Cyril Ramaphosa: Rais wa Afrika Kusini anafikiria kuhusu hatima yake huku akikabiliwa na kashfa ya ufisadi

Raia wa Afrika Kusini wanasubiri, wengi wao wakiwa na hofu kubwa, kufahamu iwapo Rais Cyril Ramaphosa anakaribia kujiuzulu kutokana na kashfa inayohusisha ng'ombe, kochi na wizi wa mamia kwa maelfu (na pengine mamilioni) ya dola.

Mengi sasa yanategemea mkutano, kuanzia Ijumaa, wa viongozi wa chama tawala nchini humo, African National Congress (ANC).

Wafuasi sugu wa Bw Ramaphosa - na anasalia kuwa kiongozi maarufu - wanafikiria wakati huu kama vita vya kila kitu au chochote kati ya mtu mwenye heshima, anayejaribu sana kusafisha nchi iliyojaa ufisadi, na nguvu za machafuko na ANC ambao wakijaribu kumwondoa ili kusalia na mali zao na kuepuka kwenda gerezani.

Mchambuzi mmoja alifananishakisa hiki na Henry V wa Shakespeare, akimsihi Bw Ramaphosa "kukaza mishipa" na kupambana kusafisha jina lake.

Hakuna shaka kwamba kesi dhidi ya Bw Ramaphosa ilikuwa – angalau mwanzoni - ilichochewa kisiasa.

Mpinzani mashuhuri wa kisiasa, anayehusishwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini aliyefedheheshwa, Jacob Zuma, alifichua kwa kiasi kikubwa madai kwamba mamilioni ya dola - zilizofichwa kwenye kochi - zilitoweka kwenye shamba la Ramaphosa la Phala Phala, na kwamba kulikuwa na njama ya polisi kuficha ukweli.

Rais - mfanyabiashara tajiri na mwanasiasa wa zamani wa mapambano ya ukombozi, aliyewahi kuungwa mkono na Nelson Mandela kumrithi – alitangaza kuwa hana hatia.

Lakini hadithi hiyo haijatoweka, na baada ya muda, huku maelezo mapya na kukanusha kukifichuka, hata baadhi ya wafuasi wake wamekiri kuwa kashfa hiyo imekuwa ikishughulikiwa vibaya na Bw Ramaphosa na wasaidizi wake.

"Kuna maswali ambayo hajaweza kujibu ... kuhusu kiasi hiki kikubwa cha fedha. Angetuambia angeweka haya yote [biashara] katika dhamana au wakfu. Nadhani alikuwa hakuwa muangalifu sana na mzembe ..’alisema Nombonisa Gasa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa.

Basi nini kinachofuata sasa?

Katika ulimwengu wa ANC uliojaa joto kupita kiasi - chama ambacho kimetawala kwa muda mrefu kiasi kwamba uhasama wake wa ndani kwa sasa unahisi kama vita vya wazi - kampeni na ugomvi unazidi kupamba moto.

Chama hicho kinatazamiwa kuchagua kiongozi baadaye mwezi huu - huku Bw Ramaphosa akiwa kipenzi kwa wengi na ni rahisi kushinda. Lakini mahesabu hayo sasa yanabadilika haraka.

Imeripotiwa sana kwamba Bw Ramaphosa tayari ameamua kujiuzulu, lakini anashawishiwa na washirika kufikiria tena, au angalau kupitisha muda ili kuhakikisha kuna mchakato mzuri wa mpito kwa mtu anayeaminika.

Naibu wake wa sasa, na mrithi wa moja kwa moja, Makamu wa Rais David Dabede Mabuza, hatajwi kama mtu sahihi kwa jukumu hilo.

Lakini je, kuna yeyote katika uongozi wa sasa wa ANC - wengi waliojichafua wenyewe, kwa madai ya ufisadi - kupata viwango vya uungwaji mkono wa kitaifa ambao Bw Ramaphosa bado anao?

Na kama sivyo, je, tunatazama kufumuliwa polepole kwa chama kilichowahi kuikomboa Afrika Kusini kutoka kwa ubaguzi wa rangi - na kushindwa katika uchaguzi mwaka wa 2024? 

Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini, Democratic Alliance, hakika kinatumai kufaidika na mzozo uliopo, kikitaka uchaguzi wa mapema. Baadhi ya wachambuzi wanaona kudorora kwa ANC kama jambo lisiloepukika, na kinafaa kwa demokrasia changa ya nchi.

