Juhudi zinazofanywa kubaini chanzo cha moto wa nyika Marekani

fd

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Christal Hayes
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Jambo moja ambalo watu wa Angeles wanatamani kujua: moto ulianza vipi? Vidole vimeelekezwa kwa uchomaji moto wa makusudi, kampuni ya umeme na watalii wanaofanya utalii wa kutembea nje ya miji mikubwa.

Wachunguzi wanachunguza nadharia hizo zote na nyinginezo. Wanachunguza picha za kamera za CCTV na mashahidi ili kuelewa kilichotokea Los Angeles.

Vilevile wanachunguza makongoro, mawe, chupa, makopo - uchafu wowote ulioachwa ambao unaweza kutoa jawabu juu ya chanzo cha moto huu.

Ni janga la moto mbaya zaidi katika historia ya Los Angeles lililoanza 7 Januari, na hadi sasa limeuwa watu 27 na kuharibu nyumba na biashara zaidi ya 12,000.

"Ni mapema kujua. Kwa sasa kila mtu anataka majibu, tunataka majibu, jamii inataka majibu, lakini itachukua muda," anasema Ginger Colbrun, msemaji wa Idara ya Los Angeles ya Pombe, Tumbaku, Silaha za Moto na Vilipuzi (ATF).

Pia unaweza kusoma

Watalii wa porini?

Watu wa kwanza huko Palisades kuona moto alikuwa Kai Cranmore na marafiki zake, walipokuwa katika matembezi katika bonde la Temescal Canyon, linalotembelewa sana na watalii wa ndani.

Ni kawaida kwa wageni kwenda na pombe na muziki, ili kujistarehesha kwenye bonde hilo lenye mawe na mabonde ya kuvutia.

Katika mfululizo wa video zilizochapishwa mtandaoni, Cranmore na marafiki zake wanaonekana wakiteremka kwenye korongo asubuhi ya tarehe 7 Januari. Video zake za kwanza zinaonyesha wingu dogo la moshi ukifuka kutoka kwenye kilima. Wanasema walinusa harufu ya moto kabla ya kuona moshi huo.

Katika video nyingine, wingu hilo dogo linazidi kuwa jeusi na miali ya moto inaanza kuonekana ikitanda juu ya kilele cha mlima.

Video za watalii hao zinachunguzwa kama sehemu ya uchunguzi rasmi wa chanzo cha Moto wa Palisades. Baadhi ya watu kwenye mtandao hawakuacha kulilaumu kundi hilo la vijana kwa moto huo.

Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani, vijana hao walieleza jinsi walivyoingiwa na woga watu walipoanzisha mashambulizi mtandaoni dhidi yao. Mmoja ya vijana hao alisema amefuta akaunti zake za mitandao ya kijamii. Lakini bado hakuna ushahidi wa kuhusika kwao hadi sasa.

Moto wa Januari 1?

Wachunguzi pia wanazungumza na wazima moto ambao walikwenda kwenye moto uliozuka karibu na eneo hilo. Kuna madai kuwa moto huo mdogo wa tarehe 1 Januari haukuzimwa vizuri na ukawaka tena siku sita baadaye baada ya upepo kuvuma.

Moto wa Palisades unaaminika ulianza tarehe 7 Januari, lakini mlinzi ambaye anafanya kazi karibu na eneo hilo ameiambia BBC kuwa aliona moshi kwa siku kadhaa katika eneo hilo.

Lakini Mkuu wa Zimamoto wa Kaunti ya Los Angeles Anthony Marrone amepuuza uvumi kwamba moto wa Palisades, unaweza kuwa ni moto uliowaka karibu wiki moja nyuma, yaani ule wa Januari 1.

"Siamini. Binafsi, siamini hilo," ameiambia BBC. "Naamini wiki ni ndefu sana kwa moto kuwaka tena kwa moto ambao haukuzuiwa kikamilifu." Alikiri matukio kama haya hutokea lakini ni nadra.

Uliwashwa makusudi?

ef

Ingawa idara ya Marrone haifanyi uchunguzi wa moto wa Palisades, lakini anasema wachunguzi wanachunguza uwezekano wa kuwa moto huo ulianza kutokana na uchomaji wa makusudi.

"Moto ulikuwa unawaka katika maeneo mengi LA, hilo linatufanya tuamini kuwa moto huu unaweza kuwa uliwashwa na mtu kimakusudi," anasema Marrone.

Anaongeza kuwa takriban nusu ya mioto ambayo huwaka mwituni kwa kawaida huwa imewashwa kimakusudi.

Ni umeme?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Moto uliowaka huo Eaton, umeharibu sehemu kubwa ya mji wa Altadena na biashara na umeua takribani watu 17.

Katika eneo hilo mnara mkubwa wa chuma wa umeme, ulirikodiwa ukiwaka moto Januari 7, wachunguzi wanaelekeza nguvu zao kubaini ikiwa ndio ulikuwa chanzo cha moto huo.

Watoa huduma ya umeme wamelaumiwa siku za nyuma kwa moto huko California, ikiwa ni pamoja na moto wa Camp mwaka 2018 ambao iliua watu 85 na kuharibu mji wa Paradise.

Mwaka 2019, kampuni ya umeme ya Pacific Gas and Electric (PG&E) ililipa fidia ya dola za kimarekani bilioni 13.5 kwa waathiriwa wa moto wa Camp.

Wiki moja tangu Moto wa Eaton, tayari kumekuwa na kesi tano zilizowasilishwa dhidi ya Southern California Edison, kampuni ya usambazaji umeme inayoendesha mnara huo.

Kampuni hiyo inasema haijapata ushahidi wowote kuwa vifaa vyake vilihusika na moto huo na inakagua kesi hizo. Uchunguzi wake wa awali katika njia za kusambaza umeme katika korongo hilo unaonyesha, "hakuna hitilafu ya umeme ndani ya saa 12 kabla ya taarifa ya kuanza kwa moto na hadi saa moja baada ya taarifa ya kuanza kwa moto huo."

Marrone ameiambia BBC, wachunguzi wanachunguza uwezekano wa ikiwa mahali hapo ndipo ambapo moto uliwashwa kimakusudi - kumaanisha kuwa moto wa awali huenda uliwashwa mahali pengine lakini ukaenea kwenye mnara huo kwa cheche kuruka.

Idara ya zima moto ya Los Angeles imeonya dhidi ya kuonyesha kidole cha lawama kwa yoyote kwani bado ni mapema na uchunguzi unaendelea.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah