka 2021, mwandishi wa Harry Potter JK Rowling alisema kuwa alikuwa mwathiriwa wa tukio hilo, baada ya picha iliyopigwa nje ya nyumba yake, ikionesha anuani yake, kusambazwa mtandaoni.
Hata hivyo, polisi walisema hakuna hatua ambayo ingechukuliwa dhidi ya wanaharakati waliomlenga.
Tangu Aprili 2022, Facebook na Instagram, zinazomilikiwa na Meta, zimekataza kuweka anuani ya nyumbani ya mtu, hata kama inaonekana katika rekodi za umma au taarifa za habari. Watumiaji bado wanaweza kutoa anuani zao wenyewe, lakini wengine hawawezi kuisambaza tena.
Mabadiliko haya yalifanywa kufuatia mapendekezo kutoka Meta Oversight Board ili kuimarisha ulinzi wa faragha na kupunguza hatari za kufichuliwa kwa taarifa binafsi.
3. Video au picha bandia zinazoundwa kwa AI (Deepfakes)

Chanzo cha picha, Getty Images
Deepfakes ni video, picha, au sauti zinazoundwa kwa kutumia akili mnemba ili kuonekana halisi.
Zinaweza kutumika kwa burudani, au hata kwa utafiti wa kisayansi, lakini wakati mwingine hutumika kuiga watu kama wanasiasa au viongozi wa dunia, ili kuwalaghai wananchi makusudi.
Pia zimekuwa zikitumika zaidi kuunda video au picha za kibaguzi za watu wa mapenzi ya jinsi moja au za watu mashuhuri, au hata watu wa kawaida.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na polisi nchini Uingereza umebaini kuwa "mmoja kati ya watu wanne anahisi hakuna tatizo katika hilo, au ana mtazamo wa kawaida kuhusu, kuunda na kuchapisha picha za AI za ngono, hata pale mtu aliyeoneshwa hajaridhia."
Kuchapisha au kutishia kuchapisha picha bila idhini ni kosa la jinai nchini Uingereza, ambalo sasa linashughulikiwa hasa chini ya Sheria ya Usalama Mtandaoni ya 2023 (Online Safety Act 2023). Hii inashughulikia picha zilizotengenezwa au kubadilishwa, ikiwemo deepfakes.
Nchi nyingi nyingine, kama Australia na Ireland, zina sheria zinazofanana kulinda watu dhidi ya unyanyasaji wa picha za namna hiyo.
4. Ushawishi au kumtumia mtoto mtandaoni kwa madhumuni mabaya (grooming)

Chanzo cha picha, Getty Images
Watoto na vijana wanaweza kulengwa na kushambuliwa kisaikolojia mtandaoni (groomed). Watekelezaji wa vitendo hivi wanaweza kutumia majukwaa ya mtandaoni kujenga uhusiano wa kuaminiana na mtoto ili kumnyanyasa.
Unyanyasaji huu unaweza kutokea mtandaoni au mtekelezaji anaweza kupanga kukutana na mtoto ana kwa ana kwa nia ya kumnyanyasa. Unyanyasaji zaidi unaweza kutokea pale maudhui hatarishi yanaporekodiwa, kupakiwa au kuchapishwa na wengine mtandaoni.
Iwapo unyanyasaji unafanyika mtandaoni au nje ya mtandao, unaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa ustawi wa mtoto, na kusababisha wasiwasi, kujiua kwa hiari, matatizo ya lishe, au mawazo ya kujiua.
5. Unyanyasaji mtandaoni
Unyanyasaji mtandaoni (Cyberbullying), hutokea pale mtu anakabiliana na tabia ya manyanyaso kwenye mitandao ya kijamii, programu za ujumbe, michezo ya mtandaoni na sehemu nyingine za mtandao.
Unyanyasaji unaweza kutokea mtandaoni na nje ya mtandao kwa wakati mmoja, na wakati mwingine mtu anayefanya unyanyasaji mtandaoni anajulikana na mwathiriwa.
Pia ni kawaida kukabiliana na unyanyasaji kutoka kwa watu ambao hujawahi kukutana nao binafsi, lakini unajua kutoka kwenye majukwaa ya mtandaoni, michezo au mitandao ya kijamii. Mnyanyasaji pia anaweza kubaki bila kutambulika (anonymous).
Jinsi ya kuwa salama

Chanzo cha picha, Getty Images
Hapa kuna baadhi ya vidokezo vya kupunguza hatari ya kuwa mwathiriwa wa unyanyasaji mtandaoni, kulingana na Umoja wa Mataifa (UN):
- Fikiria mara mbili kabla ya kuchapisha au kushiriki kitu chochote mtandaoni, kinaweza kubaki mtandaoni milele na kutumika kukudhuru baadaye.
- Punguza taarifa unazochapisha mtandaoni, hasa taarifa binafsi kama anuani yako na namba ya simu.
- Wajulishe marafiki na watu unaowajua, wasichapishe taarifa binafsi kuhusu wewe.
- Jifunze kuhusu mipangilio ya faragha kwenye programu zako za mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na nani anaweza kuona taarifa zako na chaguzi za kuzizuia au kuzificha.
- Zima (deactivate) eneo la kijiografia (geo-location) kwenye akaunti zako zote.
- Ripoti akaunti zinazoshukiwa au zinazotishia.
Hatari ya kutisha
Ili kuzuia kwa ufanisi ukatili mtandaoni na unaofanywa kwa kutumia teknolojia, ni muhimu kuelewa asili yake na athari zake kwa wanawake na wasichana, umesema Umoja wa Mataifa (UN).
Utafiti wa UN Women wa mwaka 2021 katika eneo la Nchi za Kiarabu ulipata kuwa asilimia 60 ya wanawake watumiaji wa mtandao walikabiliwa na ukatili mtandaoni mwaka huo.
Utafiti mmoja wa Ulaya ulionesha kuwa wanawake wako katika hatari mara 27 zaidi ya wanaume kukabiliana na unyanyasaji mtandaoni, na uchambuzi mwingine ulionesha kuwa asilimia 92 ya wanawake waliripoti kuwa ukatili mtandaoni unaathiri vibaya ustawi wao.
Wanawake walio kwenye maisha ya umma, kama wanasiasa, waandishi wa habari, na watetezi wa haki za binadamu, wanakuwa lengo maalumu, na hatari ni kubwa zaidi kwa wanawake weusi, watu wa LGBTQI+, na wanawake wenye ulemavu, kulingana na UN.
Shirika hilo limezindua kampeni ya kumaliza ukatili wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana wote, ambayo itadumu hadi Desemba 10. Kampeni hiyo inatoa wito kwa serikali kulinda taarifa binafsi na kuhalalisha ukatili wa kidijitali, na inahimiza makampuni makubwa ya teknolojia kuondoa maudhui hatarishi.