"Waafrika Kusini wengi wana wasiwasi sana kuhusu kitakachotokea baadaye. Kwa sababu hakuna mtu aliye tayari [kuchukua nafasi ya Bw Ramaphosa]. Lakini huu ni mwanzo wa mwisho wa ANC - na hilo ni jambo zuri. ANC imefanya yake. Iliikomboa nchi. Ni wakati wa kitu kipya," mchambuzi wa siasa Thembisa Fakude alisema.

"Nadhani Afrika Kusini imeweza kuanzisha vishawishi vikali vya kidemokrasia, na [kujiuzulu kwa Bw Ramaphosa - ikiwa itatokea, kutakuwa] mfano wa kuigwa kwa Afrika - huyu hapa kiongozi ambaye alijiuzulu kwa hiari."

Huenda hilo lisifanyike - lakini bado kuna uwezekano – wa kundi la Bw Zuma ndani ya chama cha ANC kunufaika na machafuko hayo, kurejea madarakani, na kuzima mpango mzima wa kupambana na ufisadi. Hiyo itakuwa kichocheo cha ANC kusahaulika kisiasa katika chaguzi zijazo.

"Kundi la Zuma linapigania kuungana, zaidi ya kundi la watu wana manung'uniko kwa sababu wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi. Lakini ni mapema mno kusema hawawezi kurejea," alisema Bi Gasa.

Lakini hata mtu aliye na uwezo kidogo kuliko Bw Ramaphosa huenda akatikisa masoko na kuwafukuza wawekezaji wachache wa kigeni ambao bado wako tayari kuipa Afrika Kusini nafasi, wakati ambapo uchumi – unaoathiriwa na kukatwa kwa umeme kila siku - unajitahidi kujikwamua kutoka janga hilo, na ufisadi ambao umekuwa ukikumba serikali tangu enzi ya utawala wa Bw Zuma.

Mwaka jana, mzozo ndani ya ANC ulizua ghasia mjini Durban na kwingineko kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300 na serikali kulazimika kulipa fidia ya mabilioni ya dola.

Kulikuwa na hisia kwamba Afrika Kusini ilikuwa inakabiliwa na hali ngumu hasa ikizingatiwa - kwamba sasa inaelewa jinsi demokrasia yake changa ilikuwa dhaifu.

Huenda ikawa hivyo, lakini kwa kuwa hakuna chama kimoja, kinachoaminika kilicho tayari kunufaika na mapambano ya ANC, wasiwasi hapa ni kwamba Afrika Kusini inaelekea kwenye zama za siasa za muungano zisizotabirika na zisizo imara, zinazotumiwa kirahisi na vyama vidogo vya watu wengi.

Kuhusu Rais Ramaphosa mwenyewe - wengi wanashangaa kama ana ubavu wa kuhimili vita vya muda mrefu, au kama mfanyabiashara bilionea huyo anayesifiwa kwa mtazamo wake wa kujenga taasisi za serikali, lakini anakosolewa kwa ukosefu wa misuli ya kisiasa - anaweza kupendelea kuondoka ANC. vita vyake na kurudi kwenye shamba lake la mifugo.

"Hakuwa na ubavu wa kutosha wakukabiliana vikali kuwaondoa watu wenye sumu zaidi wanaoipinga katiba [katika ANC]. Tulihitaji mtu mwenye mtazamo wa imara," alisema mchambuzi wa kisiasa Eusebius McKaiser.

Mambo saba kuhusu Cyril Ramaphosa:

  • Alizaliwa Soweto, Johannesburg, mwaka 1952
  • Alikamatwa mwaka wa 1974 na 1976 kwa shughuli za kupinga ubaguzi wa rangi na alizindua Muungano wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa Migodini mwaka wa 1982.
  • Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Mapokezi iliyotayarisha kuachiliwa kwa Nelson Mandela kutoka gerezani mwaka 1990
  • Alikua mbunge na mwenyekiti wa bunge la katiba mwaka 1994
  • Aliingia katika biashara kwa muda wote mwaka wa 1997, na kuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri zaidi Afrika Kusini
  • Alikuwa kwenye bodi ya Lonmin wakati wa mauaji ya Marikana 2012
  • Alichaguliwa kuwa kiongozi wa ANC mwaka 2017 na tarehe 15 Februari 2018 akawa rais baada ya kujiuzulu kwa Jacob Zuma.