'Ngome 12 za siri': Jinsi CIA inavyoisaidia Ukraine kupambana na Putin - NYT

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa zaidi ya miaka 10, Marekani imedumisha ushirikiano wa siri wa kijasusi na Ukraine, ambao sasa ni muhimu kwa nchi zote mbili katika kukabiliana na Urusi, limeandika gazeti la The New York Times la Marekani , baada ya kuhoji vyanzo 200 katika nchi zote mbili na nchi za Ulaya.

Gazeti hilo limeandika kuwa katika kipindi cha miaka minane iliyopita, CIA imejenga vituo 12 vya kijasusi kwenye mpaka wa Urusi, kimojawapo kilitembelewa na ripota wa NYT.

Katika handaki la chini ya ardhi msituni, wanajeshi wa Kikosi cha Marekani wanafuatilia satelaiti za kijasusi za Urusi na kusikiliza mazungumzo kati ya makamanda wa jeshi la Urusi.

Kwenye moja ya skrini, mstari mwekundu ni njia ya ndege isiyo na rubani ambayo ilivunja ulinzi wa anga wa Urusi kutoka kituo katikati mwa Ukraine hadi kulengwa huko Rostov, Urusi, mwandishi wa habari anabainisha.

Ngome hii inafadhiliwa na CIA kwa kiasi fulani. "Kwa asilimia 110," jenerali wa ujasusi Serhiy Dvoretskyi alisema katika mahojiano aliyotoa katika kituo hicho.

Kama gazeti la New York Times linavyoandika, maelezo ya ushirikiano kati ya ujasusi wa Kiukreni na Marekani yameainishwa kwa muongo mmoja.

CIA na mashirika mengine ya kijasusi ya Marekani hutoa taarifa za kijasusi kwa ajili ya kulenga mashambulizi ya makombora, kufuatilia mienendo ya wanajeshi wa Urusi, na kusaidia kudumisha mitandao ya kijasusi.

Kulingana na chapisho hilo, huduma za ujasusi za Ukraine hapo awali zilikabidhi vidhibiti vya redio vinavyohusiana na ajali ya MH17 katika eneo la Donetsk mwaka 2014 kwa huduma maalum za Marekani. Na pia ziliisaidia Marekani katika ufichuzi wa taarifa zinazohusiana na kuingiliwa kwa uchaguzi wa rais nchini humo mwaka 2016.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati huo huo, makala hiyo inasema, CIA ilianza kutoa mafunzo kwa kitengo maalum cha wasomi cha Kiukreni ambacho kilikamata ndege zisizo na rubani za Urusi na vifaa vya mawasiliano ili wahandisi wa CIA waweze kuziunda upya na mifumo ya alama za siri.

CIA pia ilisaidia kutoa mafunzo kwa majasusi wa Ukraine ambao walifanya kazi ndani ya Urusi, kote Ulaya, Cuba na kwingineko.

Maafisa wa CIA walisalia katika eneo la mbali magharibi mwa Ukraine huku utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden ukiwahamisha wafanyakazi wake wiki kadhaa kabla ya mashambulizi makubwa ya Urusi kuanza Februari 2022.

Chapisho hilo linaonyesha kuwa mtandao huu ni muhimu sana kwa sasa, huku Urusi ikiendelea kupigana na Ukraine inazidi "kutegemea hujuma na mashambulio ya makombora ya masafa marefu, ambayo yanahitaji uwepo wa majasusi nyuma ya safu za adui."

Pia, kulingana na waandishi wa habari, mnamo Februari 22, mkurugenzi wa CIA William Burns alikuja Ukraine ili kuwahakikishia viongozi wa Ukraine ushirikiano unaoendelea. Ziara hii ilikuwa ya kumi tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.

"Tangu mwanzoni, adui wa pamoja - Rais wa Urusi Vladimir Putin - aliiunganisha CIA na washirika wake wa Ukraine.

Akiwa na mawazo ya kuchelewesha hatua ya Ukraine kuelekea Magharibi, Putin aliingilia mara kwa mara mfumo wa kisiasa wa Kyiv, akiwachagua kibinafsi viongozi ambao, kwa maoni yake, wanaweza kuiweka Ukraine katika ramani ya Urusi, lakini kila mara ilirudi nyuma, na kuwaleta waandamanaji mitaani," The New York Times linasema.

f

Chanzo cha picha, EPA

Kizazi kipya cha wapelelezi

Kulingana na makala hiyo, ushirikiano wa CIA-GUR ulianza mwishoni mwa mwezi Februari 2014, wakati rais wa zamani Viktor Yanukovych alipokimbilia Urusi.

Wakati huo huo, sheria za Marekani zilipiga marufuku huduma za kijasusi kutoa Ukraine msaada wowote ambao ungekuwa na matokeo mabaya.

CIA ilipaswa kuimarisha huduma maalum za Ukraine bila kuwakasirisha Warusi. Hata hivyo, mistari myekundu ambayo haikupaswa kuvukwa haikufafanuliwa wazi, jambo ambalo lilileta mvutano wa mara kwa mara katika ushirikiano, waandishi wa makala wanaelezea.

