Cartel de los Soles: Lifahamu kundi linaloiumiza kichwa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imeliorodhesha kundi la Cartel de los Soles (Kihispania kwa Cartel of the Suns) - kundi ambalo inadai kuwa linaongozwa na rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na viongozi wakuu katika serikali yake - kama shirika la kigeni la kigaidi.
Kulitaja shirika kuwa ni kundi la kigaidi kunaipa mamlaka ya kutekeleza sheria ya Marekani na mashirika ya kijeshi uwezo mkubwa zaidi wa kulilenga na kulisambaratisha.
Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikizidisha shinikizo kwa Maduro, ikisema serikali yake si halali kufuatia uchaguzi wa mwaka jana, ambao ulipuuzwa na wengi kuwa uliibiwa. Uteuzi huo unaipa njia nyingine ya kuendeleza shinikizo.
Lakini maswali yameibuliwa iwapo Cartel de los Soles kweli ipo huku wizara ya mambo ya nje ya Venezuela "ikikataa kimsingi, kwa uthabiti, na kabisa" jina hilo, ambalo inaelezea kama "uongo mpya na wa kejeli".
Haishangazi, waziri wa mambo ya ndani na haki wa Venezuela, Diosdado Cabello, kwa muda mrefu ameiita "uvumbuzi".
Cabello, ambaye anadaiwa kuwa mmoja wa wanachama wa ngazi za juu wa shirika hilo, amewashutumu maafisa wa Marekani kwa kutumia kama kisingizio cha kuwalenga wale wasiowapenda.
"Kila mtu anapowasumbua, humtaja kama mkuu wa Cartel de los Soles," alisema mnamo Agosti.
Gustavo Petro, rais wa mrengo wa kushoto wa jirani ya Venezuela, Colombia, pia amekanusha kuwepo kwa kundi hilo.
"Ni kisingizio cha kubuni cha serikali za mrengo wa kulia kuziangusha serikali ambazo hazizitii," aliandika kwenye X mnamo Agosti.
Lakini wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasisitiza kwamba Cartel de los Soles ipo na kwamba "imeathiri kwa njia ya mlungula jeshi, kijasusi, bunge na mahakama ya Venezuela".
Wataalamu waliotoa ushauri kwa BBC wanasema ukweli upo mahali fulani katikati.
Jina Cartel de los Soles liliibuka kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Iilibuniwa na vyombo vya habari vya Venezuela kufuatia tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya dhidi ya jenerali anayesimamia operesheni za kukabiliana na mihadarati katika Walinzi wa Kitaifa wa Venezuela na kurejelea nembo yenye umbo la jua inayovaliwa na majenerali ili kuonyesha vyeo vyao.
Mike LaSusa, mtaalam wa uhalifu uliopangwa Amerika ambaye ni naibu mkurugenzi wa maudhui katika Insight Crime, anasema nembo hiyo ilianza kutumika hivi karibuni kwa maafisa wote wa Venezuela waliokuwa na uhusiano na madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya, bila kujali iwapo maafisa hao walikuwa sehemu ya shirika hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Raúl Benítez-Manau, mtaalam wa uhalifu uliopangwa kutoka chuo kikuu cha UNAM cha Mexico, anasema shughuli za kundi hilo zilianza mwishoni mwa miaka ya 1980 na mapema miaka ya 1990 katika kukabiliana na maendeleo katika nchi jirani ya Colombia, mzalishaji mkubwa zaidi wa kokeini duniani.
Wakati huo, kundi la Medellín Cartel lenye nguvu na lenye makao yake makuu katika jiji la Colombia, lilikuwa likivunjwa na mashambulizi makubwa ya kukabiliana na mihadarati nchini humo yalikuwa yakizaa matunda.
Huku njia zilizoanzishwa za magendo zikiwa chini ya shinikizo, Bw Benítez-Manau anahoji, Cartel de los Soles lilianza kutoa njia mbadala za kusafirisha kokeini kutoka Colombia. Kisha liliimarika katika miaka ya mwanzo ya urais wa Hugo Chávez, rais wa mrengo wa kushoto ambaye aliongoza Venezuela kutoka 1999 hadi kifo chake mnamo 2013, anasema.
"Chávez alipenda kutoa changamoto kwa Marekani, na kukata uhusiano wote wa ushirikiano wa kijeshi kati ya jeshi la Venezuela na Marekani," anaeleza.
Bila uangalizi wa Utawala wa Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Marekani (DEA), "baadhi ya maafisa wa jeshi [la Venezuela] walijihisi huru kufanya biashara na wahalifu", Bw Benítez-Manau anasema.
Ushirikiano wa Chávez na waasi wa mrengo wa kushoto wa Farc wa Colombia - ambao walijifadhili kwa kiasi kikubwa kupitia ulanguzi wa kokeini - ulikuwa sababu nyingine katika kudhibiti tena ulanguzi wa dawa za kulevya kupitia Venezuela, anasema.
Wakikabiliwa na shinikizo la kijeshi nyumbani, kundi la wapiganaji wa msituni lilihamisha oparesheni kadhaa hadi Venezuela, baada ya kugundua kwamba rais wa Venezuela "aliwaona kama washirika wa itikadi ya mrengo wa kushoto", Bw Benítez-Manau anaelezea.
