Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Nigeria: Madai ya udanganyifu ya Peter Obi na Atiku Abubakar
Bola Ahmed Tinubu ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Nigeria uliokuwa na ushindani mkali lakini wengi, vikiwemo vyama vya upinzani, wamedai kuwa kura hiyo ilivurugwa na udanganyifu.
Wametaka uchaguzi huo ufutiliwe mbali, kwa madai ya ukiukaji wa Sheria ya Uchaguzi na uwezekano wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa (Inic) kulaghai matokeo na kumpendelea Bw Tinubu.
Madai hayo yamekanushwa na IEC na chama cha Bw Tinubu, chama tawala cha All Progressives Congress (APC).
Kwa upande wa vyama vya upinzani, hadi sasa havijatoa uthibitisho wowote wa kuunga mkono madai yao.
Lakini chama cha Labour, ambacho mgombea urais wake Peter Obi aliibuka wa tatu, kimesema kitaenda mahakamani kubatilisha ushindi wa Bw Tinubu. Bado haijaonekana ni ushahidi gani utawasilishwa.
Kiini cha mzozo huo ni mfumo mpya wa upigaji kura wa kielektroniki, unaojulikana kama Bvas, ambao ulipaswa kufanya uchakachuaji wa matokeo kuwa mgumu zaidi na upigaji kura kuwa wazi zaidi.
Kutoweza kwa wafanyakazi wa uchaguzi kupakia matokeo kutoka kwenye vituo vya kupigia kura kwa seva ya Inec kulisaidia kuchochea madai ya njama.
Hofu ya wizi wa kura iliibuka asubuhi ya uchaguzi wakati mshawishi maarufu alipodai kwenye mitandao ya kijamii kwamba tovuti ya IReV ya Inec, ambapo matokeo yalikusudiwa kupakiwa, ilikiukwa na wadukuzi. Chapisho hili limetazamwa mara milioni 1.4 kwenye Twitter.
BBC ilichunguza dai hilo na ikagundua kuwa tovuti iliyorejelewa ni tovuti ya kughushi inayojifanya kuwa tovuti ya INEC. IEC yenyewe ilitoa hakikisho kwamba tovuti yake "imelindwa vyema", na haiwezi kuharibiwa.
Baadaye, wakati ucheleweshaji wa kupakia matokeo kwenye seva ukiendelea, vyama vinne vya upinzani, vikiwemo Peoples Democratic Party (PDP) na Labour, viliishutumu IEC kwa kukiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kushindwa kupeleka matokeo kwenye tovuti ya IReV.
Kanuni na miongozo ya Inec ilihitaji matokeo kuchanganuliwa na kupakiwa kwenye seva kutoka kwa kila kituo cha kupigia kura zaidi ya 175,000 baada ya kusainiwa na mawakala wa vyama na maafisa wa uchaguzi.
Huku akilalamika kushindwa kupakia matokeo, mgombea makamu wa rais wa PDP Ifeanyi Okowa, katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa chama cha Labour, Yusuf Datti Baba-Ahmed, alidai kuwa huenda INEC "imeungana [na chama tawala] au mfumo wao ulikuwa chini".
"Kama mfumo ulikuwa chini na walijua kuwa umeshuka, basi walipaswa kuahirisha uchaguzi. Kama mfumo haukuwa chini, na hawakuruhusu upakiaji wa matokeo, ina maana kwamba wameingilia kati.
Inec iliomba radhi kwa kile ilichokiita "hitilafu za kiufundi", na kusema kwamba hitilafu zozote kati ya matokeo kwenye tovuti na zitachunguzwa na kutatuliwa.
Inec pia ililaumu ucheleweshaji kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake, kama vile ukosefu wa ufikiaji wa mtandao katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Wafanyakazi walilazimika kupeleka Mfumo wa Uidhinishaji wa Wapiga Kura wa Biomodal (Bvas), unaotumiwa kuwaidhinisha wapiga kura na kupakia matokeo, kwa vituo vya upatanishi vya INEC kufanya hivyo, ilisema. Pia kulikuwa na ripoti za wapiga kura kuruhusu maafisa wa uchaguzi kutumia simu zao za mkononi kupata mtandao.
Lakini watu wengi walilalamika kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais yalikuwa yakipakiwa polepole kuliko matokeo ya uchaguzi wa wabunge uliofanyika kwa wakati mmoja. Inec haijatoa maelezo kwa hili.
Katika masuala mengine yaliyoibuliwa na upinzani, Dino Melaye wa PDP, ambaye aliongoza kuondoka kwa baadhi ya wawakilishi wa chama cha upinzani kutoka kituo cha kukusanya matokeo, alidai kuwa kulikuwa na upigaji kura kupita kiasi katika jimbo la Ekiti jimbo la kwanza kutangaza matokeo, na ambalo lilimuunga mkono Bw Tinubu. .
Akipuuzilia mbali madai hayo, mwenyekiti wa INEC Mahmood Yakubu alisema jumla ya kura zilizopigwa Ekiti, ngome ya Bw Tinubu kusini-magharibi mwa Nigeria, ilikuwa chini ya jumla ya wapiga kura walioidhinishwa.
