Uchaguzi wa Marekani 2024: Je, upigaji kura kwa barua za posta hufanyikaje?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Wamarekani wanaweza kuchagua rais wa nchi hiyo yenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa njia ya posta, licha ya upigaji kura huo kutiliwa shaka na rais wa zamani na mgombea wa sasa Donald Trump hapo mwanzoni.

Zaidi ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi, wapiga kura wa Marekani walianza kupiga kura ya mapema. Septemba 20, kura ya mapema ilianza katika majimbo kadhaa kati ya 47 ambayo hutoa fursa za kupiga kura ya mapema.

Upigaji kura wa mapema unajumuisha upigaji kura wa ana kwa ana au kura za barua za posta. Kila jimbo la Marekani linaweza kuweka kanuni ya namna wakazi wake wanavyopiga kura zao.

Wengine watapiga kura kupitia masanduku ya mtaani ya kupigia kura, wengine kwenye vituo vya kupigia kura. Na wengine watapiga kura wakiwa mbali, wiki kabla ya tarehe ya kupiga kura.

Upigaji kura wa barua ya posta upo katika majimbo yote. Jinsi barua hizo zinavyoombwa, kupokelewa na kurejeshwa hutofautiana kulingana na Tume ya Usaidizi ya Uchaguzi ya Marekani.

Aina ya kura za barua ya posta

Shirika la Habari la Associated Press linasema hakuna tofauti kubwa kati ya upigaji kura kituoni na kutuma kwa barua, kwa kuwa zote zinahusisha kura mbayo mwisho hutiwa katika masanduku ya vituoni au mahali pengine palipoteuliwa.

Baadhi ya majimbo yanahitaji wapiga kura kutoa sababu ya kuomba kura ya posta au sahihi ya shahidi au hati nyingine kabla ya kutoa kura, na kisha ofisi ya uchaguzi hushughulikia ombi hilo na kutuma kura kwa mpiga kura.

Majimbo ya Marekani huruhusu wapiga kura kufuatilia kura zao kwa njia ya mtandao. Majimbo 31 huruhusu mtu mwingine asiyekuwa mpiga kura kurudisha karatasi ya kupigia kura baada ya kuijaza kwa niaba ya mpiga kura, na majimbo mengi hutaka mwanafamilia tu ndio anaweza kurudisha kura hiyo, jambo ambalo linakosolewa na Republican.

Majimbo 28 huruhusu upigaji kura wa aina hiyo hata bila udhuru, na majimbo manane hutuma barua ya posta kwa wapigakura wote waliosajiliwa.

Kwa jumla, majimbo 47 yanatoa fursa za upigaji kura wa mapema. Alabama, Mississippi na New Hampshire hazitoi fursa ya upigaji kura wa ana kwa ana wa mapema wala hakuna sababu kwa kura ya posta.

Kura zote katika kinyang'anyiro cha urais wa Marekani huhesabiwa, na baadhi ya majimbo huzihesabu punde tu zinapoingia, huku nyingine, kama vile Michigan na Pennsylvania, huzuia kuhesabiwa kwa kura za posta kabla ya siku ya schaguzi.

Historia ya Kura hiyo

Paul Groenke, profesa wa sayansi ya siasa katika chuo cha Reed nchini Marekani, anasema upigaji kura kwa njia ya posta umetumika kwa zaidi ya karne moja nchini humo, na ulitumiwa kwa mara ya kwanza na wanajeshi wakati wa Marekani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

"Katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe, Marekani ilijaribu kwa mara ya kwanza upigaji kura wa watu wengi wasioweza kufika kituoni wakati wa uchaguzi wa urais wa 1864 ambapo Abraham Lincoln alimshinda George McClellan - walipiga kura katika kambi na hospitali chini ya usimamizi wa makarani au maafisa wa serikali," kulingana na gazeti la Time. .

Sheria zilizotungwa na Congress wakati wa Vita vya Pili vya Dunia kusaidia kupiga kura kwa wanajeshi walio ng'ambo bado zinatumika.

