Tunachokijua kuhusu watu watano waliopotea na nyambizi ya kitalii?

Waokoaji wanakimbizana na muda kuitafuta nyambizi ya kitalii iliyopotea siku ya Jumapili karibu na kisiwa cha Newfoundland, Canada katika bahari ya Atlantiki. Nyambizi hiyo ilizama ili kuyafikia mabaki ya meli ya Titanic, iliyo umbali wa mita 3,800 katika sakafu ya bahari.
Kuzamia hadi katika mabaki hayo kwenda na kurudi inachukua jumla la masaa nane. Lakini timu nyambizi ya Titan inayomilikiwa na kampuni ya OceanGate, ilipoteza mawasiliano na meli ya MV Polar Prince, saa moja na dakika 45 baada ya kuzamia baharini, kwa mujibu wa vikosi vya ulinzi wa baharini vya Marekani.
Kikosi cha Marekani na kile cha Canada, wanajaribu kuitafuta nyambizi hiyo ambayo ina akiba ya gesi ya dharura ya masaa 96. OceanGate hutoza dola za kimarekani 250,000 kwa mtu mmoja kwa safari ya siku nane kuondokea Canada kwenda kutalii mabaki ya Titanic.
Hadi sasa utambulisho wa watu watatu walio katika nyambizi hiyo umethibitishwa, na kuna majina ya watu wawili ambayo bado hayaja thibitishwa.
Hamish Harding

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwenda kuyaona mabaki ya Titanic kunahitaji mambo mawili, pesa nyingi na moyo wa kusafiri. Biliona wa Uingereza, Hamish Harding 58 ana yote mawili hayo.
Harding alikuwa katika nyambizi hiyo siku ya Jumapili, kampuni yake ya Action Aviation na mtoto wake wa kambo, Brian Szasz alisema kupitia mtandao wa kijamii katika ujumbe ambao baadaye ulifutwa.
Msafiri wa angani na mtalii, ambaye anaishi Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwanzilishi wa Action Group na mwenyekiti wa Action Aviation, kampuni ya uuzaji na utoaji wa huduma za usafiri wa angani yenye makao yake Dubai.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ni mhitimu wa fani ya Natural Sciences and Chemical Engineering kutoka chuo kikuu cha Cambridge. Harding ana shauku na mambo ya anga tangu akiwa kijana, ndio maana akawa rubani na michezo ya kuruka kutoka angani.
Mwaka 2022 alitajwa miongoni mwa mashujaa wa safari za angani, na mwanachama wa bodi ya kilabu ya wasafiri. Klabu maarufu ya kimataifa ya wavumbuzi na wanasayansi.
Harding ameshasafiri mara kadhaa kwenda bara la Antaktika, ambako alimsindikiza mwana anga wa zamani Buzz Aldrin mwaka 2016. Akiwa na miaka 86 Aldrin alikuwa mtu wa kwanza wa umri wake kufika ncha ya Kusini ya Dunia.
Mwaka Harding akishirikiana na kampuni ya kitalii ya White Dissert walizindua ndege ya kwanza binafsi itayokwenda katika bara hilo. Mapenzi yake kwa safari pia yalimpeleka anga za juu. Juni 2022 alikuwa katika msafara wa misheni ya Blue Origin ya kampuni ya Jeff Bezos.
Harding ana rikodi tatu za Guinness: Mwaka 2019 alisafiri kuzizunguka ncha za dunia kwa kasi kubwa zaidi. Mwaka 2021, pamoja na Mmarekani, Victor Vescovo, alivunja rikodi mbili ya masafa na ya muda, kwa kuzama umbali wa kina cha mita 11,0000 katika shimo la baharini la Mariana katika bahari ya Pacific.
Shahzada na Suleman Dawood

Chanzo cha picha, Seti Institute
Taarifa iliyotolewa Jumanne, familia ya Dawood ilithibitsha Shahzada Dawood na mtoto wake wa kiume, Suleman Dawood walikuwa katika msafara huo wa kwenda kuyaona mabaki ya Titanic.
“Tunashukuru kwa kuguswa kulikooneshwa na wenzetu na marafiki zetu, na tungewaomba kila mmoja kuwaombea warudi salama, wakati tukiipa familia faragha kwa wakati huu.”
Shahzada Dawood 48, anatokea familia ya kitajiri Pakistan. Anaishi Surrey, Kusini mwa London, na mke wake Christine na watoto wao, Alina na Suleiman 19 ambaye alikuwa katika Titan.
Alizaliwa Pakistan na kuhamia UK alikopata shahada ya kwanza ya sheria kutoka chuo kikuu cha Buckingham. Dawood ni mwanachama wa taasisi ya SETI, ya California - inayojishughulisha na kuvumbua, kuelewa na kuelezea asili ya chanzo cha maisha ya ulimwengu.
Ni mwanachama wa Founders Circle, Mfuko wa British na Asia, ambao mwenyekiti wake ni Mfalme wa UK, Charles III.
Wengine ambao hawajathibitishwa

Chanzo cha picha, Ocean gate
Wengine wawili ni Stockton Rush na Paul-Henry Nargeolet. Wa kwanza ana asili ya Marekani, ni rais wa OceanGate, kampuni ya kukodisha na tafiti za kisayansi, na uvumbuzi katika vina virefu vya bahari.
Tangu kuundwa kwake 2009, kampuni hiyo imeweza kutengeneza vifaa vya kufika umbali wa mita 4,000 na 6,000 chini ya bahari.
Rush alianza kazi yake angani, akawa rubani mdogo zaidi duniani akiwa na miaka 19 mwaka 1981. Miaka mitatu baadaye, alijiunga na McDonnell Douglas Corporation kama injinia katika majaribio ya programu ya usafiri wa anga ya F.15. Uzoefu wake wa anga, na shauku ya bahari vilimfanya kuanzisha kampuni ya OceanGate 2019.
Mwaka 2012 alishiriki uanzishaji wa OceanGate Foundation, shirika lisilo la kibiashara linaloshughulika na kukuza maendeleo ya teknolojia za baharini, sayansi, historia na kiakiolojia. 1989 alitengeneza ndege ya majaribio ya Glasair III ambayo inafanya kazi hadi leo.
Kwa mujibu wa ujumbe wa Facebook, uliochapishwa na Harding kabla ya safari hiyo, wasafiri wengine ni Mfaransa, Paul-Henry Nargeolet, mtu anaye heshimika katika taaluma ya tafiti za chini ya maji.
Kamanda wa zamani wa Jeshi la Majini la Ufaransa. Alijiunga na taasisi ya utafiti na uvumbuzi wa baharini (Ifremer), mwaka 1986 na mwaka mmoja baadaye aliongoza safari ya mwanzo ya kuifikia Titanic.
Akiwa kama mkurugenzi wa kampuni za utafiti wa chini ya maji ya Experiential Media Group na RMS Titanic, anatambulika kuwa sauti ya mamlaka kuhusu ajali ya kihistoria ya meli ya 1912.
Nargeolet aliongoza safari kwenda katika mabaki ya Titanic, akizamia mara 35 na kusimamia uchukuliwaji wa masalia 5,000 ikiwemo sehemu ya a tani 20 ya meli hiyo ambayo kwa sasa iko katika maonyesho ya Las Vegas, Marekani.
2010 aliongoza safari iliyotengeneza ramani ya kwanza inayoeleweka ya Titanic, kwa kutumia sona na kuzalisha picha za 3D sehemu ya sehemu ya mbele ya meli, sehemu ya nyuma na mabaki yaliyovunjika yaliyo chini ya bahari.












