Jinsi jasusi wa KGB alivyojikita ndani ya maisha ya maafisa wa ngazi ya juu wa Ufaransa kwa miongo kadhaa

Na Laura Gozzi
BBC News
Jarida kuu la Ufaransa L'Express limefichua kwamba mhariri wake mashuhuri wa zamani, Philippe Grumbach, alikuwa jasusi wa KGB kwa miaka 35.
Grumbach alikuwa mtu aliyechomekwa vyema katika jamii ya Wafaransa kwa miongo kadhaa.
Marais, waigizaji na watu mashuhuri walikuwa miongoni mwa marafiki wa karibu. Alikuwa mtu mashuhuri katika uandishi wa habari ambaye alitengeneza mwelekeo wa uhariri wa mojawapo ya machapisho yenye ufanisi zaidi nchini Ufaransa. Alipofariki mwaka 2003, Waziri wa Utamaduni Jean-Jacques Aillagon alisema Grumbach amekuwa "mmoja wa watu wa kukumbukwa na kuheshimiwa katika vyombo vya habari vya Ufaransa".
Lakini pia alikuwa "Brok", jasusi wa KGB.
Uthibitisho wa kina wa maisha ya aina mbili ya Grumbach unaweza kupatikana katika kile kinachoitwa kumbukumbu za Mitrokhin - iliyopewa jina la mkuu wa Soviet ambaye alisafirisha maelfu ya kurasa za nyaraka kutoka kwa kumbukumbu za Soviet na kuzikabidhi kwa Uingereza mnamo 1992. Baadaye zilikusanywa na kuwa kitabu na Christopher Andrew na Vasili Mitrokhin mwenyewe.
Miongoni mwa maelfu ya kurasa za hati ni maelezo mafupi yanayoonyesha sifa za watu wa Magharibi ambao walipeleleza kwa niaba ya Muungano wa Sovieti.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miezi kadhaa iliyopita, rafiki wa Etienne Girard, mhariri wa masuala ya kijamii katika L'Express na mwandishi mwenza wa ufichuzi wa Grumbach, alimwarifu kwamba mtu anayemfahamu ambaye alikuwa akitafiti faili za Mitrokhin alikutana na kutajwa kwa L'Express. Hati hizo zilisema kwamba wakala aliye na jina la msimbo la Brok alifanya kazi na KGB - na aliandika maelezo ya wasifu yanayolingana na ya Grumbach.
Nia ya Bw Girard ilichochewa mara moja.
"Nilianza kuichunguza na nikapata jina la Grumbach limeandikwa kwa Kirusi, na picha zingine," Bw Girard aliambia BBC. "Na kisha mambo yakawa mabaya zaidi. Niliwasiliana na huduma ya siri ya Ufaransa ili kuthibitisha kwamba Brok alikuwa Grumbach - na mambo yakachacha kutoka hapo."
Grumbach alizaliwa Paris mnamo 1924 katika familia ya Kiyahudi, alitoroka Ufaransa na mama yake na ndugu zake mnamo 1940 - mwaka ambao Ujerumani ya Nazi ilivamia na Marshal Philippe Pétain alichukua mamlaka huko Vichy akiwa na serikali ya walioshirikiana naye. Grumbach alijiunga na jeshi la Marekani mara moja na akapigana pamoja na upinzani nchini Algeria mwaka 1943. Baada ya vita, alijiunga na shirika la habari la AFP - lakini alijiuzulu mara baada ya kupinga hatua za serikali ya Ufaransa katika vita vya Indochina.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 1954, Grumbach aliajiriwa kufanya kazi katika L'Express na Jean-Jacques Servan-Schreiber, mwanzilishi wake.
Kuanzia hapo na kuendelea, Grumbach alianza kutangamana na baadhi ya watu mashuhuri wa Ufaransa wa Karne ya 20.
Alisaidia kuboresha sifa ya seneta wa wakati huo - na rais wa baadaye - Francois Mitterand aliposhutumiwa kwa kughushi maujaji mwaka 1960. Alikuwa karibu na Servan-Schreiber mwenye ushawishi , Rais Valéry Giscard d'Estaing na mwanasiasa mashuhuri Pierre Mendes France, miongoni mwa wengine. Waigizaji Alain Delon na Isabelle Adjani walikuwa wageni katika harusi yake ya 1980, ambapo mwandishi Francoise Sagan na Pierre Berge, mwanzilishi mwenza wa Yves Saint Laurent, walikuwa mashahidi .
Na Grumbach alikuwa jasusi muda huo wote.
Huenda wengine wakauona uamuzi wake wa kuupeleleza Muungano wa Sovieti kuwa hadithi ya kimapenzi ya uaminifu-kwa serikali iliyoangamizwa. Lakini Mitrokhin mwenyewe alikisia kwamba ingawa pengine ni itikadi ambayo hapo awali ilimvutia Grumbach kwa KGB, baada ya miaka michache tu sababu zake za kusalia kama jasusi hazihusiani sana na kutaka kuendeleza Ukomunisti huko Uropa lakini ilikuwa ni hamu ya kupata pesa za kutosha kununua gorofa huko Paris.