NYT inaandika kwamba huko Kyiv, Nalyvaichenko alichagua msaidizi wake wa muda mrefu, Jenerali Kondratyuk, kama mkuu wa ujasusi, na waliunda kitengo kipya cha kijeshi ambacho kiliwekwa nyuma ya safu za adui kufanya operesheni na kukusanya habari ambazo CIA au MI6 hazingeweza kuzitoa.

Kitengo hiki, kinachojulikana kama Kurugenzi ya Tano, kilikuwa na maafisa waliozaliwa baada ya Ukraine kupata uhuru.

"Hawakuwa na uhusiano wowote na Urusi," Jenerali Kondratiuk alisema. "Hawakujua hata Muungano wa Usovieti ni nini."

Ujasusi wa Ukraine ulishirikiana kwa bidii na CIA na polepole ikawa muhimu kwa Wamarekani, inasema makala.

Mnamo mwaka wa 2015, Jenerali Kondratyuk alifika kwenye mkutano na naibu mkuu wa CIA na kumkabidhi faili nyingi za siri bila tahadhari.

Kifurushi hiki cha kwanza kilikuwa na siri za Meli ya Kaskazini ya Jeshi la Wanamaji la Urusi, pamoja na maelezo ya kina juu ya miundo mpya ya manowari ya nyuklia ya Urusi. Hivi karibuni, vikundi vya wafanyakazi wa CIA walianza kuondoka mara kwa mara ofisini kwake na begi zima la hati, kifungu hicho kinasema.

"Tulielewa kuwa tunahitaji kuunda hali ya uaminifu," Jenerali Kondratyuk alielezea.

Majira hayo ya kiangazi, ndege ya shirika la ndege la Malaysia kutoka Amsterdam hadi Kuala Lumpur ililipuka angani na kuanguka mashariki mwa Ukraine, na kuua karibu abiria 300 na wafanyakazi.

Ndani ya saa chache baada ya maafa hayo, Kurugenzi ya Tano ilinasa simu na kutoa taarifa nyingine za kijasusi ambazo ziliwalaumu haraka watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi.

CIA ilifurahishwa na kutoa ahadi yake kuu ya kwanza, kutoa vifaa salama vya mawasiliano na mafunzo maalum kwa wanachama wa Kurugenzi ya Tano na vitengo vingine viwili vya wasomi.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mabaki ya Boeing MH17

"Waukraine walitaka samaki, na sisi, kwa sababu za kisiasa, hatukuweza kuwapa samaki huyu," afisa wa zamani wa Marekani alisema, akimaanisha ujasusi ambao ungeweza kuwasaidia kupambana na Warusi. "Lakini tulifurahi kuwafundisha jinsi ya kuvua na kutoa vifaa vya uvuvi."

Waandishi wa habari wameandika kwamba ushirikiano na Ukraine ulifanikiwa sana hivi kwamba USA ilikuwa ikifikiria kuunda vitengo sawa katika huduma nyingine maalum za Ulaya ili kukabiliana na Shirikisho la Urusi.

Mkuu wa idara ya CIA, ambayo inahusika na operesheni dhidi ya Shirikisho la Urusi, hata aliandaa mkutano wa siri Uholanzi. Huko, wawakilishi wa CIA, MI-6 ya Uingereza, GUR ya Ukraine, huduma ya Uholanzi na mashirika mengine yalikubali kuunganisha data zao za kijasusi kwa ajili ya kukabiliana na Urusi zaidi.

Matokeo yake yalikuwa muungano wa siri dhidi ya Urusi, na Waukraine walikuwa washiriki muhimu ndani yake.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Lakini, ikiwa Wana Republican katika Congress wataacha ufadhili wa kijeshi kwa Kyiv, CIA inaweza kulazimika kupunguza matumizi, NYT imeandika.

Baadhi ya maafisa wa ujasusi wa Ukraine sasa wanawauliza wenzao wa Marekani ikiwa CIA itawatelekeza. "Tayari ilitokea Afghanistan, na sasa inaweza kutokea nchini Ukrainia," afisa mmoja wa Ukraine alisema.

Hata hivyo, ziara ya hivi majuzi ya mkurugenzi wa CIA William Burns nchini Ukraine inaonyesha kinyume chake, waandishi wa makala wanaeleza.

Akizungumzia kuhusu ziara ya Burns mjini Kyiv wiki iliyopita, afisa wa CIA alisema: "Tumeonyesha dhamira ya wazi kwa Ukraine kwa miaka mingi, na ziara hii ni ishara nyingine kubwa kwamba ahadi ya Marekani itaendelea."

CIA na GRU wamejenga vituo viwili vya siri zaidi vya kunasa mawasiliano ya Urusi, pamoja na ngome 12 za uendeshaji ambazo Jenerali Kondratyuk anasema bado zinafanya kazi, GRU sasa inakusanya taarifa nyingi za ujasusi kuliko wakati wowote wakati wa vita - wengi wao wanashirikiana pamoja na CIA.

"Habari kama hizo haziwezi kupatikana popote - hapa tu na sasa," alithibitisha Jenerali Dvoretsky.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi