Mwinyi vs Masoud: Haiba moja katika mbio za farasi wawili Zanzibar

s

Chanzo cha picha, IkuluZanzibar

    • Author, Na Rehema Mema,
    • Akiripoti kutoka, Zanzibar
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wote ni wasomi, watulivu, na wanapendelea siasa za hoja kuliko makelele. Lakini licha ya kufanana kwa haiba, wanatofautiana kwa itikadi na dira ya kisiasa. Pamoja na utitiri wa wagombea, uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka 2025 unawakutanisha wagombea wakuu wawili: Hussein Ally Mwinyi wa CCM na Othman Masoud Othamn wa ACT-Wazalendo.

Mwinyi anatetea kiti cha urais alichoshinda mwaka 2020 kwa asilimia 76 ya kura, akimshinda mpinzani wake Maalim Seif Sharif wa ACT aliyepata asilimia 19.87.

Kwa Katiba ya Zanzibar, mshindi wa pili huwa Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi ambayo Maalim Seif alishika kwa muda mfupi kabla ya kifo chake mwanzoni mwa mwaka 2021. Baada ya hapo, nafasi hiyo ilichukuliwa na Othman Masoud, ambaye anaendelea kuishikilia hadi sasa.

Hivyo basi, katika uchaguzi wa mwaka huu Zanzibar, Mwinyi na Masoud wanakutana si kama wapinzani wa kawaida pekee, bali pia kama viongozi waliowahi kushirikiana katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Lakini viongozi hawa ni watu wa aina gani, na wanatofautiana vipi?

Hussein Mwinyi na ndoto ya kuendeleza kilichoanzishwa

Mwinyi

Chanzo cha picha, Getty Images

Hussein Mwinyi ni daktari kwa taaluma na mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania, awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi. Amehudumu kama Waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika wizara kadhaa zikiwemo afya, masuala ya muungano na ulinzi.

Kwa haiba, Mwinyi anatambulika kama kiongozi mpole na mtulivu, sifa alizopewa mara nyingi zikihusishwa na malezi yake ya kisiasa ndani ya familia yenye historia ya uongozi. Amejijengea taswira ya kiongozi anayeamini katika utulivu na maelewano, mtindo unaofanana na ule wa baba yake, aliyewahi kuongoza Zanzibar mwaka 1984 na baadaye Tanzania kati ya mwaka 1985 na 1995.

Mwinyi, akiwa na umri wa miaka 59, anaingia kwenye uchaguzi huu wa 2025 akibeba bendera ya CCM kwa mara ya pili mfululizo. Tangu kuingia madarakani, ameelekeza juhudi zake katika maeneo matatu makuu: utalii, uwekezaji na huduma za kijamii. Pia amesifiwa kwa kuendesha Zanzibar yenye hali ya utulivu na mshikamano zaidi kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tofauti na misuguano ya kisiasa iliyoshuhudiwa kabla ya hapo.

Othman Masoud – Mwanasheria wa Mageuzi

Othman Masoud

Chanzo cha picha, ACT-Wazalendo

Kwa upande mwingine, Othman Masoud ni mwanasheria mwenye taaluma ya juu na uzoefu mpana serikalini. Kabla ya kuingia rasmi katika siasa za upinzani, aliwahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa mashtaka (2002–2011) na baadaye mwanasheria mkuu wa Serikali wa Zanzibar.

Hapo awali hakujitokeza sana kwenye medani ya urais kutokana na kivuli kikubwa cha kisiasa cha Maalim Seif, alama kuu ya upinzani Zanzibar kwa zaidi ya robo karne. Lakini baada ya kifo cha Maalim Seif mwaka 2021, ACT-Wazalendo ilimteua Masoud kuziba nafasi yake na kuwa makamu wa kwanza wa rais katika serikali ya umoja wa kitaifa, nafasi ambayo anashikilia hadi sasa.

Haiba ya Masoud inafanana na ya Mwinyi: mtulivu, mpole na anayependelea hoja badala ya siasa za ukali. Hata hivyo, tofauti na Maalim Seif au wanasiasa wengine wenye sauti kali kama Tundu Lissu, kiongozi wa Chadema, Masoud hujenga mvuto.

kupitia hoja za kisheria na mantiki badala ya hotuba za kishindo. Hii inamfanya kuvutia zaidi kwa tabaka la kati na wasomi, lakini bado kuna swali: je, inatosha kushawishi umma mpana wa wapiga kura wa Zanzibar?

Changamoto na itikadi zinazowatenganisha

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya kufanana kwa haiba, Mwinyi na Masoud wanatofautiana kwa misimamo ya kiitikadi na changamoto walizonazo. Mwinyi anasimamia kuendeleza kilichoanzishwa chini ya serikali zilizopita na kujaribu mambo mapya, akisisitiza kuimarisha sera zilizopo, kukuza sekta binafsi na kudumisha mshikamano wa Muungano. Masoud, kwa upande wake, anajipambanua kama sauti ya mageuzi ya kiutawala, uwajibikaji wa kisiasa na kudai nafasi kubwa zaidi kwa Zanzibar ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Changamoto za Mwinyi zipo katika kuthibitisha kuwa muhula wake wa kwanza umeleta matokeo ya kweli kwa wananchi. Upinzani unaweza kumshinikiza kuhusu ahadi ambazo hazijatekelezwa kikamilifu. Kwa upande mwingine, changamoto za Masoud ni kujitambulisha kama mrithi halali wa urithi wa kisiasa wa Maalim Seif bila kubaki katika kivuli chake.

Aidha, nafasi yake Masoud kama sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inamfanya isiwe rahisi kumkosoa Mwinyi moja kwa moja, kwa kuwa naye pia ni sehemu ya utendaji huo wa serikali.

Kwa hali hiyo, Katiba ya Zanzibar inawaweka pamoja, haiba inawaunganisha, lakini misimamo na mitazamo ya kisiasa inawatenganisha. Mwinyi ni taswira ya mwendelezo wa sera na utulivu, huku Masoud akijipambanua kama taswira ya mageuzi na mabadiliko. Uchaguzi wa mwaka huu ni pambano la haiba zinazofanana lakini dira zinazotofautiana. Hatua ya wapiga kura itajibu swali moja kubwa, Je, Zanzibar itaendelea na utulivu wa CCM au itajaribu sura mpya ya uongozi wa juu kabisa wa nchi kupitia ACT?

.
,