Ajali tano mbaya ziwa Victoria

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili

Ziwa Victoria ndio ziwa kubwa barani Afrika. Liko katika nchi tatu za Afrika Mashariki, Tanzania, Uganda na Kenya. Kwa raia wanaoishi karibu na ziwa hili, hunufaika kwa shughuli za uvuvi. Vilevile, ziwa Victoria hutumika kwa usafiri.

Katika shughuli hizi za kibinaadamu, zipo nyakati za ajali. Ajali ambazo huondoka na roho za makumi ya watu ama wengine miili yao hupotea ziwani. Nyingi ya hizo zikichangiwa na vyombo kubeba watu na mizigo kupita kiasi.

Wiki kumetokea ajali mbili katika ziwa hilo. Moja ikitokea upande wa Tanzania na nyingine upande wa Uganda. Makala haya yana lengo la kuzidurusu baadhi ya ajali katika ziwa Victoria.

MV Bukoba – 1996, Tanzania

Hii ni ajali ya kihistoria, pengine ni moja ya ajali iliyoua watu wengi zaidi kwa wakati mmoja kuwahi kutokea Tanzania katika miongo ya hivi karibuni. Ilitokea Mei 21, 1996. Serikali ilikiri kwamba ajali hiyo itaendelea kuwa miongoni mwa kumbukumbu mbaya kutokana na kuangamiza maisha ya mamia ya Watanzania wengi kwa wakati mmoja.

Inakadiriwa zaidi ya watu 800 walifariki katika ajali hiyo iliyotokea kilomita chache kutoka bandari ya Mwanza. Meli hiyo iliyoundwa mwaka 1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 ilikuwa tegemeo kubwa la kutoa huduma yndani ya Ziwa Victoria kati ya Bandari za Bukoba na Mwanza. Siku ya ajali inaelezwa kupakia zaidi ya abiria 2,00.

MV Nyerere – 2018, Tanzania

Septemba 2018 jumla ya watu 224 walifariki na watu wengine 41 wakiokolewa katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere. Ajali hii ilileta kumbukumbua ya jali MV Bukoba - iliyotokea katika ziwa hilo hilo.

Mhandisi wa kivuko hicho Alphonce Charahani alikuwa wa mwisho kuokolewa akiwa hai baada ya kukaa majini kwa saa 48.

Rais wa wakati huo hayati John Magufuli alieleza kuwa kivuko hicho cha MV Nyerere kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kwa takwimu za miili iliyopatikana na pamoja na manusura, ni wazi kwamba chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria wengi kuliko uwezo wake.

Boti la starehe, Uganda 2018

Novemba 2018, watu 32 walifariki baada ya boti ya starehe kuzama katika ziwa Victoria kwa sababu ya hali mbaya ya hewa. Polisi ya Uganda ilisema boti hyo ilikuwa na watu takribani 90, ilipozama majira ya saa moja za jioni.

Afisa wa ngazi za juu wa polisi ya Uganda, Zurah Ganyana alieleza kwamba boti hiyo iliyokuwa imebeba vijana kwa safari za kitalii za mwisho wa wiki, ilikuwa chakavu, na imefanyiwa matengenezo mara kadhaa na haikuwa na kibali cha kufanya kazi.

Kenya, Septemba 2021

Septemba 2021, watu saba walifariki dunia baada ya boti lao kupinduka ziwa Victoria. Kamishna wa Polisi wa kaunti ya Homa Bay, nchini Kenya Moses Lilan alieleza miili saba iliyoopolewa ilijumuisha mtoto mmoja.

Polisi ilieleza kwa vyombo vya habari, boti hiyo ilibeba abiria 19, ilipinduka umbali wa nusu kilomita kabla ya kuwasili bandarini. Chanzo cha ajali kinaelezwa ni upakiaji wa watu na mizigo uliozidi uwezo wa chombo.

Uganda 2023

Siku ya Jumatano ya wiki hii, takribani watu 20 wamefariki baada ya boti kupinduka katika maji ya Uganda ndani ya ziwa Victoria. Polisi ya nchi hiyo imeeleza kuwa watu wengine watano hawajuulikani walipo.

Chombo hicho kilikuwa kimebeba mkaa, chakula na samaki wakati inapata ajali saa 11 alfajiri. Kupitia ukurasa wa twitter wa Polisi ya Uganda, taarifa inaeleza kuwa watu tisa wameokolewa.