Wanawake watano wanaobadili maisha katika jamii zao na Afrika
Na Dinah Gahamanyi
BBC News Swahili

Chanzo cha picha, Faraja Kota Nyarandu/Twitter
Wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo katika familia na jamii zao kwa ujumla. Katika makala hii tunawaangazia wanawake watano waliojitokeza, kwa kubuni shughuli zilizotambuliwa ambazo zimeweza kubadili maisha kwa namna moja au nyingine katika jamii zao na Afrika kwa ujumla.
Nora Magero

Chanzo cha picha, UNICEF
Norah Magero, mwanamke kutoka Kenya ni mtaalamu wa Uhandisi mitambo na Nishati mbadala kutoka Kenya ambaye anazisaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, katika mazingira ya kukabiliwa na ubaguzi wa jinsia.
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi Bi Magero ambaye ni muasisi wa Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Drop Access, amekuwa akiongoza kampeni ya usawa katika haki za wanawake za kupata elimu, nishati, mahitaji ya kimsingi kulingana na Malengo ya kudumu ya maendeleo ya Umoja wa mataifa.
Bi Magero ameweza kubuni kifaa cha VacciBox - ambacho ni friji inayotumia nishati ya jua ambayo inaweza kusafirishwa kwa baiskeli, pikipiki n ahata kubebwa , iki kurahisisha usambazaji wa chakula, vifaa vya tiba na madawa kwa usalama na kusafirishwa kwenye jamii mbali mbali ambazo zimeathiriwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi nchini Kenya.
Faraja Kotta Nyalandu

Chanzo cha picha, Faraja Kotta Nyalandu/Instagram
Faraja Kotta, ni mmoja wa wanawake wa Kitanzania, anayeaminiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu hususan ni katika utoaji wa elimu ya mtandao kwa vijana wa kike. Mwanamke huyu ambaye anashikilia taji la urembo nchini Tanzania la mwaka 2004, ni muasisi na Mkurugenzi mtendaji wa Shule Direct, kampuni inayobuni maudhui ya kidigitali ya kielimu kwa ajili ya vijana wa Tanzania na kote Afrika kwa njia ya wavuti na simu za mkononi.
Mwaka 2016 alitunukiwa Tuzo ya mwanamke anayeongoza katika teknolojia barani Afrika kutokana na kazi yake ya Shule Direct, na Mwaka huo huo alitunukiwa tuzo la Uongozi nchini Tanzania, kitengo cha mwanamke maarufu wa mwaka.
Christelle Kwizera

Chanzo cha picha, Christelle Kwizera
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Christelle Kwizera, 25, ni kijana wa Kinyarwanda Mhandisi Mitambo na mjasiliamali wa Kijamii. Katika mwaka 2014, Christelle alianzisha kampuni yake inayoitwa Water Access Rwanda, inayotoa huduma ya usafishaji maji yanayotumiwa.
Kampuni ya Bi Kwizera imetoa maji safi kwa zaidi ya Wanyarwanda 100,000 kupitia mtandao wa mashimo ya kuhifadhia maji (boreholes) 95 pamoja na mfumo wa usafishaji maji INUMA.
Water Access Rwanda ndio kampuni pekee ya Rwanda ambayo imewahi kutunukiwa tuzo la ujasiliamali la Afrika. Christelle pia alitambuliwa kama Mwanamke mjasiliamali wa mwaka 2019 mjini Paris na kampuni ya INCO.
“Tunatoa maji salama yaliyochujwa kwa bei nafuu. Hii husaidia upatikanaji wa mud ana fedha ambazo zinaweza kutumiwa kwa ajili ya shughuli nyingine za kuongeza kipato , kuwawezesha watoto kupata muda zaidi wa kuangazia masomo na wanawake kutumia muda zaidi katika shughuli za kiuchumi na kisiasa kiuchumi na hivyo kuwezesha mafanikio kuelekea maendeleo ya kudumumu’’, alisema Bi Kwizera katika mahojiano na jarida la Vital Voices.
''Mama Police''

Chanzo cha picha, UN news
Katika kitengo cha polisi cha kuwalinda watoto nchini Uganda anapatikana Sejenti Milly Labol, al maarufu ‘Mama Police’ kutoka wilaya ya Namayingo , mashariki mwa Uganda.
Ingawa jukumu la kuwalinda watoto na watoto dhidi ya unyanyasaji ni jukumu lake , Mama police amekukuwa akiwahamasisha wadau wengine wa masuala ya watoto kama vile Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na wengine kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwa na uelewa wa vitendo vya kiutamaduni vinavyowanyanyasa wanawake na watoto.
‘‘Mama police’’, amesifika na kutambuliwa na Shirika la watoto la Umoja wa mataifa Unicef kama mmoja wa wanawake walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa watoto katika jamii yake.
Nancy Tembo

Chanzo cha picha, Nancy Tembo/Twitter
Nancy Tembo , ni Waziri wa misitu na Maliasili wa Malawi, ambaye alichaguliwa kama mbunge katika miaka ya 2004 na 2019.
Akiwa katika wadhifa wake wa sasa , amekuwa mtari wa mbele katika kuhakikisha misitu ya Malawi inarejeshwa kwa kuwahamasisha watu kuacha kutumia mkaa – na badala yake kutumia majiko yanayopiga kwa haraka au majiko ya gesi, ili kurejesha misitu .
Katika tukio la hivi karibuni la upandaji wa miti mjini Lilongwe alielezea athari zinazosababishwa na ukataji wa miti : “Sote tunajitaki miti karibu kwa kila kitu tunachokifanya kila siku. Ukweli ni kwamba, tunahitaji miti kuliko miti inavyotuhitaji sisi .”