Wesley Tabor, wakala wa zamani wa DEA ambaye alifanya kazi nchini Venezuela, anasema Farc haikupata tu "mahali pa usalama nchini Venezuela" lakini pia maafisa wengi wa serikali, "kutoka kwa polisi wa ngazi ya mitaani hadi wale wa kijeshi", hivi karibuni wakawa washirika wao katika biashara ya madawa ya kulevya.
Kwa pamoja, "walianza kuijaza Marekani na mamia ya tani za kokeini", anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Cartel de los Soles, linatofautiana na mitandao mingine ya madawa ya kulevya kwa kuwa halina muundo rasmi, anasema Bw LaSusa.
Sio kundi kwa kila mtu, anasema, bali ni "mfumo wa rushwa uliyoenea".
Anaongeza kuwa limechochewa na mzozo wa kiuchumi ambao umeikumba Venezuela chini ya mrithi wa Rais Chávez ofisini, Nicolás Maduro.
"Utawala wa Maduro hauwezi kuvipa vikosi vya usalama mishahara mizuri na, ili kudumisha uaminifu wao, unaviruhusu kupokea hongo kutoka kwa walanguzi wa dawa za kulevya," Bw LaSusa aeleza.
Maafisa wa vyeo vya kati na chini ambao hudhibiti maeneo muhimu ya kuingia na kutoka Venezuela, kama vile viwanja vya ndege, wanaunda Cartel de los Soles, Bw Benítez-Manau anasema, kwa kuwa wako katika nafasi nzuri ya kuwezesha mtiririko wa dawa za kulevya.
Lakini maafisa wa Marekani wanasisitiza kwamba misimamo ya Cartel de los Soles inafikia ngazi za juu kabisa za serikali ya Maduro, akiwemo rais mwenyewe.
Mnamo mwaka wa 2020, idara ya sheria ya Marekani ilimshtaki Maduro na wengine 14 kwa kula njama na vikundi vilivyojihami vya Colombia kusafirisha kokeini hadi nchini humo.
Miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu waliotajwa ni Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino na mkuu wa zamani wa Mahakama ya Juu ya Venezuela, Maikel Moreno.
Katika shtaka hilo, waendesha mashtaka wa Marekani pia walidai kuwa tangu angalau 1999, Cartel de los Soles liliongozwa na kusimamiwa na Maduro, Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello, mkuu wa zamani wa ujasusi wa kijeshi Hugo Carvajal, na Jenerali wa zamani Clíver Alcalá.
Wanasema habari iliyotolewa na maafisa wa zamani wa ngazi za juu wa kijeshi wa Venezuela - ni kwamba Carvajal na Alcalá - pia wanaunga mkono kundi hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Leamsy Salazar, mkuu wa zamani wa usalama wa marehemu Hugo Chávez, aliwapa maafisa wa Marekani habari kuhusu Cartel de los Soles mapema 2014.
Salazar, ambaye alikuwa ameondoka Venezuela kwa usaidizi wa DEA, alisema Waziri wa Mambo ya Ndani Cabello aliongoza Cartel de los Soles.
Cabello alikanusha madai hayo, akisema ni sehemu ya "njama ya kimataifa".
Lakini shutuma kutoka kwa maafisa wa zamani wa Venezuela ziliendelea kuenea.
Mnamo 2020, Jenerali Alcala alijisalimisha kwa maajenti wa DEA baada ya kutofautiana na serikali ya Maduro, na akakiri hatia ya kutoa msaada kwa Farc na shughuli zao za ulanguzi wa cocaine.
Mapema mwaka huu, jasusi wa zamani wa Venezuela Carvajal - ambaye pia aliikimbia Venezuela baada ya kutofautiana na Maduro - alikiri katika mahakama ya Marekani, pia, kwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi wa mihadarati.
"Kwa miaka mingi, yeye na maafisa wengine katika Cartel de los Soles walitumia kokeini kama silaha, wakisafirisha Cocaine hadi mjini New York na miji mingine ya Marekani," mwendesha mashtaka mkuu alisema kuhusu Carvajal, anayejulikana kama "El Pollo" (The Chicken), wakati wa kesi yake.

Chanzo cha picha, Getty Image
Maduro na Waziri wa Mambo ya Ndani Cabello wamesalia ndani ya Venezuela lakini hivi majuzi Marekani iliongeza zawadi yake kwa habari itakayopelekea kukamatwa kwao hadi $50m (£38m) na $25m mtawalia.
BBC iliwasiliana na serikali ya Venezuela kwa maoni yake kuhusu madai hayo ya Marekani lakini haikupata jibu kabla ya kuchapishwa.
Hata hivyo, serikali ya Maduro kwa muda mrefu imetupilia mbali shutuma za ulanguzi wa dawa za kulevya zilizotolewa dhidi yake kama jaribio la Marekani kuhalalisha kumwondoa Maduro madarakani.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, wizara ya mambo ya nje ya Venezuela ilitaja kuorodheshwa kwa kundi Cartel de los Soles kama shirika la kigaidi "uzushi wa kipuuzi".
Ilisisitiza Cartel de los Soles "halipo" na kwamba hatua hiyo ilikuwa "uwongo wa kuhalalisha uvamizi haramu dhidi ya Venezuela".