Hadi mwishoni mwa miaka ya 1970, upigaji kura kwa njia ya posta ulihitaji udhuru na ulitumiwa hasa na wanajeshi, Wamerika walio ng'ambo na wanafunzi waliokuwa mbali na nyumbani, kulingana na Groenke.

Groenke anasema majimbo kadhaa yalibadilisha sheria zao ili kuruhusu upigaji kura hata bila udhuru mwishoni mwa miaka ya 1970, na kuzindua enzi ya sasa ya upigaji kura wa barua ya posta.

Mwaka 1974, Washington lilikuwa jimbo la kwanza kuruhusu mpiga kura yeyote kuomba kura ya barua ya posta kwa sababu yoyote.

Katika miaka ya 1980, California iliruhusu wapiga kura kuomba kura wa barua ya psota kwa sababu tu walipendelea kupiga kura kwa njia hiyo.

Mwaka 2000, Oregon likawa jimbo la kwanza kufanya upigaji kura wote uwe kwa njia barua ya posta, kulingana na Groenke.

Katika uchaguzi wa 1972, takriban 95% ya wapiga kura walikwenda kwenye vituo vya kupigia kura na kupiga kura wenyewe, kulingana na Associated Press. Na 90% ya wapiga kura katika uchaguzi wa 1996 walipiga katika vituo.

Idadi ya watu waliopiga kura kabla ya siiku ya uchaguzi ilipanda karibu 70% katika uchaguzi wa 2020, ambapo idadi ya kura za posta ilizidi zile zilizopigwa siku ya uchaguzi, kwa mara ya kwanza.

Uskosoaji wa Trump

Trump kwa muda mrefu amekosoa aina zote za upigaji kura isipokuwa ile ya siku ya uchaguzi, na amesema kushindwa kwake katika uchaguzi dhidi ya Biden 2020 ni kwa sababu ya kura ya posta.

Bila ushahidi alidai kuwa aina hiyo ya upigaji kura inaweza kuathiri matokeo, kulingana na shirika la habari la Associated Press.

Alizungumzia kuhusu "udanganyifu na kughushi," na mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka sabini na nane, alisema mara kwa mara bila ushahidi kwamba chama cha Democratic kiitumia upigaji kura wa posta ili kujaza masanduku ya kura wakati wa uchaguzi uliopita.

Mwaka 2022, Trump alisema, "Marekani ni kituko cha dunia linapokuja suala la uchaguzi.”

Uchunguzi katika jimbo la Georgia kuhusu madai ya ulaghai katika kura haukupata ushahidi wa kuunga mkono madai ya Trump.

Groenke anasema posta ni mfumo wa haki na usawa wa kutoa fursa kwa mtu yeyote ambaye ana shida kufikia masanduku ya kura katika siku ya uchaguzi, anasisitiza kuwa ni mfumo wa wazi kama vile kupiga kura ana kwa ana kituoni.

Licha ya kukosoa mfumo huo mara kwa mara, Trump mwenyewe alipiga kura yake huko Florida kwa barua ya posta wakati wa mchujo wa 2020 wa Republican.

Trump aliachana na kampeni yake dhidi ya upigaji kura kwa njia ya barua ya posta, baada ya kugundua kuwa kupinga kunaweza kumgharimu katika harakati zake za kurejea Ikulu ya White House, na akatangaza kuzindua mpango wa kuhimiza upigaji kura kwa njia ya posta, bila kutaja ukosoaji wake wa zamani.

Katika uchaguzi wa 2020, ambao ulifanyika huku kukiwa virusi vya Corona, wapiga kura walipendelea kupiga kura kwa njia ya posta, na mfumo huo ulipata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa Democratic, kulingana na Taasisi ya Utafiti ya Pew. Na 32% ya Warepublican pia walipiga kura kwa mfumo huo.

Groenke anasema "kihistoria, wapiga kura wengi ambao walipiga kura zao kwa njia ya posta walikuwa ni wafuasi wa Republican kwa sababu wapiga kura hawa walikuwa na umri mkubwa, elimu bora, na mapato ya juu, na watu wa aina hiyo mara nyingi huwa ni wa-Republican."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla