Wanasiasa wanatajirika, sisi tunateseka - nilisaidia kuiangusha serikali kwa saa 48

Chanzo cha picha, Tanuja Pandey
- Author, Rama Parajuli, Kamal Pariyar & Kelly Ng
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Waandamanaji wa Gen Z wa Nepal waliiangusha serikali chini ya saa 48 - lakini ushindi huo umekuja kwa gharama kubwa.
"Tunajivunia hilo, lakini pia kuna mchanganyiko wa maumivu, majuto na hasira," anasema Tanuja Pandey, mmoja wa waandalizi wa maandamano.
Huku watu 72 wakiuawa, maandamano ya wiki iliyopita yalikuwa machafuko mabaya zaidi katika nchi hiyo ya Himalaya katika miongo kadhaa.
Majengo ya serikali, makazi ya viongozi wa kisiasa na hoteli za kifahari kama vile Hilton, iliyofunguliwa Julai 2024, yalichomwa, kuharibiwa na kuporwa. Mke wa waziri mkuu wa zamani anapigania maisha yake baada ya nyumba yao kuchomwa moto.
Uharibifu huo hauko kwenye mji mkuu wa Kathmandu pekee - angalau ofisi 300 za serikali za mitaa kote nchini zimeharibiwa.
Hasara za kifedha inaweza kufikia rupia za Nepali trilioni 3 (dola bilioni 21.3; £15.6bn), karibu nusu ya Pato la Taifa, kulingana na mtandao wa habari wa Kathmandu Post. Ofisi zake pia zilishambuliwa na umati wa watu na kuchomwa moto.
Maandamano hayo yaliashiria "kukataliwa moja kwa moja kwa tabaka la sasa la wanasiasa wa Nepal lililoongoza kwa miongo kadhaa - chini ya utawala mbovu na unyonyaji wa rasilimali za serikali," anasema Ashish Pradhan, mshauri katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Migogoro.
Chanzo cha Maandamano

Chanzo cha picha, Instagram / sgtb
Siku mbili kabla ya maandamano hayo ya tarehe 8 Septemba, Bi Pandey, mwanaharakati wa mazingira mwenye umri wa miaka 24, aliweka video inayoonyesha eneo la uchimbaji madini huko Chure na kuandika: “Rasilimali za Nepal zinapaswa kuwa za watu, sio "kampuni binafsi za wanasiasa,” na kutoa wito kwa wenzake "kuandamana dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya utajiri wa taifa letu."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama vuguvugu nyingi za vijana barani Asia, maandamano ya Gen Z ya Nepal hayakuwa na kiongozi. Wengine walitoa wito wa maandamano baada ya serikali ya Nepal kuamua kupiga marufuku mitandao 26 ya kijamii, ikitaja kushindwa kwao kusajiliwa nchini.
Kwa muda wa miezi kadhaa, ghadhabu ilitanda dhidi ya watoto wa wanasiasa wenye nguvu, ambao walishutumiwa kwa kuonyesha utajiri wao usioelezeka kwenye mitandao ya kijamii.
Mojawapo ni picha za Saugat Thapa, mtoto wa Waziri wa mkoa, amesimama karibu na mti wa Krismasi na maboksi ya bidhaa za kifahari. Akijibu, alisema ni "tafsiri isio sawa" kwani babake "alirudisha kila rupia kwa jamii - iliyopatikana kutokana na utumishi wa umma.”
Bi Pandey alikuwa akifuatilia picha hizo, lakini video moja inayoonyesha maisha ya anasa ya familia ya mwanasiasa na video ya kijana wa kawaida wa Kinepali ambaye alilazimika kutafuta kazi katika nchi ya Ghuba ilimvutia.
"Inatia uchungu kutazama, hasa kujua kwamba hata vijana wasomi wanalazimika kuondoka nchini kwa sababu mishahara ya hapa ni chini sana," anasema.
Historia ya Nepal
Nepal ni nchi changa. Imekuwa nchi mwaka 2008, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoongozwa na Wamao vilivyodumu kwa muongo mmoja na kuua zaidi ya watu 17,000.
Lakini maendeleo yaliyoahidiwa bado hayajatimia. Katika miaka 17, Nepal imekuwa na serikali 14, na hakuna kiongozi aliyemaliza muhula kamili wa miaka mitano.
Siasa za nchi hiyo zinafanana na mchezo wa kuwania kiti, huku vyama vya kikomunisti na Bunge la Nepali lenye msimamo mkali huchukua zamu katika kutawala. Viongozi watatu, akiwemo KP Sharma Oli ambaye alijiuzulu kutokana na maandamano ya Gen Z, wamerudi madarakani mara nyingi.
Pato la Taifa la Nepal kwa kila mtu ni chini ya dola 1,500, na kuifanya kuwa nchi ya pili kwa umaskini zaidi Asia Kusini, nyuma ya Afghanistan. Takriban 14% ya watu hufanya kazi ng'ambo, na moja kati ya kaya tatu hupokea pesa kutoka nje.
Maandamano ya Vurugu