Kwa madai kwenye mitandao ya kijamii kwamba matokeo kutoka kwa Ekiti yalichapishwa siku tano kabla ya uchaguzi, mwenyekiti wa INEC alisema kwamba hadithi kama hizo zinaweza kupita tu kwa "habari bandia".
Pia kulikuwa na video kwenye mitandao ya kijamii zikionesha vitisho vya wapiga kura na kuporwa kura, na vurugu katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, hasa katika jimbo kubwa zaidi la Lagos alishinda Bw Obi.
BBC imethibitisha uhalisi wa baadhi ya video hizi na wanahabari wa BBC walifika katika kitengo cha kupigia kura mjini Lagos huku majambazi walipotatiza shughuli ya upigaji kura.
Barry Andrews, mangalizi mkuu wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi huo, aliambia BBC kuwa kulikuwa na mapungufu kadhaa.
"Kwa ujumla tuliweza kuona kwamba kulikuwa na ushahidi wa ununuzi wa kura. Ni mapema mno kwetu kuhitimisha jinsi hali hii ilivyokuwa imeenea," alisema.
Pamoja na ucheleweshaji wa upakiaji wa matokeo, alibainisha "tatizo la wazi kati ya ukweli kwamba kura za uchaguzi wa urais hazikupakiwa, ilhali kura za uchaguzi wa wabunge zilipakiwa".
"Ujumbe wetu uko wazi sana - kwamba tungehimiza malalamiko yoyote yaletwe kupitia njia zinazofaa za kisheria. Lakini uchunguzi wetu kwa hakika unabeba mapungufu makubwa katika mchakato wa uchaguzi," alisema.
Picha kadhaa za kura, zinazosemekana kuonesha ushahidi wa kuchezewa kura, pia zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii.
BBC imeangalia baadhi ya picha na kuzifuatilia hadi kwenye upakiaji kwenye seva ya INEC.
BBC iliona mabadiliko makubwa kwenye baadhi ya matokeo yaliyopakiwa, lakini haiwezi kuthibitisha kama yalibadilishwa kwa nia mbaya.
Pia kulikuwa na matukio ambapo, badala ya kupakia picha ya matokeo ya uchaguzi wa urais kwenye tovuti ya INEC, picha za nyuso za watu zinaonekana kuchapishwa.
BBC ilichunguza kesi mbili zilizoangaziwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika video moja inayoshirikiwa na watu wengi, mtu hupitia lango la INEC ili kukagua matokeo kutoka Ado-Ekiti, mji mkuu wa jimbo la Ekiti.
Picha ya matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka eneo hilo inapaswa kuoneshwa pamoja na saini za mawakala wa vyama. Badala yake, picha ya mwanamke inaoneshwa kwenye skrini.
Haijulikani jinsi makosa kama hayo yalivyokuwa yameenea, na kama yalikuwa matokeo ya ukosefu wa mafunzo au udanganyifu wa makusudi, lakini itaongeza shinikizo kwa Inec.
BBC pia iliona mchanganyiko wa matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka kwa baadhi ya majimbo 36 ya Nigeria. Kwa mfano, matokeo mengi kutoka Sokoto ya kaskazini yalipakiwa ambapo matokeo kutoka kwa vituo vya kupigia kura kutoka Rivers kusini yalipaswa kuwa.
Bw Abubakar alishinda Sokoto huku Bw Tinubu akishinda Rivers, ambayo ilitarajiwa kumuunga mkono Bw Obi.
Upakiaji huu usio sahihi, ambao BBC ilibaini, uliathiri matokeo katika majimbo mengi. Lakini ukaguzi uliofuata unaonesha kuwa vituo vingi vya kupigia kura vilivyoathiriwa sasa vina matokeo sahihi.
Kuna machapisho ya mtandaoni yanayoonesha matokeo yanayodaiwa kuwa kutoka kwenye vituo vya kupigia kura ambapo upigaji kura haukufanyika katika hali halisi, lakini BBC haijaweza kuthibitisha haya.
Ucheleweshaji wa upigaji kura ulizingatiwa kote Nigeria. Watu wengi walisubiri kuanzia asubuhi hadi usiku sana ili kupiga kura, lakini wengine walikata tamaa na kurudi nyumbani. Katika baadhi ya matukio, wafanyakazi wa INEC walishindwa kujitokeza kabisa katika vituo vya kupigia kura. Hii imesababisha madai kuwa wafuasi wa upinzani walinyimwa haki kwa makusudi.
Mtandaoni, wafuasi wa chama tawala wanaashiria hasara aliyopata Bw Tinubu - ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu wa Abuja na Lagos kama ushahidi kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Bw Tinubu mwenyewe alikiri kulikuwa na dosari katika uchaguzi lakini akasema "walikuwa wachache kwa idadi na hawakuwa na uwezo wa kuathiri matokeo".
Hata hivyo, vijana wengi waliomuunga mkono Bw Obi katika kura hiyo wamepuuzilia mbali jambo hilo na kusema ni uzushi.
Uchaguzi huo ulikuwa wenye ushindani mkali zaidi tangu utawala wa kijeshi ulipomalizika mwaka 1999 na haishangazi kwamba matokeo yameonekana kuwa na mgawanyiko mkubwa