Vita vya Ukraine: Nani anayedhibiti Soledar na kwanini ni muhimu?

Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Urusi haijachukua mji au jiji kuu nchini Ukraine kwa miezi kadhaa, licha ya juhudi kubwa za kupata mafanikio ya kijeshi. Ikiwa vikosi vya Urusi vitauteka mji wa mashariki wa Soledar, matumaini yao ni kwamba mkondo wa vita unaweza kubadilika.

Nani anadhibiti Soledar?

Wakati kiongozi wa mamluki wa Urusi Yevgeniy Prigozhin alipotangaza vikosi vyake vya Wagner vimechukua udhibiti wa eneo lote la Soledar, picha zilizotolewa zilionekana kushawishi. Lakini wapiganaji wa Wagner sio sehemu ya vikosi vya kawaida vya jeshi la Urusi na wizara ya ulinzi huko Moscow inasema vita bado vinaendelea.

Rais wa Ukraine pia anasema mapambano yanaendelea na Kyiv inasisitiza kwamba Warusi hawafanikiwi katika harakati zao za kuuteka mji huo.

Kwa nini Soledar ni muhimu?

Kuanguka kwa Soledar kunaweza kusaidia wanajeshi wa Urusi katika shambulio lao kwenye mji wa kimkakati wa Ukrain wa Bakhmut, takriban kilomita 10 (maili 6) kusini magharibi, kuwapatia nafasi salama ya kushambulia maeneo ya jiji hilo.

ukraine

Soledar pia ina migodi mirefu ya chumvi, ambayo inaweza kutumika kuwahifadhi askari na kuhifadhi vifaa dhidi ya makombora ya Kiukreni.

Katika video iliyochapishwa na akaunti mojawapo ya Telegram ya Urusi, ambayo BBC bado haijaweza kuthibitisha, Bw Prigozhin anaonekana akiwa na wanajeshi wa Wagner kwenye mgodi wa chumvi wa Soledar.

Migodi hiyo ina mtandao mpana wa chini ya ardhi wa vichuguu, ambayo inaweza kuwa ya umuhimu wa kimkakati wakati majeshi ya Urusi yanajaribu kupenya eneo linalodhibitiwa na Ukraine. Hata hivyo, haijabainika ni kiasi gani cha mtandao huu kinachofikiwa na uelekeo wake.

Umuhimu wa Bakhmut

ukraine

Chanzo cha picha, Reuters

Migodi ya Soledar pia ina chumvi yenye thamani, ambayo inaweza kutoa chanzo muhimu cha mapato kwa mtu yeyote anayedhibiti kwa kuweza kuchimba rasilimali hiyo.

Lakini labda moja ya mambo muhimu zaidi katika vita vya Soledar ni la ishara. "Ndo sababu wanaelekeza nguvu zote huko," anasema mwandishi wa BBC James Waterhouse huko Ukraine, "ni kwamba kuna ushindi mkubwa wa propaganda hapa... ushindi muhimu kwa Rais Vladimir Putin kuwasilisha kwa wakosoaji huko Urusi".

Jukumu la mamluki

Kundi la Wagner limezidi kuwa na ushawishi mkubwa katika mzozo wa Ukraine na Bw Prigozhin amekuwa akiliongoza katika uwanja wa vita. Anadai wapiganaji wake ndio pekee wanaopigana huko Soledar, ingawa wizara ya ulinzi ya Urusi inasema vikosi vyake pia vinashiriki.

Vita vya Soledar na Bakhmut ni sehemu tu ya mstari wa mbele na kampeni pana ambayo haiendi vyema kwa Vladimir Putin.

Urusi ilibadilisha tena mkuu wa vikosi vyake vya kawaida nchini Ukraine miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa, katika ishara nyingine ya kutoridhika na maendeleo ya vita. "[Prigozhin] ataendelea kutumia mafanikio yaliyothibitishwa na kubuniwa ya Wagner Group huko Soledar na Bakhmut," inasema Taasisi ya Utafiti wa Vita "kuifanya kama jeshi pekee la Urusi nchini Ukraine linaloweza kupata mafanikio yanayoonekana."