Chanzo cha picha, Reuters
Bi Pandey anatoka katika familia ya tabaka la kati mashariki mwa Nepal na babake ni mwalimu mstaafu. Miaka mitatu iliyopita, aligundulika kuwa na uvimbe kwenye ubongo, na bado anapatiwa matibabu. Bili za matibabu zilikaribia kuifilisi familia, hivyo dada yake mkubwa alihamia Australia ili kutafuta kipato.
Kabla ya maandamano, Bi Pandey alifanya kazi na watu wengine kuunda miongozo inayosisitiza kutotumia nguvu na kuwakumbusha waandamanaji kuwa na tahadhari dhidi ya "watekaji nyara."
Asubuhi ya tarehe 8 Septemba, aliwasili Maitighar Mandala, kisiwa kikubwa chenye watu wengi katikati mwa Kathmandu akiwa na marafiki zake kadhaa. Alitarajia maelfu ya watu wangejitokeza – na ni kweli umati uliendelea kuongezeka.
Aakriti Ghimire, muandamanaji mwenye umri wa miaka 26, anasema, awali hali ilikuwa ya amani. "Sote tulikuwa tumeketi, tukiimba nyimbo za zamani za Kinepali.”
"Tukitoa kauli mbiu na tulikuwa tukifurahi. Na baada ya hapo, tulianza kuandamana... polisi walikuwepo kuhakikisha hakuna magari yanayotusumbua."
Bi Pandey na Bi Ghimire walianza kuhisi hatari ilipokaribia saa sita mchana, pale umati wa watu ulipoanza kwenda New Baneshwor, bunge la nchi hiyo. Wote wawili waliona watu wakiwasili kwa pikipiki, na Pandey alisema watu hawa walionekana kuwa wazee kuliko waandamanaji wa Gen Z.
Ghimire anaamini walijipenyezaji. "Sasa ikawa vigumu kutofautisha waandamanaji wa amani – yaani kati ya wale waliokuja kwa ajili ya jambo fulani - na wale walioingia kwa nia ya kuleta vurugu."
Baadhi ya waandamanaji walipojaribu kukiuka uzio wa usalama karibu na bunge, polisi waliwarushia vitoa machozi, maji ya kuwasha na risasi. Kuna ushahidi kwamba risasi za moto zilitumika na wanatuhumiwa kuwapiga risasi watoto wa shule pia. Uchunguzi wa kilichotokea unaendelea.
Machafuko na vurugu vilitawala siku iliyofuata. Waandamanaji walilipiza kisasi kwa kuchoma moto bunge, ofisi ya waziri mkuu na majengo mengine ya serikali. Pandey na Ghimire walibaki ndani na kutazama matukio hayo mtandaoni.
"Ni akina nani hawa?" aliuliza Ghimire. "Video zinaonyesha watu hawa wote wamefunikwa nyuso."
Utulivu fulani ulirejea baada ya jeshi kutumwa kudhibiti hali hiyo - amri ya kutotoka nje iliwekwa kwa siku kadhaa. Katika wiki hiyo aliyekuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu Sushila Karki aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa muda. Na anaungwa mkono na waandamanaji kushika wadhifa huo.

Chanzo cha picha, Reuters
Pandey anatumai "ataongoza nchi vozuri, kufanya uchaguzi kwa wakati uliopangwa na kukabidhi mamlaka kwa watu."
Lakini wasiwasi kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Nepal unaendelea - wakati huu ambapo, familia za waandamanaji waliouawa wanahesabu vifo vya watoto wao.
Lakini Pandey anasema ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa nchi yake, lakini kiwewe cha wiki iliyopita kitabaki kwa maisha yake yote.
Huu ni mwamko wa kisiasa wa kizazi chake. "Hatuko tayari kukaa kimya au kukubali ukosefu wa haki," anasema.















