Waliohama Chadema: Wanakwenda kukifufua Chaumma au kudidimia nacho?

fc

Chanzo cha picha, MITANDAO

Maelezo ya picha, Waliokuwa vigogo wa Chadema wakipokewa tayari kujiunga na Chaumma
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kuna wimbi la wanasiasa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kukihama chama hicho kikuu cha upinzani na kuhamia chama kingine cha upinzani cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Mei 19, 2025, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe aliwapokea baadhi ya vigogo hao; akiwemo Salum Mwalim ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chaumma, Devotha Minja, Makamu Mwenyekiti Bara na Benson Kigaila, Naibu katibu Mkuu Bara.

Taarifa za vyombo vya habari vya ndani nchini Tanzania zinaeleza, mamia ya wafuasi wengine wa Chadema wako njiani kuhamia Chaumma. Bila shaka hizi ni taarifa za neema kwa chama hicho na taarifa mbaya kwa Chadema.

Mwanasiasa wa ngazi ya juu anapohama chama kimoja kwenda kingine, kuna mambo mawili ya kuyatazama. Je, mafanikio yake ya kisiasa yatakibeba chama anachohamia au mafanikio ya chama hicho yatambeba yeye? Twende polepole, utaelewa.

Katika kesi hii ya vigogo hawa wa zamani wa Chadema – ambao wote watatu wamepata kuwa katika nafasi za juu za uongozi katika chama hicho, inaonekana kwa hakika mafanikio yao kisiasa ni makubwa, kuliko mafanikio ya Chaumma.

Chukua mfano huu: Wakati hayati Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alipohamia chama cha ACT Wazalendo Machi 2019, mafanikio ya Maalim katika siasa yalikuwa ni makubwa kuliko mafanikio ya ACT Wazalendo kwa wakati huo.

Ukubwa wa jina lake, ushawishi na uzoefu, vikaleta neema kwa chama hicho na ghafla kikamea. Kutoka kuwa na Mbunge mmoja baada ya uchaguzi wa 2015 hadi kuwa na Wabunge wanne wa kuchaguliwa baada ya uchaguzi wa 2020.

Wafuasi wa chama wakaongezeka na kujikuta ni sasa ni chama kikuu cha upinzani kwa upande wa Zanzibar. Pia ni sehemu ya serikali ya Umoja wa Kitaifa, kimetoa Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud na kina Mawaziri katika Serikali ya Zanzibar.

Pia unaweza kusoma

Wataifufua CHAUMMA?

gv

Chanzo cha picha, MICHUZI

Turudi CHAUMMA; kilianzishwa mwaka 2013 na kiongozi wake wa muda mrefu, Hashim Spunda Rungwe na akagombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na 2020. Rungwe alipata kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na kugombea urais kwa chama hicho katika uchaguzi wa 2010.

Bila shaka si dhambi kusema, Chaumma hakina mafaniko makubwa katika siasa za Tanzania. Hakijawahi kutoa hata Mbunge. Na katika haraka za kugombea urais, hakikuwahi kuwa tishio kwa chama tawala.

Hakuna miujiza kama ya Yesu kwenye siasa, kufufua vilivyokufa kwa siku moja. Kwa hivyo, ikiwa waliohamia Chaumma wana nguvu za kuvutia wafuasi na kukijenga chama hicho hata kwa muda mrefu, bila shaka tunaweza kuiona Chaumma, ikiibuka na kukuwa kama vile ACT Wazalendo. Kwa sasa hakuna haja ya kucheza kamari ya kisiasa, kusema wana nguvu hizo au la! Muda utatoa jawabu.

Aliyeporomoka hainuki?

fg

Chanzo cha picha, MWANANCHI

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika historia ya siasa za upinzani Tanzania, vyama vya upinzani ambavyo vilikuwa na ushawishi, kisha vikapoteza ushawishi wao, havirudi tena kileleni na kuwa vikuu. Kwa lugha nyingine, chama kinachoporomoka hakiinuki tena kuongoza siasa za upinzani.

Unaweza kukitazama chama cha NCCR Mageuzi, ambacho kulikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania – miaka ya mwanzo baada ya kurudi mfumo wa vyama vingi. Kilikuwa chama kikuu cha upinzani katika uchaguzi wa 1995, kikishika nafasi ya pili nyuma ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kilipoporomoka hakikuinuka tena hadi sasa.

Chama kingine ni CUF, ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania, kikishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005 nyuma ya CCM. Kilianza kuporomoka na Chadema kuwa kileleni baada ya uchaguzi wa 2010. Tangu wakati huo CUF, haijafanikiwa kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania bara.

Na hata upande wa Zanzibar ambako kwa miaka mingi ndicho chama kikuu cha upinzani, lakini baada ya mgogoro wa vigogo wawili hayati Maalim Seif na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, na Maalim kujiondoa chamani 2029, CUF imepoteza ushawishi Zanzibar na ACT Wazalendo imeibuka kama mrithi wa siasa za upinzani visiwani humo.

Kwa Chaumma, hakina historia ya kuwa chama kikuu cha upinzani upande wowote wala katika nyakati zozote – yaani, hakijapanda wala kuporomoka, kipo hapo hapo kilipo. Hakijamezwa na kutemwa na wapiga kura kama NCCR Mageuzi na CUF.

Hilo pengine linaweza kuwa ni faida kwao, kwa kuzingatia ukweli kwamba Watanzania hutaka kitu kipya panapohusika siasa za upinzani, hawataki kurudia kile ambacho tayari walishakiacha.

Hata hivyo, ushindani utakuwa mkubwa kwa Chaumma, mbele ya chama tawala CCM, vyama vya upinzani Chadema na ACT ambavyo vyote vina ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania. Kwa muktadha huo, timu mpya na kongwe ya Chaumma ina mlima mrefu kuupanda mbele yao, ikiwa hawataki kudidimia nacho.