Kwa nini Ruto na Odinga wanakaa mezani?

Na Ezekiel Kamwaga

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Raila odinga na Rais William Samoei Ruto

BAADA ya hekaheka ya takribani mwezi mmoja, inaonekana kwamba hali ya kisiasa nchini Kenya inaweza kutulia baada ya hatua ya jana ya Kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, kutangaza kusitisha maandamano makubwa yaliokuwa yamepangwa kufanyika leo.

Hatua ya jana itatoa fursa ya kupumua kwa Rais William Ruto na uwezekano wa mazungumzo baina ya vinara wa Azimio na Kenya Kwanza kwenye kutafuta mwafaka wa kisiasa wa taifa hilo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Ingawa maandamano ya Azimio yanahusu zaidi suala la kupanda kwa gharama za maisha na kudai mabadiliko katika sheria za uchaguzi za nchi hiyo, kiini has ani matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa mwaka jana uliompa ushindi Ruto – huku kambi ya Raila ikidai matokeo hayakuwa halali.

Kwa vyovyote vile, kama Raila angeshinda uchaguzi ule, huenda maandamano na vurugu zinazoendelea sasa zisingekuwepo; na kama zingekuwepo zingekuwa zinaongozwa na Ruto na labda kwa sababu nyingine.

Kwenye hotuba yake ya kusitisha maandamano hayo, Raila alisema lengo ni kutoa nafasi kwa mazungumzo baina ya Kenya Kwanza na Azimio na kwamba kama hakutakuwa na makubaliano, maandamano yataanza upya baada ya wiki mbili.

Ilisadifu kwamba Raila ndiye atoe tamko la kusitisha maandamano kwa sababu ni yeye aliyetangaza kuanza kwa maandamano yasiyo na ukomo mwezi uliopita. Hata wiki iliyopita, yeye pia alisema maandamano yaliyopangwa kufanyika leo, Aprili 3,2023, yangekuwa ndiyo “Mama” wa maandamano yote ambayo yameshafanyika tangu mwezi uliopita.

Ingawa Ruto na Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, wote wamekuwa wakisisitiza kwamba hawana nia ya kuwa na ushirikiano wa aina yoyote na Raila na kuwa hakutakuwa na “nusu mkate” na wapinzani kwenye utawala wao, ilikuwa wazi kwamba lilikuwa suala la muda kabla ya Rail ana Ruto kukutana

Mafahali wa siasa za Kenya

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa sababu ya historia yake kisiasa, Kenya limekuwa taifa la kipekee miongoni mwa jirani zake katika nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Kwa sababu ya aina ya sera zilizofuatwa na waasisi za taifa hilo baada ya Uhuru, lipo tabaka teule la wanasiasa na matajiri kwenye uongozi wa taifa hilo.

Ndiyo sababu ilisadifu kwamba katika fujo zilizosababishwa na maandamano ya wiki iliyopita, mali za familia ya Kenyatta - iliyotoa marais wawili wa taifa hilo baada ya Uhuru na ile ya Odinga – iliyotoa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika Kenya huru, zilivamiwa na kufanyiwa uharibifu na watu wasjojulikana.

Kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Ruto alikuwa akijinadi kwamba yeye hatoki katika mojawapo ya familia kubwa za kisiasa za Kenya na kwamba kama watu wanataka mabadiliko ya kweli, uchaguzi ule ulikuwa ni fursa ya kuachana na tabaka lililozoeleka la watawala.

Lakini wengi wanamwona Ruto kama mwanasiasa ambaye anatamani naye kuifanya familia yake iwe na nguvu na ushawishi wa kisiasa kama ilivyo kwa akina Odinga na Kenyatta. Kitendo cha bintiye kutaka kuwa na Ofisi Rasmi ya Mtoto wa Rais kilichukuliwa na wengi kama sehemu ya kutaka kujenga mazingira hayo kwa familia yake.

Raila, Musalia Mudavadi, Ruto, Uhuru Kenyatta, Kalonzo Musyoka na wengine wa chini yao kama akina Moses Wetangula, Eugene Wamalwa, Aden Duale na Joho Hassan wamewahi kufanya kazi kwa pamoja na kama washindani kwenye maisha yao ya kisiasa nchini Kenya.

Ukweli huo unafanya kwamba tofauti na nchi nyingi za Afrika ambapo ni mara chache au hakuna kabisa uwezekano wa wapinzani na watawala kufanya kazi kwa pamoja – Kenya iko katika daraja la kipekee kwenye eneo hilo.

Ukweli huu kwamba Ruto na Uhuru waliwahi kuwa pamoja, Raila na Ruto waliwahi kuwa kitu kimoja na sasa Rail ana Uhuru ni kitu kimoja – ingawa walikuwa mahasimu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 uliozua maafa, ndiyo unaofanya siasa za Kenya kuwa walau zinatabirika.

Kwenye uchambuzi wa siasa za Afrika, mojawapo ya mambo yanayoweza kutuliza nchi kwa haraka ni uwepo wa uhusiano mzuri – au wa kuaminiana baina ya tabaka la watawala. Kama watawala wanaweza kukaa chini na kuzungumza kwa sababu wanajuana na kuaminiana, hilo linaweza kuleta maridhiano kwa urahisi.

Jambo lingine la muhimu ni uwezekano wa mahasimu kufanyiana vurugu. Kama mahasimu wa kisiasa wote wana uwezo wa kufanyiana vurugu na kuumizana, uwezekano wa wanasiasa kukaa chini na kumaliza tofauti zao ni mkubwa zaidi.

Fundisho kutoka vurugu za mwaka 2008

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ghasia zilizosababishwa na maandamano

Katika safu yake ya kila wiki kwenye gazeti la Sunday Nation la la Kenya toleo la Aprili 2, 2023, mmoja wa maswahiba wakubwa kisiasa wa Raila, Profesa Makau Mutua, alionya; “Kama tukio la uharibifu wa mali za familia ya Kenyatta na Odinga litatokea tena, ni wazi kesho itakuwa zamu ya wengine kuumia”.

Kauli hiyo ya Mutua ni matukio ya vurugu zilizotokea nchini Kenya mwaka 2008 kutokana na uchaguzi wa mwaka 2007. Maelfu ya watu walipoteza maisha katika maeneo tofauti nchini humo.

Kama kuna funzo kubwa lililotokea kwa wanasiasa matajiri wa Kenya ni kwamba inapotokea vurugu, kinachoumizwa si maisha ya watu pekee bali na maslahi yao ya kibiashara pia. Na ilionekana pia kwamba Ruto, Uhuru na Raila wote wana idadi ya kutosha ya wafuasi kupitia ngome zao za kisiasa na kikabila.

Kwa sababu hiyo, kufahamiana na kuaminiana kwao kwa sababu ya maslahi ya pamoja kiuchumi na kisiasa -ndicho hasa kilichowafanya Raila na Ruto kukaa mezani kwa niaba ya wenzao.

Kwa vyovyote vile, ni lazima maridhiano ya namna fulani baina yao yatafikiwa.

Na kwa jinsi hiyo, Kenya itaendelea kuwa salama – angalau kwa tabaka la mafahali wa kisiasa wa taifa hilo.