Motisha za kifedha hakika zilivutia. Kulingana na faili za Mitrokhin, kati ya 1976 na 1978 pekee Grumbach alitunukiwa tuzo inayotoshana na Euro 250,000 (£214,000) kwa thamani ya leo kwa huduma zake kwa KGB. Katika matukio mengine matatu katika miaka ya 1970, alipokea bonasi ya ziada kwa kuwa mmoja wa majasusi 13 wakuu wa Soviet nchini Ufaransa.
Hata hivyo haijulikani ni misheni gani alitekeleza haswa. Faili za Mitrokhin zinaonyesha kuwa wakati wa uchaguzi wa urais wa 1974 KGB ilimpa faili za kubuni ambazo zilikusudiwa kuleta mvutano kati ya wagombea urais wa mrengo wa kulia. Ingawa L'Express inanukuu hati zikisema kwamba Grumbach alikabidhiwa majukumu ya "kusuluhisha maswala nyeti" na "kuwasiliana na wawakilishi na viongozi wa vyama vya siasa na vikundi", kuna mifano mingine michache halisi ya Grumbach kusaidia USSR kikamilifu.
Labda hiyo ndiyo sababu, mwanzoni mwa miaka ya 1980, KGB ilikata uhusiano naye. Kulingana na kitabu cha faili cha Mitrokhin, maajenti wa KGB huko Paris walimwona Grumbach kama mtu "mdanganyifu" na walihisi alizidisha uwezo wake wa kukusanya habari na thamani ya taarifa zake za kijasusi. Aliachiliwa mnamo 1981.
Hatutawahi kujua ikiwa Grumbach alifarijika kwa sababu maisha yake mawili hayakuwepo tena, au jinsi alihisi kuhusu miaka yake ya utumishi kwa KGB.
Iwe kwa sababu ya aibu au hali ya uaminifu iliyodumu, alikataa jaribio pekee lililojulikana mwaka 2000 na mwandishi wa habari, Thierry Wolton, kujua zaidi kuhusu miaka yake kama jasusi. Hapo awali Grumbach alionekana kukiri kwa uwazi maisha yake ya zamani, lakini baadaye aligeuka, akitishia kumshtaki Wolton ikiwa angeendelea na kitabu cha kufichua-yote alichokuwa akipanga.
Wolton aliachana na mradi huo, lakini inaonekana tukio hilo lilizua hamu kwa Grumbach kuzungumzia uzoefu wake.
Mjane wake Nicole hivi majuzi aliiambia L'Express kwamba, punde tu baada ya ziara ya Wolton, marehemu mume wake alimwambia ukweli. “Alinieleza kwamba alikuwa amefanya kazi na KGB kabla hatujafunga ndoa,” aliambia gazeti hilo. Alisema alitaja kuwa "alikasirishwa" na ubaguzi wa rangi alioshuhudia huko Texas alipokuwa katika jeshi la Marekani, na alisema hii ilimfanya kutafuta ushirikiano na USSR badala yake. "Mara akaongeza kwamba alitaka kuacha mara moja, lakini alikuwa ametishiwa," Nicole aliiambia L'Express.
Bw Girard anasema hakuwa na tatizo kubaini ukweli kuhusu aliyekuwa mhariri mkuu wake.
"Kwa hakika nilikuwa na hisia kwamba nilikuwa nikifanya kazi yangu. Ni juu yetu kufanya uchunguzi, kwa sababu unatuhusu - hata kama inamaanisha kufichua ukweli mchungu," alisema.
Kuandika kipande hicho kulichukua miezi mitatu, lakini imelipa. Takriban kila chombo cha habari nchini Ufaransa kimepokea habari hii - labda kwa sababu wengi bado wanamkumbuka Grumbach kama mtu mashuhuri ambaye alitawala mandhari ya vyombo vya habari vya Ufaransa kwa miongo kadhaa.
Baadhi wanaweza kujaribiwa kutafuta nakala zao za zamani za L'Express kutoka miaka ya Grumbach ili kutafuta ujumbe mdogo wa kuiiunga mkono Soviet. Lakini hakuna uwezekano wa kupata chochote. Katika miaka ya 1950, chini ya usimamizi wa kwanza wa Grumbach kama mhariri mkuu, L'Express iliegemea kushoto bila kuunga mkono ukomunisti; katika miaka ya 1970, wakati Grumbach alipokuwa tena usukani, L'Express ilihamia kwenye nafasi ya wastani, huria, na ya katikati.
Kama ripoti katika L'Express inavyoonyesha, kazi ya Grumbach kama jasusi haikuwa kamwe kueneza propaganda.
"Alikuwa mwangalifu kuweka kazi yake kama jasusi tofauti na kazi yake kama mhariri wa gazeti," Bw Girard alisema. "Lakini hii ndiyo sababu haswa ya jinsi KGB ilivyofanya kazi.
"Ilikuwa katika roho ya KGB. Ilikuwa hatua nzuri. Na ilifanya kazi."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












